Ni miaka 14 imepita tangu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alipofariki dunia Oktoba 14, 1999 katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas, London, nchini Uingereza.

Nyerere aliyefariki kutokana na ugonjwa saratani ya damu, alikuwa muumini mkubwa wa Ujamaa. Aliiongooza Tanzania kuanzia mwaka 1961 hadi mwaka 1984 alipong’atuka.

Ujamaa ni siasa iliyoanzishwa kwa misingi ya sera ya kuleta maendeleo ya kijamii na ya kiuchumi, baada ya Tanganyika kupata Uhuru kutoka Serikali ya Uingereza mwaka 1961.

Miaka sita baada ya Uhuru wa Tanganyika, Mwalimu Nyerere alitangaza Azimio la Arusha, azimio ambalo lilikuwa na misingi ya Ujamaa. Azimio hilo lilikuwa kama ishara ya kutambua kwamba Uhuru wa nchi na watu wake haukamiliki kutokana na kupata wimbo na bendera ya kitaifa au mawaziri na viongozi wazawa.

Mwalimu Nyerere aliamini kwamba Uhuru wa nchi uliopatikana kutoka kwa wakoloni ilikuwa ni hatua ya kwanza, ya awali kabisa, katika mchakato wa ukombozi.

Aliamini nchi haiwezi kuwa huru wakati watu wake hawako huru hivyo hiyo ndiyo sababu ya kuamua kufuata siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.

Aliamini kuwa mtu hawezi kuwa huru katika nchi ambayo inatawaliwa kimabavu na nchi ya nyingine. Pili, kuna uhuru wa watu au jamii katika nchi. Unaweza ukawa na nchi huru bila ya watu kuwa huru, kwa maana kwamba hawana uwezo wa kujiamulia mambo yao wenyewe.

Ingawa nchi yao ni huru, lakini bado wanajikuta kwamba kuna kundi au tabaka dogo la watu wanaowatawala na kufanya uamuzi kwa niaba yao, au kwa ajili ya walio wengi. Katika hali halisi, tabaka-tawala la ndani linakuwa bado chini ya himaya ya ubeberu na kwa hiyo watawala hao wanakuwa vibaraka wa matabaka-tawala ya kibeberu.

Na hali hii inasababisha si tu tabaka-tawala la ndani kuwa tegemezi, lakini hata nchi yenyewe inakuwa tegemezi kwa sababu inakosa uongozi unaojitegemea na kufanya uamuzi kwa manufaa na maslahi ya watu wake.

 

Nyerere aliamini kuwa ukombozi wa kijamii au tabaka hauwezi kupatikana bila kufanya mapinduzi ya mfumo wenyewe wa uzalishaji na utawala.

Azimio la Arusha lilitambua kwamba Uhuru wa nchi hautakuwa na maana wala hautakuwa salama kama tukiendelea kuwa tegemezi – kutegemea misaada, mikopo na uwekezaji kutoka nje. Kwa sababu mikopo haitapatikana ya kutosha na hiyo kidogo itakayopatikana itaambatana na masharti yatakayoididimiza nchi zaidi.

Nyerere alitumia Ujamaa kama msingi wa mradi wa maendeleo ya Taifa. Aliitafsiri dhana ya Ujamaa kuwa mfumo wa usimamizi wa kisiasa na wa kiuchumi kwa namna mbalimbali.

 

Ujamaa ulisaidia kuimarisha mshikamano na kujitegemea kwa Watanzania baada ya kupata uhuru.

Ustawishaji wa usawa kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa kuwapo kwa demokrasia kuu, kukomesha ubaguzi kwa misingi ya hali ya mtu, na kuzifanya sekta muhimu za uchumi kulifikia Taifa zima.

Msingi mwingine wa Ujamaa ulikuwa ni kupeleka uzalishaji katika vijiji, ambapo ilifanya uwezo wa uzalishaji wa aina zote kufanyika kwa pamoja. Katika uhai wake, Mwalimu Nyerere aliwataka Watanzania wajifunze kujikomboa kutoka kwa utegemezi wa nchi za Ulaya.

Mwalimu Nyerere alitaka Watanzania wajifunze kufanya mambo wenyewe na kujifunza kuridhika na kile ambacho wangeweza kufikia kama nchi huru. Utekelezaji wa elimu bila malipo na ya lazima kwa Watanzania wote, ili kuwahamasisha wananchi kuhusu kanuni za Ujamaa.

Uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere uliivutia Tanzania macho na heshima ya kimataifa, kutokana na msisitizo wake wa maadili kama msingi wa uamuzi wa siasa.

Wakati wa uongozi wa Mwalimu Nyerere, Tanzania ilipiga hatua kubwa katika vipengele mbalimbali vya maendeleo. Vifo vya watoto vilipungua kutoka 138 kwa kila 1,000 waliozaliwa hai mwaka 1965 hadi 110 mwaka 1985.

Matarajio ya kuishi yalipanda kutoka miaka 37 (1960) hadi 52 (1984). Uandikishaji wa wanafunzi katika shule za msingi ulipanda kutoka asilimia 25  mwaka 1960 hadi asilimia 72 kwa mwaka 1985.

Hata hivyo, kutokana na ongezeko la watu asilimia ya watu wazima waliojua kusoma na kuandika ilipanda kutoka asilimia  17 mwaka 1960 hadi asilimia 63 mwaka 1975.

Nyerere alitangaza kuwa atang’atuka uongozi kitaifa asigombee tena urais katika uchaguzi wa mwaka huohuo.

Maisha yake

Julius Kambarage Nyerere alizaliwa mwaka 1922 katika Kijiji cha Butiama, Wilaya ya Musoma, mkoani Mara.

Alikuwa mmoja wa watoto 26 wa mzee Nyerere Burito, chifu wa kabila la Wazanaki.

Alipokuwa mdogo Nyerere alichunga mifugo ya baba yake na  alipofikisha umri wa miaka 12 aliingia shule iliyokuwa umbali wa kilomita 30 hadi Musoma. Baada ya kumaliza masomo ya shule ya msingi aliendelea na masomo katika Shule ya Wamisionari Wakatoliki Tabora.

 

Katika umri wa miaka 20 alibatizwa akawa Mkristo Mkatoliki hadi mwisho wa maisha yake.

Walimu wake baada ya kuona ana akili sana, walimsaidia kusomea ualimu katika Chuo Kikuu cha Makerere, Kampala, Uganda kuanzia mwaka 1943 hadi 1945. Akiwa Makerere alianzisha tawi la Umoja wa Wanafunzi Watanganyika, pia alijihusisha na tawi la Tanganyika African Association (TAA).

Baada ya kumaliza masomo ya ualimu, alirudi Tabora akafundisha katika Shule ya St. Mary. Mwaka 1949 alipata ufadhili na kwenda kusoma katika Chuo Kikuu cha Edinburgh, Uingereza na kupata shahada ya M.A. ya Historia na Uchumi.

Alikuwa Mtanganyika wa kwanza kusoma katika Chuo Kikuu cha Uingereza na wa pili kupata shahada ya elimu ya juu nje ya Tanganyika. Aliporejea nchini, alifundisha Historia, Kiingereza na Kiswahili katika Shule ya Mtakatifu Francis sasa Sekondari ya Pugu Dar es Salaam.

Mwaka 1953 alichaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Tanganyika African Association (TAA), ambacho alisaidia kukijenga alipokuwa mwanafunzi Makerere. Mwaka 1954 alibadilisha jina la chama cha TAA na kuwa Chama cha Tanganyika African National Union (TANU), ambacho pia kilikuwa cha kisiasa zaidi kuliko TAA.

Ndani ya mwaka mmoja TANU ikawa tayari chama cha siasa kinachoongoza nchini Tanganyika.

Uwezo wa Nyerere uliwashtua viongozi wa kikoloni, akalazimika kuchagua kati ya siasa na kazi ya ualimu.

 

Nyerere alisikika akijisemea kuwa alikuwa mwalimu kwa kuchagua na mwanasiasa kwa bahati mbaya.

Alijiuzulu ualimu na kuzunguka nchi nzima kuzungumza na watu wa kawaida na machifu ili kuleta umoja katika kupigania Uhuru. Pia alizungumza kwa niaba ya TANU katika Trusteeship Council na Fourth Committee ya Umoja wa Mataifa (UN) huko New York.

Uwezo wake wa kuzungumza na wa kuunganisha watu ulimwezesha kufanikisha Uhuru wa Tanganyika bila umwagaji damu.  Ushirikiano mzuri aliouonesha aliyekuwa Gavana wa wakati huo, Sir Richard Turnbull, ulisaidia pia kuharakisha upatikanaji wa Uhuru.

Nyerere aliingia katika Bunge la kikoloni mwaka 1958 na kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu mwaka 1960. Desemba 9, 1961 Tanganyika ilipata Uhuru na Nyerere alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika huru; mwaka mmoja baadaye akawa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Tanganyika.


Nyerere alikuwa kiungo muhimu katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kutengeneza Tanzania mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964 yaliyomtoa madarakani Sultani wa Zanzibar, Jamshid bin Abdullah.

 

Februari 5, 1977 aliiongoza TANU kuungana na Chama cha siasa Zanzibar, Afro-Shirazi (ASP) na kuanzisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwa mwenyekiti wake wa kwanza.

Nyerere aliendelea kuongoza Taifa hadi mwaka 1985 alipong’atuka na kumwachia nafasi Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi.

Aliacha kuongoza Tanzania ikiwa ni mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani, ingawa yenye huduma za elimu na afya zilizoenea kwa wananchi wengi. Hata hivyo, aliendelea kuiongoza CCM hadi mwaka 1990 na kuwa na athari kubwa katika siasa ya Tanzania hadi kifo chake.

Nyerere alikaa muda mwingi kijijini kwake Butiama akifanya kazi za shambani. Pamoja na haya, alianzisha Taasisi Mwalimu Nyerere mwaka 1996 na alikuwa  mpatanishi wa sehemu mbalimbali zilizokuwa na machafuko na vita za wenyewe kwa wenyewe kama  Burundi.

Mafanikio

Kati ya mafanikio makubwa ya Nyerere ni kujenga umoja wa Taifa kati ya watu wa makabila na dini tofauti, na hivyo kudumisha amani ya muda mrefu, tofauti na hali ya nchi jirani, iliyofanya Tanzania iitwe “kisiwa cha amani”.

Pia Mwalimu Nyerere alistawisha utamaduni wa Kiafrika pamoja na lugha ya Kiswahili, kushinda ubaguzi wa rangi, kutetea usalama wa Taifa letu katika vita dhidi ya nduli Idi Amin wa Uganda.

Mwalimu alitoa mchango mkubwa kwa vyama vya ukombozi vya nchi za kusini mwa Afrika kama vile Zimbabwe (ZANU), Afrika Kusini (ANC na PAC), Namibia (SWAPO), Angola (MPLA) na Msumbiji (Frelimo).