Kocha wa Riadha wa Timu ya Taifa la Brunei, ambaye pia amepata kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Suleiman Nyambui, amekishauri Chama cha Riadha kuwekeza nguvu nyingi katika ujenzi wa misingi mizuri kwa watoto wenye vipaji.

 

Amesema mchezo wa riadha ni miongoni mwa michezo ambayo ikipata uangalizi mzuri unaweza kuzalisha ajira nyingi kwa vijana katika nchi yoyote ile na kugeuka kuwa mamilionea ndani ya miaka michache.

Akizungumza na JAMHURI, mkongwe huyo ambaye kwa sasa ni kocha wa timu ya taifa ya riadha nchi ni Brunei, amesema wakati umefika kwa vyama vya michezo nchini kuisaidia Serikali kuzalisha ajira kupitia michezo.

“Tanzania kuna vipaji vya kila michezo na kama vingepatiwa elimu na kuandaliwa kwa usahihi, nina uhakika mataifa mengi yangetuheshimu linapokuja suala la michezo,” amesema Nyambui.

Amesema yote yatawezekana endapo RT kwa kushirikiana na Serikali pamoja na wadhamini watajitokeza  na kuunganisha nguvu kwa ajili ya kuwasaidia vijana wenye vipaji.

 

“Niombe Serikali yangu chini ya Rais John Magufuli kutoa msisitizo katika suala zima la michezo ili vijana wapate ajira kupitia michezo,” amesema Nyambui.

Amesema yeye ni mfano, kwani amepata kazi nje ya nchi kwa ajili ya rekodi yake nzuri aliyoiweka miaka ya nyuma wakati Tanzania ilipokuwa katika ubora wake katika riadha.

Amesema pamoja na RT kujitahidi kwa miaka mingi, lakini imejikuta ikilemewa na mzigo mzito na kuhitaji msaada; kwa hiyo ni jukumu la wadau wote wapenda michezo kuingilia kati kwa manufaa ya michezo huo.

 

“Tanzania ina medali mbili kutoka katika Michezo ya Olimpiki ilizopata Moscow, Urusi mwaka 1980 kupitia kwa Filbert Bayi na Suleiman Nyambui ni miaka zaidi ya 36,” amesema Nyambui.

Amesema miaka hiyo yote Tanzania imekuwa ikishiriki mashindano ya dunia ya riadha, lakini imekuja kupata medali  mwaka 2005, yaani miaka 12 iliyopita nchini Finland katika mji wa  Helsinki.

“Ni lazima kama Taifa tujiulize maswali magumu juu ya mustakabali wetu juu ya kwa nini tupo hapa tulipo tangia miaka yote hiyo bila ya kupiga hatua kuelekea waliko wenzetu,” amesema Nyambui.

 

Amesema hakuna nchi yoyote duniani iliyopiga hatua katika michezo  bila ya serikali kutia mkono ukizingatia kuwa michezo katika miaka ya hivi karibuni imekuwa ni ajira kubwa.

“Serikali inapotangaza kutengeneza ajira ni bora ikaiangalia sekta ya michezo kwa jicho pevu kwa kuwa  ina uwezo wa kuzalisha ajira kwa vijana wengi kwa wakati mmoja,” amesema Nyambui.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa RT, Wilhelm Gidabuday, amesema  katika kuhakikisha riadha inarudi katika ubora wake  tayari Shirikisho limeshakamilisha utekelezaji wa kozi maalumu ya mchezo wa riadha kwa watoto ‘Kids Athletics’.

 

Gidabuday amesema  mpango huo maalumu wa kuzalisha wakufunzi wa riadha kwa watoto umewezeshwa na Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF) na unalenga kuwajengea uwezo watoto wadogo wenye vipaji.

“Mpango huo uliokuwa chini ya Mkufunzi anayetambulika na IAAF, Dk Ahmand Ndee, ulienga kuvumbua vipaji vya mchezo huo kwa ajili ya miaka ijayo,” amesema Gidabuday.

Amesema wanafanya kila linalowezekana kuweza kuzunguka nchi nzima ili kupata watoto wenye vipaji ili kuweza kupata vijana wenye uwezo wa kuja kulitumikia Taifa katika miaka ijayo.

“Tayari kama wasimamizi wakuu wa mchezo wa riadha, tunayo mipango ya muda mrefu na mfupi lengo likiwa ni kuiona nchi ikirudi katika zama zile za akina Filbert Bayi, Suleiman Nyambui, Juma Ikangaa na wengine wengi waliokuwa gumzo duniani katika riadha,” amesema Gidabuday.