Na Cresensia Kapinga,JamhuriMedia,Ruvuma

Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya ya Nyasa na Mbinga zilizopo mkoani Ruvuma wamekemea baadhi ya wazazi wenye watoto waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu ambao hawajawapeleka shule kwa visingizio mbalimbali visivyokuwa na msingi wawapeleke shule haraka iwezekanavyo kabla mkono wa sheria haujawapitia.

Hayo wamesema jana kwa nyakati tofauti wakati wakizungumza na waandishi wa habari waliotembelea Halmashauri hizo kwa lengo la kujua idadi ya wanafunzi wa msingi na sekondari walioandikishwa na kushindwa kuripoti shuleni.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Bw. Jimson Mhagama amesema kuwa kuna wazazi wanatabia ya kuwapeleka watoto shambani kwa lengo la kwenda kulima kwenye mashamba ya wazazi ama kuwa vibarua hivyo amewaagiza viongozi kuanzia ngazi ya shina hadi kata pamoja na watendaji wa vitongoji na vijiji kuendesha msako ambao utapita kila nyumba na watakaobainika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Amesema kuwa Halmashauri yake ilipangiwa kupokea jumla ya wanafunzi wa kidato cha kwanza 4452 lakini hadi Januari 17 mwaka huu wamepokea wanafunzi 1201 sawa na asilimia 27 ambapo kwa upande wa Elimu msingi kwa darasa la awali walitarajaia kuandikisha wanafunzi 5484 lakini hadi Jana wameandikisha watoto 5444 sawa na asilimia 96 ya lengo.

“Hakuna sababu ya wazazi kuwakataza watoto wao wasiende shule kwani kupitia Serikali ya Awamu ya Sita inayoongoza na Rais Samia Suluhu Hassan inatoa elimu bure lakini pia hatuangalii kipengele cha mtoto hana sale ya shule ama kiatu sisi tunachotaka mwanafunzi aje kuripoti akiwa na daftari pamoja na kichwa basi na si vinginevyo” amesema Mkurugenzi Mhagama.

Wanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari ya Mbinga Day wakiwa darasani baada ya kuripoti shuleni hapo

Naye kaimu Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Mbinga Lucy Luwungo amesema kuwa walipangiwa jumla ya wanafunzi 2721 wa kidato cha kwanza walioripoti hadi kufika Januari 16 walikuwa 1147 sawa na asilimia 42.2 na ambao bado hawajaripoti 1574 sawa na asilimia 57.8. 

Amefafanuwa zaidi kuwa tayari wamejiwekea mikakati kwa wakuu wa shule zote za sekondari kutangaza maeneo mbalimbali kama makanisani na msikitini kwa lengo la kuwakumbusha wazazi wawapeleke watoto shule.

“Kuna shule watoto 13 ndo walioriporti shule ya sekondari ya Dkt. Shein ipo Kata ya Mpepai kati ya watoto 242 kwa hiyo wasioriporti wapo 219 changamoto kubwa watoto wapo shambani na wazazi wao lakini pia tumeandika barua kwa maafisa watendaji na waratibu elimu kata wafuatilie hao wazazi wa watoto ambao hawajawaleta watoto shuleni na kuwapeleka mahakamani.” amesema Luwungo.

Aidha amesema kuwa wanachohitaji wao ni kichwa na daftari tu basi hayo mengine hawaangalii pia wametoa maelekezo kwa wazazi hata usipokuwa na chakula mtoto aende tu akaripoti.