Katika siku za hivi karibuni, nimekuwa nakumbuka wimbo niupendao wa gwiji la muziki, Ramadhani Mtoro Ongala ‘Dk Remmy’, ‘Narudi nyumbani’.
Aliimba kuwa anarudi Songea, anarudi Mlale, anarudi kijijini kwa sababu maisha ya Dar es Salaam yamemshinda, akikiri kuwa nyumbani ni nyumbani tu hata kama kubaya.
Anaendelea kutaja shughuli ambazo atazifanya kijijini kama vile anaanza kukubali uhalisia na tofauti ya maisha ya kijijini kulinganisha na yale ya mjini.
Wapo wanaoamua kurudi kijijini kwa sababu ya ugumu tu wa maisha ya mjini, lakini wapo wanaorudi nyumbani bila kulazimika kufanya hivyo. Ni kweli, sababu zinazohusiana na urahisi wa maisha zipo. Nimewahi kutaja kuwa ninapofanya kazi hapa kijijini, sina gharama ya usafiri kutoka nyumbani mpaka ofisini kwa sababu natembea kwa mguu na inanichukua chini ya dakika tano kufika ofisini.
Lakini nilisema hayo kabla sijahamishia ofisi chumbani kwangu. Kwa kazi zile ambazo ni za mezani tu na hazihitaji kutoka nje, muda wa kutoka kitandani mpaka kufikia meza yangu ya kazi ni hatua mbili tu.
Licha ya ukaribu wa nyumbani na maeneo ya kazi au uzalishaji, umuhimu mkubwa zaidi wa kurudi kijijini ni ule mchango mkubwa wa hali na mali unaoweza kutolewa kijijini na wale ambao wametapakaa sehemu nyingi nchini au ulimwenguni kujiongezea elimu, uzoefu, na maarifa mbalimbali.
Ni vyema kuwa wanawakumbuka jamaa zako kijijini ambao huwatembelea wanapopata likizo, na kuhakikisha kuwa wanapata pesa ya matumizi na mahitaji mengine ya lazima. Wanaweza kuwatembelea mara moja kwa mwaka, lakini kuwaacha mwaka mzima wanabadilishana mawazo wao kwa wao tu. Hawana jipya. Kama ni mawazo mabovu itakuwa wanaongezana ujinga tu. Lakini hata kama ni mawazo mazuri, mwanadamu hawezi kuishi kwa mawazo yale yale kila wakati, pamoja na kwamba yapo masuala ya msingi ambayo huwa hayabadiliki sana.
Tatizo la jumuiya ya watu, hasa kijijini, kuishi miaka nenda miaka rudi bila kuwa na mchango wa mawazo kutoka kwa jamii nyingine nchini, au hata nje ya nchi ni kukosekana kwa mawazo mapya ya kukabiliana na changamoto za maisha yao.
Sijengi hoja yangu kwa kuihusisha sana na suala la kutokuwa na elimu na maarifa, kwa sababu naamini pia kuwa hata wale wenye elimu na maarifa wanaoishi kijijini wanaweza kujikuta wanaoishi ndani ya ukuta unaozuwia kupenya kwa mawazo mapya yenye kuchangamsha upeo wao wa uelewa. Matokeo ni kuwa baada ya muda utakuta yule wa darasa la nne, au ambaye hajasoma kabisa, hatofautiani sana na yule aliyepata elimu nzuri na uzoefu wa kutosha. Na tofauti hii haimpandishi yule aliyesoma kumkaribia yule ambaye hakusoma, bali itamshusha yule aliyesoma kumkaribia yule ambaye hajasoma.
Kipo kikomo juu ya kiasi gani Serikali inaweza kuleta maendeleo kwa wananchi wake. Inaweza kuwekeza kwa kila hali, na kwa mamilioni ya pesa, lakini iwapo watakosekana watu ambao wana elimu na uzoefu uliopatikana kutoka maeneo mbalimbali, basi maendeleo yanayotarajiwa kijijini hayawezi kushika kasi ya kuridhisha.
Nimeshuhudia watu waliohamia vijijini na kuona jinsi gani mawazo yao, bila kusahau pesa yao, yanavyoweza kuleta mabadiliko chanya kwenye eneo ambalo lingeonekana kuwa halina nafasi ya kuendelea. Lakini, kama nilivyosisitiza, suala la msingi zaidi ni mawazo yaliyopevuka na ambayo yanamsaidia yule mtu ambaye ameishi kijijini kwa muda mrefu kufunguliwa macho na kuona fursa ambazo labda zilikuwa hazionekani kwake, au kuona namna bora ya kufanya kazi ya aina fulani ambayo awali hakuifanya kwa ufanisi.
Ipo faida nyingine. Mara nyingi ni wale ambao wametoka kijijini ndiyo wenye kelele zaidi kwa Serikali ya kuboresha maisha duni ya wanaoishi kijijini. Wanapoishi kijijini wanakuwa na sauti kubwa zaidi ya kuhimiza Serikali na mamlaka mbalimbali kutekeleza kwa ufanisi mipango ya maendeleo. Uanaharakati si tu kukosoa utendaji wa Serikali; uanaharakati unaweza pia kuwa kuhimiza nini kifanyike na Serikali ili kuhudumia vyema zaidi wananchi. Na uanaharakati wa aina hii unaweza kufanyika vyema zaidi na Watanzania wengi ambao wameng’ang’ania mijini na kuwaacha jamaa zao vijijini bila msaada.
Wakati mwingine, lipo tatizo la wale wenye dhamana ya kusikiliza kutosikia. Wanaharakati ninaozungumzia mimi watakuwa ni wale ambao wamejenga uzoefu wa kuzibua masikio yaliyojaa nta.
Haipingiki ya kuwa siyo kila mtu ambaye anaweza kuhamia kijijini kwa urahisi, ingawa naamini asilimia moja tu ya Watanzania wenye elimu nzuri na uzoefu wakirudi kijijini maendeleo ya nchi yataongezeka kwa kasi kubwa. Na mabadiliko ya kila siku ya teknolojia sasa yanaruhusu aina nyingi za kazi kufanyika popote hata bila mhusika kulazimika kuwapo ofisini wakati wote. Kuna aina nyingi za kazi ambazo hazihitaji kabisa mhusika kuwapo ofisini.
Tatizo la watu kung’ang’ania mijini halihusu kutokuwapo kwa ajira peke yake. Wakati mwingine linajengeka kwa woga tu wa watu waliozowea kuishi mjini kwa muda mrefu kutoona namna gani wanaweza kuishi tena kijijini. Woga huo unapoondoka, uamuzi wa kuishi tena kijijini unapungukiwa vikwazo.
Sitaki kujenga taswira kuwa ni rahisi kuchukua hatua ya kuhamia kijijini. Siyo wote wanaoishi vijijini watakubali kwa urahisi mawazo ya mtu aliyeishi mjini kwa muda mrefu na ambaye anajaribu kuwashawishi wafanye jambo kwa namna tofauti, au wachukue hatua fulani ambazo hawajawahi kuchukua.
Kwa sababu hiyo ni muhimu kubaki wanyenyekevu wakati wote na kukumbuka kuwa sote ni wanadamu kwanza. Elimu, uzoefu, na maarifa vinakuja baadaye. Na ukweli, ni kuwa siyo wote wanaoishi kijijini ni wajinga. Suala la kujifunza linaweza kujitokeza kwa pande zote mbili. Cha msingi ni kuwa sisi wa kijijini tunaweza kujifunza mengi zaidi kutoka kwa wengine kuliko yale ambayo tunaweza kuwafundisha wengine. Dunia ni kubwa sana kuliko kijiji.