Kwa mujibu wa nyaraka ambazo JAMHURI imezipata, kufanyika kwa mkutano huo kunatokana na shinikizo la Waziri Nyalandu, anayetajwa kama muumini mkuu na rafiki wa karibu wa raia wa kigeni, hasa Wazungu.
Nyaraka ambazo JAMHURI imezipata zinaonesha kuwa Nyalandu amemwamuru Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maimuna Tarishi, awape taarifa watu wanaopaswa kuhudhuria mkutano huo nchini Afrika Kusini bila kukosa.
Pamoja naye Nyalandu, wengine walioko kwenye msafara huo kwa maelekezo ya Waziri ni mwakilishi kutoka Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA). Kwa sababu hiyo, Mkurugenzi wa TANAPA, Allan Kijazi, bila shaka atatakiwa asikosekane kwenye mkutano huo.
Mwingine ni Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori. Hata hivyo, kuna uwezekano wa Idara hiyo kuwakilishwa na Kaimu Mkurugenzi wake, Paul Sarakikya.
Katika hatua inayotia shaka dhamira ya mpango huu, mwingine kwenye msafara huo amepangwa kuwa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli. Pamoja naye, ametakiwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Tarishi awepo; lakini kuna habari kwamba huenda akawakilishwa na Naibu Katibu Mkuu, Nuru Millao.
Uchunguzi wa awali uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa suala hili la kutolewa kwa Hifadhi za Taifa kwa wawekezaji umeweza kuwaunganisha Nyalandu na Lembeli, jambo ambalo linazidi kuzua shaka.
Kampuni ya African Park Network imekuwa na mpango wa kuhodhi Hifadhi za Taifa katika mataifa kadhaa barani Afrika, lakini inatajwa kuwa imekosa mafanikio. Mfano wa karibuni ni umiliki wake wa Hifadhi ya Taifa ya Akagera nchini Rwanda ambako kama ilivyokuwa Net Group Solutions nchini Tanzania, imeshindwa kabisa kuonesha mafanikio.
Vyanzo vya habari vimeiambia JAMHURI kwamba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ameweza kukubaliana na ujio wa African Park Network, ingawa barua kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi imepinga vikali mpango huo.
Pinda ameonekana kuwa njia ya mkato kwenye suala hili kutokana na uelewa wake wa kiasi katika masuala la uhifadhi. Kwa mwanya huo, imeelezwa kuwa Waziri Nyalandu ameweza kupenyesha hoja yake ya kuletwa kwa makaburu hao na kufanikiwa.
Bado wahifadhi wengi wanapinga mpango wa kutolewa kwa Hifadhi za Taifa kwa maelezo kwamba haupaswi kuchukuliwa kama uamuzi wa Wizara, bali ni jambo linalostahili mjadala wa kitaifa.
Chanzo cha habari kimesema kama kampuni hiyo ya makaburu itafanikiwa kuitwaa Katavi, basi huo utakuwa mwendelezo wa kutwaa Hifadhi nyingine, ikiwamo Serengeti.
Kadhalika, imebainika kuwa mashirika kadhaa yaliyo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii yanashinikizwa yatoe fedha za tiketi na za kujikimu kwa ujumbe utakaokwenda Johannesburg kubariki “kuuzwa” kwa Hifadhi za Taifa. Mashirika ya umma yanayolengwa ni Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).
Wasifu wa Katavi
Katavi ina mto Katuma ambao ni muhimu kwa uwepo kwa maziwa Katavi na Chada. Sifa nyingine ya pekee ya hifadhi hii ni wingi wa wanyama aina ya viboko na mamba.
Kabla ya ujangili kushamiri, ilikadiriwa kwamba Katavi ilikuwa na ndovu 4,000, maelfu ya nyati, twiga, pundamilia, impala na aina nyingine mbalimbali za wanyamapori.
Utata wa Nyalandu
Nyalandu, licha ya kuwa ni Waziri wa Maliasili na Utalii, ana uhusiano wa karibu mno na wa muda mrefu na kampuni ya Mwiba Holdings Ltd. Hii ni kampuni dada ya kampuni nyingine za Friedkin Conservation Fund (FCF) ambazo ni Wengert Windrose Safaris (WWS) na Tanzania Game Trackers and Safaris (TGTS). Hata hivyo, tofauti na WWS na TGTS, Mwiba Holdings Ltd haijasajiliwa kama kampuni ya uwindaji wa kitalii.
Kuanzia Julai 24, 2013 kampuni hiyo imekuwa ikiomba kupatiwa haki ya matumizi ya eneo wanalomiliki katika Kijiji cha Makao, Wilaya ya Meatu, kwa ajili ya utalii wa picha na uwindaji wa kitalii. Maombi haya yalifikishwa wizarani na kukataliwa na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki.
Uchunguzi unaonesha kuwa Nyalandu ameshinikiza kampuni ya Mwiba na nyingine zenye nasaba nayo, zipewe maeneo kwa ajili ya kuanzisha ranchi, jambo ambalo ni kinyume kabisa cha sheria na kanuni.
Tamati