*Ni wiki moja baada ya vigogo 5 kusimamishwa

*Yaelezwa lengo ni kupoteza ushahidi wa ufisadi

*Majaar akomaa, Nyalandu alinda watuhumiwa

Nyaraka kadhaa muhimu zinazohusu ufisadi ndani ya Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro (NCAA), zimechomwa moto ndani ya ofisi.

Tukio hilo limetokea wiki moja tu baada ya Bodi ya NCCA, chini ya Balozi Mwanaidi Majaar, kuwasimamisha kazi vigogo watato kwa tuhuma za ufidadi, wizi na matumizi mabaya ya ofisi.

Habari za uhakika zinasema kuchomwa kwa nyaraka hizo, ingawa chanzo chake hakijatajwa rasmi, kunahusishwa moja kwa moja na kuondolewa kwa vigogo hao ambao wanatuhumiwa kuisababishia NCAA hasara ya mabilioni ya fedha kupitia zabuni, ununuzi, kughushi safari na malipo hewa.

Waliosimamishwa ni Mkurugenzi mmoja, mameneja watatu na Mkaguzi Mkuu wa Ndani; huku wengine kadhaa wakipewa onyo.

Bodi ya NCAA iliyoketi katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam mnamo Novemba 4, mwaka huu, ilifikia uamuzi wa kuwasimisha vigogo hao licha ya kupata upinzani mkali kutoka kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu pamoja na mjumbe mwingine mwanaume anayetajwa kuwa na ‘uhusiano wa kijamii’ na mmoja wa watuhumiwa wakuu katika ufisadi huo.

Waliosimamishwa na vyeo vyao kwenye mabano ni Injinia Joseph Mallya (Mkurugenzi wa Uendeshaji), Veronica Ufunguo (Meneja Huduma za Utalii), Amiyo Amiyo (Meneja Huduma za Uhifadhi), Dk. Justine Muumba (Meneja Maendeleo ya Jamii) na Elinipendo Mwambo ambaye ni Mkaguzi Mkuu wa Ndani.

Walioteuliwa kukaimu nafasi zao ni Peter Makutian (Kaimu Huduma za Utalii), Israel Naaman (Kaimu Meneja Huduma za Uhifadhi), Dk. Kuya ole Sayalel (Kaimu Meneja Maendeleo ya Jamii); na Alex Maleva (Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Ndani).

Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA, Balozi Majaar, anayesifika kwa misimamo ya kizalendo, amethibitisha kuwapo kwa tukio la kuchomwa kwa nyaraka za Mamlaka hiyo.

Hata hivyo, ameliambia JAMHURI kuwa tukio hilo haliwezi kukwamisha mkakati wa kujua ukweli wa tuhuma za ufisadi zinazowakabili watumishi wa NCAA, na kwamba uchunguzi utaendelea.

Kwa siku kadhaa, maofisa kutoka vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama wamekuwapo Ngorongoro wakiendesha uchunguzi wa tukio hilo.

Hayo yakiendelea, Nyalandu amefungua milango kwa waliosimamishwa kukata rufaa kwake kama wanaona wameonewa.

 

Uamuzi wa Bodi

 

Bodi imeagiza Menejimenti ya NCAA ihakikishe Polisi wanashirikiana na Mwenyekiti wa Tume Maalumu iliyokagua NCAA na mawakili wa nje ya Mamlaka hiyo ili kufanya uchunguzi na hatimaye watuhumiwa wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria.

Aliyekuwa Mhifadhi wa NCAA, Bernard Murunya, Bodi imesema anaweza kuchukuliwa hatua za kisheria kutokana na kutosimamia vema majukumu yake na kuisababishia hasara kubwa NCAA.

Kwa sababu hizo, Bodi imetupa mzigo huo kwa mamlaka husika ili ziweze kumchukulia hatua za kisheria kadri inavyofaa. Kwa sasa Murunya ni Mbunge katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Shaddy Kyambile, naye ametajwa na Bodi kuwa anapaswa kuchukuliwa hatua kutokana na kutowajibika barabara na hivyo kuisababishia NCAA hasara. Uamuzi kama huo umetakiwa pia uchukuliwe kwa aliyekuwa Mhasibu Mkuu, Simon Kalembo.

Wakurugenzi na Mameneja wengine nao wametakiwa wafike mbele ya Bodi wajieleze kutokana na kukabiliwa na tuhuma za uzembe na kutowajibika. Nao ni Bruno Kawasange, Joseph Mshana, Injinia Isra Missana, Patrice Mattay na Adam Akyoo.

Bodi imewataka wote waliochukua, au waliotumia mali za NCAA vibaya wazirejeshe mara moja.

Katika hatua nyingine, aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi NCAA, Leonard Minzi, alistaafu Novemba 8, 2014. Johnson Saiteu Laizer ameteuliwa kuwa Kaimu Meneja wa Kitengo cha Uratibu wa Ununuzi. Uteuzi huo ulianza jana, Novemba 9.

Kikao cha Bodi ya NCAA kilichoketi Novemba 4, mwaka huu; pamoja na Mwenyekiti Balozi Majaar, wajumbe wengine waliohudhuria ni Donatus Kamamba, Lucas Selelii, Lukonge Mhandagani, Juma Pinto, Dk. David Mrisho, Laban Moruo, Metui ole Shaudo, Dk. Aikande Kwayu, Francis ole Siapa na Dk. Freddy Manongi (Katibu wa Bodi na Mhifadhi wa NCAA). Mjumbe mwingine, Job Ndugai hakuhudhuria.

Wakati wa kujadiliwa kwa dondoo ya viongozi wanaopaswa kuwajibishwa, wajumbe wanne walitangaza mgongano wa maslahi kutokana na kuwapo kwao kwenye Bodi iliyopita ambayo kimsingi ufisadi huo ulifanyika chini ya uongozi wake. Wajumbe hao ni Shaudo, Selelii, Moruo na Kamamba.