Upeo wa fikra na uwezo wa kuona mbali aliokuwa nao Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ndiyo unaotufanya tuendelee kumkumbuka leo hii kama kiongozi wa watu, tofauti na viongozi wengi wa wakati wake na pengine hata wa sasa tulionao barani Afrika, ambao kipaumbele chao katika maendeleo ni mambo mengine lakini si ustawi wa watu. 

Mwalimu aliamini katika watu, aliwatazama watu kwanza na kuwaweka mbele kabla ya vitu kwa kuamini kuwa msingi wa dhati wa maendeleo ya jamii ni watu, siyo fedha au vitu vingine ambavyo kiuhalisia ni matokeo ya kazi na fikra za watu. “…ili tuendelee tunahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.” kauli iliyozoeleka sana kusikika miaka ya nyuma hasa ya 1970 ambao bila shaka wasomaji wengi wenye umri mkubwa kidogo watakuwa wanaukumbuka vyema.

Kutokana na msingi huo, haikushangaza pale serikali yake changa iliyokuwa na miezi saba tu tangu kupata uhuru ilipoamua Julai, 1962 kuwasiliana na Serkali ya Israel ili kumpata mtaalamu wa kuja kuangalia namna bora ya kushughulikia matatizo ya afya za wananchi kupitia bima ya afya. Mwalimu bila shaka aliyajua mahitaji ya wananchi ya wakati ule na wakati ujao na mwenendo wa dunia kwa ujumla.

Dk. Channan J. Lachman, Mkurugenzi kutoka Taasisi ya Taifa ya Bima ya Israel (NII), ndiye aliwasili nchini (Tanganyika, wakati huo) kwa lengo la kufanya utafiti ili kuangalia uwezekano wa kuanzisha bima ya afya, kazi aliyoifanya Oktoba, 1962.  Serikali ilimpatia hadidu za rejea naye alifanya kazi na kuwasilisha taarifa na mapendekezo yake serikalini. 

Dhana na misingi mikuu ya mfumo wa bima ya afya, hasa bima ya afya ya kijamii (social health insurance) ni utaratibu unaolenga kuikinga jamii kutokana na madhila ya kupata huduma matibabu hasa gharama zake na namna ya kuzipata huduma hizo. Chini ya bima ya afya inatarajiwa kila mwanajamii atashiriki kuchangia kulingana na uwezo wake na atapata huduma husika kulingana na tatizo alilonalo, na kwamba kutokuwa na fedha kusiwe kikwazo cha mwanajamii huyo kushindwa kupata huduma husika. 

Mfumo wa bima ya afya ambao Mwalimu na serikali yake walioufikiria ni ule wa uchangiaji (kama huu uliopo sasa) lakini ambao ungekwenda mbali zaidi kwa kutoa kinga ya kipato kwa wale wanaougua na hivyo kuwafanya kushindwa kupata kipato cha siku kutokana na ugonjwa (kitaalamu mafao haya yalijulikana zaidi kama ‘sickness benefits’). Maana yake hapa ni kwamba mwanajamii anapougua apate huduma za matibabu na wakati huo huo apate kipato cha kumuwezesha kujikimu kipindi anachoumwa na kushindwa kufanya kazi. Huyu ndiye Mwalimu Nyerere na fikra zake pevu zilizolenga wananchi.

Baadhi ya hadidu za rejea ambazo Dk. Channan alitakiwa azifanye kazi ni kuangalia  jinsi makundi mbalimbali kama waajiri, waajiriwa, familia zao na wananchi waliojiajiri au kufanya shughuli zao mijini na vijijini namna ambayo wangenufaika na utaratibu ambao ungetumika. Kitabu kilichohaririwa na Profesa Lucian Msambichaka na Emanuel Humba (2011) kiitwacho The HistoricalDdevelopment of Health Insurance in Tanzania  pia kimegusia kuhusu utafiti huo. 

Si lengo la makala hii kuidurusu taarifa ya Dk. Channan, bali ni kuonesha namna Mwalimu Nyerere alivyokuwa na upeo wa kuona mambo, hasa yale yanayohusu maslahi na ustawi wa jamii. Wakati Mwalimu aliona umuhimu wa bima ya afya tangu mwaka 1962, leo hii bado kuna watu ama hawaelewi au hawaoni umuhimu wa bima ya afya walau hata haja ya kuijua kwa kina. 

Mwalimu alifikiria umuhimu wa kinga ya kipato kwa mgonjwa (sickness benefits) mwaka 1962, miaka 43 baadaye (ilipofika mwaka 2005), taarifa ya mshauri mwelekezi, Profesa Mariuce Olivier na mwenzake Edwin Kaseke, waliofanya mapitio ya mifumo ya hifadhi ya jamii nchini na yenyewe ikaja na mapendekezo hayo hayo kwamba mafao ya kuugua yalikuwa muhimu kutolewa kwa wananchi wa Tanzania. Kitu cha msingi hapa si kutolewa au kutotolewa kwa mafao hayo, kwa sababu hiyo inahitaji mambo kadhaa kufanyiwa kazi, lakini hoja ya msingi ni uwezo wa Mwalimu kuwa na fikra ambazo zimebaki na uhalisia wake licha ya mabadiliko ya kiuchumi na kijamii ambayo Taifa limepitia kwa zaidi ya miongo 50 tangu kupata uhuru.

Serikali ya Awamu ya Kwanza haikuishia kwenye fikra tu, ilijenga mifumo mbalimbali ya huduma hasa miundombinu ikiwamo ujenzi wa zahanati na vituo vingi vya afya mijini na vijijini. Elimu ya kinga na lishe vikapewa kipaumbele, kampeni mbalimbali za kuhamasisha kama vile Mtu ni Afya, zilifanyika kila kona na usafi wa mazingira ulipewa kipaumbele. Wanafunzi wengi pia walipelekwa kwenda kusoma nje ya nchi ikiwamo kusomea fani ya udaktari katika Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda na wengine wachache waliendelea kusoma katika Chuo cha Princess Margaret Medical School Dar es Salaam kilichokuwa kinatoa madaktari kati ya 8 hadi 20 kwa mwaka. Hatua hizi ilikuwa utekelezaji wa fikra tulizozielezea hapo awali na pia ilikuwa ni maandalizi muhimu ya utekelezaji wa mfumo wowote wa huduma za matibabu ambao Taifa lingeuchagua.  

Hatua nyingine muhimu zilizochukuliwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Akiba ya Wafayakazi (NPF) Sura 564 ya mwaka 1964 ambayo ilikuwa na kifungu kuhusu sickness benefits, ingawaje kifungu hicho hakikuwahi kutumika. Shirika la Taifa la Bima (NIC) pia lililoanzishwa 1967 ingawa nalo halikuwa na huduma za bima ya afya lakini dhamira ya Mwalimu ilikuwa dhahiri. 

Katika kipindi chote cha utawala wa Mwalimu, huduma za matibabu ziliendelea kutolewa kwa watu wote chini ya falsafa ya Azimio la Arusha, 1967 ya Ujamaa na Kujitegemea ambapo huduma zote muhimu za kijamii zilihudumiwa kutokana na mfumo wa kodi huku Serikali ikiwa ndiyo mtoaji mkuu wa huduma hizo na makundi maalumu yalipewa kipaumbele katika huduma. Mwalimu aliacha ametuwekea misingi madhubuti na muhimu ya bima za afya zilizopo na hasa wakati Taifa likijiandaa kuelekea afya bora kwa wote.

Nchi mbalimbali zinatumia ama mfumo wa kodi au mfumo wa wananchi kuchangia katika kuendesha bima zao za afya na vilevile zipo pia nchi zinatumia njia mseto mfano Korea ya Kusini. Utekelezaji wa mifumo hii unaweza kupishana au kuwa tofauti kutoka nchi hadi nyingine kutokana na utashi wa kisiasa, uwezo wa kitaalamu, maendeleo ya mifumo habari, uthubutu, utamaduni wa jamii inayohusika na utayari wa jamii hasa wafanyakazi au wenye vipato kukubali kushirikiana kwa kuwashika mkono ndugu zao wenye uwezo mdogo au wasio na uwezo kabisa. Wakati huu tukiadhimisha kumbukumbu ya miaka 17 bila Mwalimu, ni muhimu tuenzi kwa vitendo mawazo na fikra zake.

Katika bara letu bado kuna mijadala katika baadhi ya nchi hadi leo hii zinazoendelea kulumbana kama zianzishe bima ya afya au zisubiri kwanza. Nchi nyingi barani humu hazijaanzisha mfumo huu (iwe kupitia utaratibu wa fedha za kodi au kwa kuchangia kutoka katika mishahara au vipato vya wananchi). 

Kutokana na uchache wa nchi zenye mfumo huu si ajabu kusikia matokeo ya tafiti mbalimbali zikiwamo za Shirika la Afya Duniani (WHO) na Benki ya Dunia (WB) kuonesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wa Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara hawana mfumo wa uhakika wa kinga ya jamii hasa ikiwamo huduma za matibabu.

Baadhi ya nchi barani Afrika zimefanikiwa kuanzisha bima ya afya hasa miaka ya 2000, lakini nazo zinakabiliwa na changamoto kubwa kwa kuwa na wigo finyu, hivyo kuishia kuhudumia wananchi wachache sana hasa wenye uwezo na kuacha wananchi wengi wasio na uwezo nje ya utaratibu huo, ama kwa kukwepa changamoto za kuwajumuisha, au kuweka masharti magumu kutekelezeka. 

Mwalimu aliona mbali, ukiacha nafasi yake kama kiongozi, alikuwa na sifa za ziada, alikuwa msomi na mfuatiliaji wa mambo yaliyokuwa yanaendelea duniani. Kadiri siku zinavyokwenda na jinsi tunavyoendelea kutafakari falsafa zake, ninayo imani kubwa kuwa tutaendelea kujifunza mengi ili maendeleo yetu yawe ya wengi.

Tunarudia na kusisitiza tena kuwa maendeleo ya kweli ni yale yanayohusu watu wengi, na kwa mwendo huu tunaokwenda nao sasa, mbona na hili  linawezekana kabisa! 

 

Mwandishi wa makala hii ni msomaji wa Gazeti la JAMHURI anayepatikana kupitia barua pepe: [email protected]