*Yeye, James Lembeli waenda Afrika Kusini kukamilisha mpango
*Baada ya Katavi Hifadhi nyingine nazo zitatolewa kwa wawekezaji
*Katibu Mkuu ashinikizwa, abaki njia panda kuidhinisha safari, malipo
*Urafiki wa Waziri, Lembeli waibua shaka miongoni mwa watumishi
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, yupo kwenye hatua za mwisho za kuikabidhi Hifadhi ya Taifa ya Katavi kwa mwekezaji wa Afrika Kusini.
Kwa kuanza, ameshakamilisha mipango ya kuingia makubaliano na kampuni ya Afrika Kusini ya African Park Network, ili ichukue Hifadhi hiyo ya Taifa.
Uamuzi wa kuikabidhi Katavi kwa mwekezaji, unafanywa kwa siri na kwa uharaka ambao umewaacha watendaji wengi ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii wakiwa wameshikwa na bumbuwazi.
Kwa sasa Hifadhi za Taifa ni 16. Nazo ni Arusha, Gombe, Katavi, Mlima Kilimanjaro, Kitulo, Mahale, Ziwa Manyara, Mikumi, Mkomazi, Ruaha, Kisiwa cha Rubondo, Saadani, Kisiwa cha Saanane, Serengeti, Tarangire na Milima ya Udzungwa.
Hifadhi ya Katavi ni ya tatu kwa ukubwa nchini Tanzania baada ya Seregenti na Ruaha. Ukubwa wake ni kilometa za mraba 4,471. Inapatikana kusini magharibi mwa Ziwa Tanganyika.
Habari za uhakika ambazo JAMHURI imezipata, zinasema Hifadhi ya Taifa ya Katavi inakabidhiwa kwa kampuni hiyo ya Afrika Kusini ikiwa ni utekelezaji maagizo ya Waziri Nyalandu.
Hili ni moja ya mapigo makubwa aliyoyaandaa, ikiwa ni mbali na uswahiba wake na kampuni za TGT zinazomilikiwa na bilionea wa Marekani. Tayari ameshaanza mipango ya kuhakikisha bilionea huyo anapewa vitalu ambavyo kwa sasa vinamilikiwa na Watanzania wazalendo.
Awali, mpango wa “kuuza” hifadhi hiyo uliwasilishwa kwa mawaziri waliopita, lakini ulikwama kutokana na hofu halali za wataalamu wa uhifadhi katika Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau wengine.
Ubarikio wa kuikabidhi Katavi kwa raia wa Afrika Kusini, ambao kwa miaka mingi Serikali ya Tanzania iliwapinga, umepangwa kuanza Machi 27 hadi 29, mwaka huu, katika mkutano utakaofanyika Johannesburg, Afrika Kusini.