Nazungumzia Uhuru wa Tanganyika. Sizungumziii Uhuru wa Tanzania Bara.
Majuzi niliona mabango yaliyosambazwa jijini Dar es Salaam. Mabango hayo yalisomeka “SHEREHE ZA MIAKA 52 YA UHURU WA TANZANIA BARA”.
Hii yote ni siasa inayopotosha ukweli wa kihitoria. Wanaona ni mwiko au kinyaa kutaja jina TANGANYIKA.
Kama tujuavyo, iliyotawaliwa na wageni na iliyotafuta Uhuru ni Tanganyika. Tanzania Bara iliyozaliwa mwaka 1964 haijawahi kutawaliwa na wageni.
Ni kutokana na ukweli huo nazungumzia Uhuru wa Tanganyika ambao umetimiza miaka 52. Si Uhuru wa Tanzania Bara.
Tunapozungumzia Uhuru wa Tanganyika tunamzungumzia Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyetoa mchango mkubwa zaidi kuliko mtu yeyote mwingine katika kuutafuta Uhuru wa Tanganyika.
Hakuna anayeweza kudai kwa haki kwamba uhuru usingepatikana bila Nyerere lakini mambo mawili yako wazi. Kwamba bila Nyerere ama Tanganyika ingechelewa kupata uhuru au ingepata uhuru kwa kumwaga damu.
Ilikuwa Julai 7, 1954 Nyerere alipoongoza kikao cha Watanganyika 17 mjini Dar es Salaam, kikao kilichoanzisha chama cha kwanza cha siasa kilichoitwa “Tanganyika African National Union” au TANU.
Kikao kile kilimchagua Mwalimu Nyerere kuwa Rais wa TANU. Alikuwa Rais pekee wa TANU mpaka mwaka 1977, TANU ilipoungana na ASP kuunda Chama Cha Mapinduzi au kwa kifupi CCM.
Lengo la kwanza la TANU lilikuwa kuleta Uhuru wa Tanganyika. Kazi ya kwanza ya TANU ilikuwa kuwatayarisha Watanganyika kwa kujitawala wenyewe.
Kwa vijana ambao hawakuwapo kipindi cha kutafuta Uhuru wa Tanganyika, wazingatie kwamba harakati za kutafuta uhuru wa Tanganyika zilizoongozwa na Mwalimu Nyerere hazikuwa rahisi.
Ni kwa sababu hiyo baada ya kupatikana uhuru, Nyerere aliitwa “Baba wa Taifa” ikiwa na maana ya mtu aliyeongoza juhudi za kutafuta uhuru na ujenzi wa Taifa jipya.
Ni kweli Nyerere hakuwa mtu wa kwanza kuongoza juhudi za kutafuta uhuru. Wananchi wengi walitafuta uhuru kwa udi na uvumba enzi za Mjerumani.
Wakaishia kujiua au kunyongwa kwa kuthubutu kutafuta uhuru wa nchi yao. Basi juhudi za awali za kutafuta uhuru hazikufanikiwa kwa kukosekana umoja na silaha bora.
Nyerere alikuwa mwanahistoria. Alijua fika sababu kwa nini mababu zetu hawakufanikiwa kukomboa nchi yao.
Nyerere aligundua kuwa bila kuwa na umoja mkubwa uhuru usingepatikana. Alipogundua pia kwamba ilikuwa kazi bure kujaribu kumfukuza Mwingereza kwa kutumia silaha. Akaja na kaulimbiu ya “Umoja na Amani.”
Silaha ya umoja na amani zikatumika na zikafanikisha juhudi za kutafuta uhuru zilizoongozwa na Mwalimu Nyerere.
Nyerere alikuwa jasiri. Pia alikuwa mkweli. Kwa hiyo aliendelea na juhudi za kutafuta uhuru bila kukata tamaa. Angekuwa mtu wa kukata tamaa basi asingechelewa kuondokana na uongozi wa TANU. Makala haya yanathibitisha hivyo.
Agosti 1954, mwezi mmoja tu tangu ilipozaliwa TANU, uliitishwa mkutano wa kwanza wa hadhara wa TANU Dar es Salaam eneo la Mnazi Mmoja.
Ingawa mkutano huo ulitangazwa maeneo yote ya Dar es Salaam ulihudhuriwa na watu sitini tu! Ilikatisha tamaa.
Na huko majimboni (miaka hii mikoani) mambo yalikuwa hayo hayo. Kwa mfano, mkutano wa kwanza wa TANU uliohutubiwa na Mwalimu Nyerere mjini Masasi mwaka 1955 ulihudhuriwa na watu kumi na mmoja tu.
Safari za Mwalimu Nyerere za kuzunguka Tanganyika kueneza madai ya uhuru zilikuwa na matatizo yasiyo na idadi kwa mfano hapo mwanzoni TANU haikuwa na gari. Mwalimu Nyerere akazoea kudandia malori kutoka wilaya moja hadi nyingine.
Na Dar es Salaam Nyerere alipokuwa Mwalimu wa Pugu alizoea kutembea kwa miguu Jumamosi asubuhi kutoka Pugu mpaka Makao Makuu ya TANU ‘News Street’ (Mtaa wa Lumumba sasa). Jioni akageuza kwa miguu kurejea shuleni Pugu. Ni kwa haki kabisa kwamba barabara hiyo aliyozoea kutembea Nyerere kwa miguu akitafuta Uhuru wa Tanganyika imeitwa “Barabara ya Nyerere”.
Huko mikoani watumishi wa Serikali walitishwa na wakuu wa wilaya wasimpokee Nyerere. Ikatokea kule Mbeya, Daktari Austin Shaba wa Hospitali ya Serikali alipopata habari kuwa Nyerere amefikia kituo cha mabasi na angelala hapo, alimpeleka Nyerere nyumbani mwake. Akalala humo.
Asubuhi Mkuu wa Wilaya alipopashwa habari kuwa mtumishi wa Serikali amethubutu kumlaza Nyerere nyumba ya Serikali alitakiwa kujieleza. Akamwambia Mkuu wa Wilaya kuwa alipashwa habari kuwa Nyerere alikuwa anaumwa malaria. Kwa kuwa udaktari hauingiliwi na siasa aliona vyema amwangalie mgonjwa huyo nyumbani kwake. Akaachwa.
Machi 21, 1955 Nyerere aliporudi shuleni Pugu akitokea Umoja wa Mataifa nchini Marekani, kesho yake alitakiwa achague kuacha ualimu au siasa.
Huku akiwa hana hakika siasa ingemfikisha wapi, aliamua kuacha ualimu ili aendelee kuongoza harakati za kutafuta uhuru.
Binafsi ninaamini siku ya Nyerere ingekuwa hii Machi 22, siku aliyoamua kuacha ualimu ili ashughulikie kikamlifu harakati za kutafuta Uhuru wa Tanganyika.
Hivyo Nyerere akaacha kazi iliyokuwa ikimpatia riziki ili aendelee na juhudi zake za kutafuta uhuru. Huo haukuwa uzalendo wa kawaida.
Nyerere alipata pigo wakati mwanachama mmojawapo mwanzilishi wa TANU, Joseph Kimalando, kule Kilimanjaro, alipojitoa TANU akawa Katibu wa chama cha siasa cha Wazungu cha United Tanganyika Party (UTP) .
Mwaka 1957 Nyerere alipigwa marufuku kuhutubia mikutano ya hadhara kwa miezi sita, wakati Serikali ya Mwingereza ilipodai kuwa hotuba zake zilikuwa zikichochea raia kuchukia Serikali ya Malkia.
Mwaka 1958 aliletwa mahakamani kwa madai kuwa alikuwa amewakashifu wakuu wawili wa wilaya wa kikoloni. Akahukumiwa kutoa faini shilingi elfu tatu au kifungo cha miezi sita. Akatoa faini.
Mifano hii inatosha kuthibitsha kamba Nyerere hakufanya kazi ya kawaida katika kutafuta uhuru. Tunajua Nyerere hakuwa pekee yake. Alikuwa na mama Maria ambaye hakuhofia kuishi na mtu aliyekuwa akichukiwa na watawala.
Pia alikuwa na Bibi Titi Mohamed ambaye alilaumiwa kwa kujidai jasiri mbele ya Mwingereza. Na wengineo.