*Aanza kuwasaka wabaya wake, awatisha
Aprili 22, mwaka huu, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, akiwa na baadhi ya watendaji waandamizi wa Wizara hiyo mjini Dodoma, alitoa vitisho akiahidi kuwashughulikia wote aliodai kuwa wanavujisha siri za ofisi kwa watu wasiohusika. Akasema ana uwezo wa kuwajua watumishi hao.
Kimsingi, hakuna ubishi hata kidogo kuwa si sahihi na ni kinyume cha maadili kuvujisha siri za ofisi yoyote. Hata hivyo, Nyalandu kwa makusudi au kwa kutokufahamu, ametumia neno “Siri za Ofisi” kwa makosa. Anachokusudia ni kuwatisha watumishi dhidi ya taarifa zinazoandikwa magazetini kuhusu tuhuma na uamuzi wake wenye utata ambao amekuwa akiufanya!
Naamini kuwa yanayojitokeza magazetini na kwenye mitandao ya kijamii yakimlenga Nyalandu ni madudu na kamwe hayana hadhi ya kuwa “siri za ofisi”. Yeyote anayesaidia kuweka madudu haya hadharani ni mzalendo wa kweli ambaye badala ya kutishiwa, anastahili kupongezwa.
Aidha, kuwekwa wazi madudu haya kunatakiwa kumsaidia Nyalandu ajirudi na kutumikia umma badala ya matajiri wachache ambao bila soni wanamtumia kugeuza Wizara kuwa shamba lao. Ni lazima Nyalandu aelewe kuwa hana hatimiliki ya Wizara na kwamba akifanya madudu ni lazima yatasemwa bila kujali atatumia nguvu gani kuyazima.
Kwanza, badala ya kukimbilia kutoa vitisho, Nyalandu alitakiwa kujiuliza, ni kwa nini siri zianze kuvuja mara tu baada ya yeye kupewa uwaziri kamili? Je, inawezekana anachukiwa kuliko mawaziri wote waliopita katika Wizara hii? Na ni kwa nini achukiwe yeye tu? Mtu mwenye tafakuri jadidi angekuwa amefahamu kuwa lazima kuna tatizo. Tatizo hili haliwezi kumalizwa kwa vitisho, bali kwa njia za kistaarabu ikiwamo kurejea kwenye maadili.
Kama alivyowahi kusema msomi mmoja, “a wise man does not solve a problem by crisis.” Katika makala haya nakusudia kuonesha kuwa ni kwa namna gani yanayoandikwa kumhusu Nyalandu ni madudu na wala si “siri za ofisi.”
Nianze kwa kukumbusha kitendo cha Nyalandu kuwahi kushinikiza Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) ichangie Sh milioni 560 kwa ajili ya mashindano ya Miss East Africa! Hii haiwezi kuwa “siri ya ofisi”, bali ni kutokuwajibika na kukosa umakini. Haiji akilini hata kidogo, wakati Wizara ina fedha kiduchu na inakabiliwa na changamoto kubwa ya ujangili, atokee waziri kudai mamilioni kwa ajili ya u-miss. Kama huku si kushindwa kujua vipaumbele vyenye umuhimu na maslahi kwa Wizara ni nini? Na kama hili si madudu na ubadhirifu, itakuwa na tafsiri ipi nyingine?
Nyalandu alikuwa miongoni mwa watu wa awali kukandia Ripoti ya Lembeli ya Operesheni Tokomeza, akidai imejaa majungu, uongo na upotoshaji. Mtu anapohoji sababu za kuamua ghafla kula matapishi yake na kujifanya anatekeleza maazimio ya ripoti hii hata kabla ya Tume ya Mahakama iliyoahidiwa kuundwa, atakuwa amevujisha siri zipi za ofisi?
Haiji akilini kudai kuwa watu wanavujisha siri za ofisi kwa kuhoji busara ya Nyalandu kukiuka sheria na taratibu za utumishi wa umma kwa kuwaondoa kazini wakurugenzi wa wanyamapori na yule wa Bodi ya Utalii kwa sababu za kutungatunga tu; hasa baada ya kutomhusisha Katibu Mkuu, ambaye ndiye mamlaka ya uteuzi. Na shaka inajengeka zaidi pale tunapojuzwa kuwa aliowateua wanatajwa kuwa “manabii wa ujangili”. Kwa nini watu wasihoji hili, na hasa ikitiliwa maanani kuwa Nyalandu mwenyewe amekuwa akituhumiwa kujihusisha na ujangili? Je, hawajibiki kuthibitisha kuwa haya si kweli, badala ya wimbo anaokuja nao wa “siri za ofisi?”
Watu wanapohoji kuhusika kwa Nyalandu na mazingira yanayolingana na hujuma dhidi ya mtangulizi wake, Balozi Khamis Kagasheki, hakuwezi kuchukuliwa kama “siri za ofisi”. Huu ni usaliti na fitina, na hasa kwa kuwa mara nyingi mazingira haya yalilenga kukwamisha utekelezaji wa majukumu ya wizara. Utata unazuka pale bosi wake anapojiuzulu na yeye Nyalandu, aliyekuwa msaidizi wake mkuu, kupanda cheo na kujipa jukumu la kutekeleza maazimio ya Kamati ya Lembeli iliyotaka wasaidizi wa Waziri wang’oke.
Nyalandu anaamini kuwa yeye hahusiki na kilichomng’oa Balozi Kagasheki, na kwamba ni jukumu lake kuwang’oa Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Wanyamapori! Hajatuambia kuwa yeye alikuwa wapi wakati wa Operesheni Tokomeza na kwamba alikuwa anapokea mshahara au la! Kama ambavyo baadhi ya watu wanadai kuwa kusitishwa kwa Operesheni Tokomeza na kuandaliwa kwa Ripoti tata ya Lembeli kulikuwa na mkono wa majangili papa, Nyalandu atajitoa vipi katika kashfa hizi? Kitu gani kimemfanya yeye akasalimika?
Kuhoji uamuzi wa kibabe wa Nyalandu uliosababisha kurefusha msimu wa uwindaji huku akidharau ushauri wa kitaalamu ni kufichua madudu, na wala si kuvujisha siri. Atuambie uamuzi huu ulikuwa na maslahi gani na kwa nani? Kwa nini hakutaka kuwashirikisha wataalamu na watendaji wa Wizara yake katika suala hili? Je, mbona hakuonesha kushtuka hata baada ya kuelezwa athari hasi za uamuzi huo kwa ustawi wa wanyamapori na uchumi wa nchi? Je, mazingira haya hayana harufu ya rushwa?
Kuhoji busara ya Nyalandu kutaka kurefusha muda wa kumiliki vitalu vya uwindaji wa kitalii kutoka miaka 5 ya sasa hadi miaka 15, kunyang’anya kwa hila baadhi ya wazawa vitalu walivyomilikishwa kisheria na kuwapa rafiki zake Wamarekani, kufungua mpaka wa Bologonja bila kufikiria athari za kiuchumi kwa Tanzania si kuvujisha “siri za ofisi”, bali ni kuzuia uharibifu na hujuma dhidi ya Taifa letu.
Kuhoji uhusiano wa kutatanisha kati ya Nyalandu na kampuni za uwindaji wa kitalii na zile za utalii wa picha si kuvujisha siri, bali ni kutahadharisha hatari ya kuwapo mgongano wa maslahi. Na hili limekuwa wazi kwani huhitaji akili kubwa sana kujua kwamba uamuzi mwingi wa Nyalandu umefanyika ili kulinda maslahi yake binafsi au marafiki zake.
Uamuzi huu ni pamoja na kuwaondoa kazini watumishi waadilifu na kuwateua wanaotuhumiwa, kurefusha msimu wa uwindaji kwa miezi tisa, kusaidia baadhi ya kampuni kukwepa kodi, kuahidi kunyang’anya wazawa vitalu na kuwapa marafiki zake, kuahidi umiliki wa vitalu kwa miaka 15, kufungua mpaka wa Bologonja na kurefusha muda wa kulipa ada ya vitalu, na kadhalika.
Mtu anayedai kuwa kufichua mpango mchafu wa kukabidhi hifadhi zetu kwa makaburu wa Afrika Kusini ni kuvujisha “siri za ofisi” atakuwa hana hoja. Kwa nini tusiambiwe kuwa mpango huu ulikuwa unafanyika kwa maslahi ya nani? Tunajua kuwa Nyalandu alikanusha kuhusika na hujuma hii kwa hoja iliyochoka – kwamba si kweli na kwamba eti “huo ni mkakati wa majangili kutumia waandishi uchwara (gutter journalists) ili Serikali ipoteze mwelekeo na kutumia muda kujibu badala ya kuwashughulikia majangili.”
Nyalandu alitakiwa auambie umma kilichompeleka Afrika Kusini yeye, Lembeli na ujumbe wa watu watano hata baada ya wataalamu bingwa wa uhifadhi kumtahadharisha juu ya utapeli wa African Parks Network (APN), asasi iliyokuwa inataka kukabidhiwa hifadhi zetu kwa udi na uvumba.
Nyalandu anataka kutuaminisha pia kuwa kuhoji sababu za kutumia mamilioni ya walipa kodi kugharimia ziara ya Martin Fletcher (na mwenzake), mtu aliyeichafua Tanzania na kumdhalilisha Rais wetu, ni kuvujisha siri za ofisi! Na kwamba anayesema kuwa tumevuna aibu kubwa zaidi kwa kutumia gharama zetu wenyewe anavujisha “siri za ofisi!
Kwanza, “Mzungu wa Nyalandu” mwenyewe anasema kuwa mwaliko wa Nyalandu ulikuwa kituko cha mwaka! Hakutarajia kuwa baada ya kututusi na sisi kukanusha vikali na kumlaani, Waziri angemzawadia yeye na rafiki yake study tour kwa kuwalaza kwenye hoteli ya nyota tano, kuwapeleka Selous kutalii na kukubali kuvunja sheria kwa kuwaruhusu kuingia kwenye ghala la pembe za ndovu na kupiga picha!
Nyalandu ndiye aliyemwambia Martin Fletcher wa Daily Mail kuwa anasoma shahada ya uzamili na kwamba kila mwezi lazima aende Uingereza kwa siku kadhaa. Inasemekana kuwa mlipaji wa gharama hizi ni Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Mtu anapohoji sababu za kujichotea mamilioni ya umma bila kufuata taratibu atakuwa amevujisha siri zipi za Serikali?
Siamini kuwa kuonesha athari za kiuchumi ambazo tayari zimeanza kujitokeza kutokana na uamuzi wa jazba wa Nyalandu ni kuvujisha siri. Sana sana ni kuonesha kutimia kwa utabiri kwa kuwa tayari alishatahadharishwa, lakini kwa kiburi chake akakaidi. Ni siri gani na kuna ubaya gani kuuonesha umma hasara itakayotokana na hatua ya majuzi ya Serikali ya Marekani kupiga marufuku nyara za uwindaji wa kitalii kutoka Tanzania?
Kwa hulka yake, Nyalandu hupenda kuita mikutano na waandishi wa habari hata kwa mambo mepesi mno. Hata hivyo, swali langu ni je, Nyalandu analiona suala la Marekani kupiga marufuku nyara kutoka Tanzania kuwa ni jepesi kiasi hicho? Au hana habari nalo? Je, hili halihitaji mkutano na waandishi wa habari? Tunataka ufafanuzi wa kina na atuambie ana mikakati gani kunusuru uchumi wa nchi kutokana na hatua hii ya Serikali ya Marekani, badala ya kutishia watu kuwa hii ni “siri ya ofisi”.
Mtu atakuwa amevujisha vipi siri kwa kuhoji kinapotoka kiburi cha Nyalandu na busara yake kujinadi kuwa ana ukaribu na Rais na familia yake? Kujigamba kuwa ana ukaribu na Rais anatarajia watu waogope, wasihoji chochote?
Kuhoji mazingira yaliyomfikisha Nyalandu kwenye ngazi ya uwaziri licha ya kuandamwa na tuhuma lukuki na kutolewa tahadhari kwenye magazeti na mitandao mingi ya kijamii siyo kuvujisha “siri za ofisi”, bali ni kuonesha madudu yanayoimaliza nchi hii. Sana sana, badala ya vitisho, Nyalandu alitakiwa kuita mkutano wa waandishi wa habari, kama alivyozoea, atuambie kwa kutumia hoja na ushahidi kuwa tuhuma hizo si za kweli.
Aseme anasingiziwa na kwamba hakuwahi kufanya uhalifu akiwa Marekani, hana uhusiano wowote na Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA), hakuwahi kuvunja vizuizi vya barabarani Singida, hakuwahi kutishia watu kwa bunduki, hakuwahi kujihusisha na ujangili wala majangili, hana uhusiano na wala hajawahi kufaidika na kampuni za uwindaji, hakuwahi kuwadhulumu watoto; na mengineyo.
Hii ingesaidia kutuweka sawa. Na kama Watanzania, anaotakiwa kuwatumikia, tuna haki ya kudai kuwa atutoe wasiwasi kuwa tuhuma hizi si za kweli ili tusonge mbele na ujenzi wa Taifa.
Ushauri wa bure kwa Nyalandu; asijiamini sana. Atulie, aache kukurupuka, ajue kuwa hana hakimiliki ya kuamua chochote bila kuulizwa. Atafute na kusikiliza ushauri na kushirikisha watendaji katika uamuzi wote wa kisheria na kitaalamu. Wale anaokaa nao hotelini wakamtuma cha kufanya kinachohusu Wizara watakuwa ndiyo sababu kubwa ya anguko lake, japo kwake anaamini kuwa ndiyo mwanzo wa utukufu.
Mwisho, kama rafiki na kiongozi wangu wa Ushirika wa Kikristo wa Wanafunzi Tanzania (UKWATA), napenda nimkumbushe Nyalandu kuwa anachofanya ni uasi kwa Bwana na kwamba ni bora atubu sasa. Namwacha kwa maneno haya ya Mtume Petro ili yamsaidie kutafakari na kujirudi:
“Lakini kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu, kama vile kwenu kutakavyokuwako walimu wa uongo, watakaoingiza kwa werevu uzushi wa kupoteza, wakimkana hata Bwana aliyewanunua, wakijiletea uharibifu usiokawia. Na wengi watafuata ufisadi wao; na kwa hao njia ya kweli itatukanwa. Na katika kutamani watajipatia faida kwenu kwa maneno yaliyotungwa; ambayo hukumu yao tangu zamani haikawii, wala uvunjifu wao hausinzii.” (2Pet.2:1-3)