Kwa mara nyingine tumeshuhudia Tanzania ikichafuliwa tena na kudhalilishwa na Wazungu mbele ya uso wa dunia. Safari hii wamarekani kupitia asasi ya Environmental Investigation Agency (EIA) wameibua aibu kubwa ya ujangili wakihusisha vigogo wa serikali yetu na Rais wa China.
Wanadai kuwa hakuna hatua zozote zinazochukuliwa dhidi ya watuhumiwa wa ujangili wakiwamo wale waliokamatwa. Serikali ya Tanzania tayari imetoa taarifa kukanusha habari hizi kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe.
Membe ana hoja ya msingi sana pale anapohoji kwa nini hawa Wamarekani waandike kashfa hizi leo baada ya ziara ya Rais Kikwete nchini China. Ni wazi kuwa hii ni vita. Wamarekani wameshajihakikishia kuwa Tanzania ni shamba lao kwa ajili ya kuvuna rasilimali za madini, gesi na wanyamapori.
Leo hii linapoibuka Taifa jingine na kutamani kushirikiana na Tanzania, linaonekana kama tishio na hivyo lazima mbinu chafu zitafutwe kudhibiti hali hii. Hata hivyo, pamoja na matusi haya ya asasi ya Kimarekani, ni vema tukajihoji wenyewe – Je, si sisi tunaosaidia kutukanwa na kudhalilishwa na hawa Wazungu?
Kashfa kama hii ni ya pili baada ya ile iliyoibuliwa na Mwandishi wa Gazeti la The Daily Mail on Sunday la Uingereza, Martin Fletcher, Februari mwaka huu. Itakumbukwa kuwa Serikali ililaani taarifa zile na kutishia kuchukua hatua za kisheria. Kikafanyika kituko cha mwaka pale Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alipokurupuka na kumwalika Fletcher na mwenzake kwa gharama za walipa kodi wa Tanzania! Akampa malazi na chakula pale Serena, akatoa ndege ya Serikali kumpeleka Selous kutalii na mwisho akamruhusu kuvunja sheria kwa kuingia na kupiga picha kwenye ghala la nyara (Ivory Room)!
Matokeo ya ziara ya Fletcher, ambaye hata yeye mwenyewe alidai kushangazwa na mwaliko wa Nyalandu, yalikuwa aibu kubwa zaidi kwa Taifa. Kadhia hii ilipohojiwa bungeni, Nyalandu akatoa majibu ya rejareja kuwa alilazimika kufanya hivyo ili kumsaidia Fletcher aweze kuandika a balanced story! Hadi leo, ukiacha magazeti (ambayo Nyalandu amekuwa akidai kuwa ni ya kufungia vitumbua), hakuna mamlaka iliyowahi kumtaka Nyalandu kuwajibika kwa kashfa hii kana kwamba hili lilikuwa jambo la kawaida tu.
Kama vyombo vya nje vinapoandika kashfa ya kuidhalilisha Serikali vinazawadiwa, na pengine kupewa fursa ya kutuvua nguo zaidi, kwa nini EIA wasiione hii kama FURSA adhimu na kuitumia? Je, kama alivyofanya kwa Fletcher, Nyalandu atawaalika hawa Mabwana waje kula kuku ili waandike a balanced story!
Nashawishika kuamini kuwa sababu nyingine ya kiburi cha Wazungu inayosababisha wafikie kutumia mbinu chafu kama hii kuharibu taswira ya Tanzania mbele ya uso wa dunia na uhusiano wake na mataifa mengine wanayoyachukia ni kutokana na wao kuamini kuwa wamewanunua na kuwaweka mfukoni baadhi ya viongozi wa Serikali yetu.
Nimekuwa nikijiuliza mara nyingi, inakuwaje Waziri wa Maliasili na Utalii anatumia muda wake mrefu nchini Marekani kuliko Tanzania? Anafuata nini huko kila siku? Tumesoma kwenye mitandao ya jamii na magazeti tuhuma kuwa Nyalandu anatumikia ‘interests’ za Marekani na kwamba hii imemfanya awe na kiburi kilichotamalaki. Baada ya Nyalandu kuwafutia umiliki GMS kwa sababu za kutatanisha alikimbilia Marekani siku iliyofuata akampa kazi Peter Msigwa kujialika kwenye vyombo vya habari kumsifu! Gazeti moja limeripoti kuwa baada ya Nyalandu kukwama kuzuia uhamisho wa wateule wake kutoka wizarani, alikimbilia ubalozi wa Marekani kuichongea Ikulu!
Katika taarifa za EIA, Nyalandu anatajwa kama mwajibikaji anayekwamishwa na baadhi ya vigogo kwenye chama na Serikali. Aidha, katika matamshi yake ya karibuni Nyalandu amenukuliwa akilalamika kuwa dhamira na kasi yake ya kupambana na ujangili vinakwamishwa na watendaji wizarani kwake na baadhi ya viongozi wenzake serikalini.
Je, kufanana huku kwa walichoandika EIA na madai ya Nyalandu, hakutoi picha kuwa Nyalandu anaweza kuwa chanzo cha taarifa hizi ili aweze kutimiza wajibu wake kwa Wamarekani? Hapa lazima Nyalandu abanwe awataje hawa anaowatuhumu kuhujumu juhudi zake za kupambana na ujangili. Sitarajii aje na zile ngonjera za majangili wake 320 ambao alidai kuwa anawajua mpaka utaifa wao, lakini baadaye akaruka eti wao kama watu hawajulikani lakini vitendo vyao!
Tumeshuhudia Nyalandu, bila kujali athari za kidiplomasia, alivyotumika kuzuia shughuli ya uwindaji kwa familia ya kifalme kutoka Emirates na kusababisha familia hiyo iliyokuwa nchini tayari kufunga virago. Bila shaka hii kwake imempa credits kutokana na chuki ya Wamarekani dhidi ya Waarabu! Hoja ya Nyalandu kuzuia utalii huo ni kile alichodai kuwapo kesi mahakamani iliyohusu kitalu walichoomba kuwinda. Akadai kuwa asingependa kuingilia uhuru wa Mahakama. Hata hivyo, Nyalandu huyu huyu, chini ya mwezi, akanyang’anya kitalu hicho kutoka kwa mmiliki halali na kukigawa kwa Wamarekani! Je, uhuru wa Mahakama hapa ulienda likizo? Ninajiuliza, kama Nyalandu hakujali kudorora kwa uhusiano wetu na Emirates kwa sababu ya maslahi ya Wamarekani, leo hii kitu gani kitamzuia kutumiwa na Wamarekani hawa hawa kuharibu uhusiano wa Tanzania na China?
Nyalandu amekuwa akitajwa kuwa na uhusiano wa karibu na kampuni za kimarekani kiasi cha kupokea amri na kuzitekeleza bila kujali kuwa anavunja sheria za nchi. Inasemekana kuwa kampuni hizoa sasa zinajigamba kuongoza wizara na kutoa amri kwa Nyalandu kufanya kila wanachotaka. Tujiulize, Nyalandu anafanya hivi bure? Hakuna anacholipwa?
Kampuni hizi za kimarekani zimeelezwa kuivuruga sana tasnia ya uwindaji wa kitalii nchini kutokana na ubabe wa wakurugenzi wake. Kampuni hizi zimeikosesha Serikali mamilioni ya dola za Marekani kutokana na vurugu na majaribio ya kutaka kupora vitalu kutoka kwa wamiliki halali. Kampuni hizi zimeishtaki Serikali mara kadhaa na kushindwa kesi, lakini bado zinaendelea kuisumbua Serikali.
Mara tu baada ya Balozi Khamis Kagasheki kujizulu uwaziri, wenye kampuni hizi walishangilia hadharani wakimtaja Kagasheki kama mtu aliyekosa weledi na wakati huo huo wakitoa ndege zao na pesa kumwezesha Nyalandu azunguke nchi nzima kuuhadaa umma kuwa ndiye aliyestahili kuvaa viatu vya Kagasheki.
Miongoni mwa mambo aliyofanya Nyalandu kuthibitisha utii wake kwa Wamarekani ni kunyang’anya kwa hila vitalu vilivyomilikishwa kihalali kwa kampuni nyingine na kuvitoa kwa Wamarekani. Wakati anaifutia kampuni moja umiliki wa vitalu kwa madai ya kukiuka sheria za uwindaji kwa kuwindisha watoto wadogo, yeye katoa Leseni ya Rais kuruhusu kuvunjwa kwa sheria hii hii! Watu hawa hawa ambao wamekuwa wanavuruga tasnia ya uwindaji wa kitalii nchini na kuipotezea nchi mamilioni ya dola, Nyalandu akawazawadia Leseni ya Rais kuua wanyama 704 kinyume cha Sheria.
Akajitungia kifungu chake cha sheria kichwani (hakimo kitabuni) kutetea uhuni huu kuwa eti wana mchango kwenye uhifadhi! Kwa mazingira haya, kwa nini tusiamini kuwa Nyalandu ni sehemu ya matusi tunayotukanwa? Wala tusitafute mchawi, mchawi tunaye na kikulacho ki nguoni mwako.
Lakini sisi kama Taifa, ni lazima tuzinduke sasa. Inawezekana tulishaiuza nchi yetu bila sisi wenyewe wala viongozi wetu wengine kulijua hilo. Henry Kissinger, aliyewahi kuwa Mshauri wa Masuala ya Usalama wa Taifa na baadaye Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani enzi za utawala Rais Nixon alishaweka wazi kuwa Marekani hana rafiki au adui wa kudumu zaidi ya maslahi. Hadi leo hii imebaki kuwa ndiyo sera ya Taifa hilo kubwa.
Nyalandu aliwahi kumshinikiza Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori (Keraryo) atoe mwaliko kwa wanajeshi wastaafu wa Marekani kuingia nchini eti kusaidia kupambana na ujangili. Keraryo alikataa kwa misingi kwamba huu ni uhaini. Nyalandu alijaribu kulileta hili suala wakiwa Marekani, lakini Rais Jakaya Kikwete alikemea na kumuonya kuwa hili halimhusu huku akisema – “HABARI YA WANAJESHI ACHANA NAYO NYALANDU HAIKUHUSU, NI MAJUZI TU UMEAMBIWA KUWA UNAUZA NCHI LEO UNALETA MAMBO YA JESHI!
Anapotokea Waziri mwandamizi wa Serikali yetu akawa anatumia muda wake mrefu nchini Marekani; akawa na ukaribu unaotia shaka na kampuni za kimarekani; akatekeleza amri za Wamarekani bila kujali haki za watu na mataifa mengine; akawa na kiburi hata kuishtaki Ikulu kwenye ubalozi wa Marekani pale mambo yake yanapokwama na; akawa anadai hadharani kuwa Marekani inamtaka awe Rais wa Tanzania; kwa nini tusishtuke? Huyu kweli atajali uhusiano wetu na China kudorora? Haiwezekani mbwa mmoja kubweka kwenye maboma mawili kwa wakati mmoja!