Sasa ni dhahiri kuwa juhudi za aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii katika Serikali ya Jakaya Kikwete, Lazaro Nyalandu, kutaka kuwa mmoja wa mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Tano ya Dk. John Magufuli zimegonga mwamba.
Kama ambavyo ilikuwa katika awamu iliyopita, Nyalandu aliamini kuwa kwa kutumia ushawishi wa Wamarekani, Rais Magufuli angesalimu amri na kumteua, ama kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, au Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Msimamo huu wa Rais Magufuli kukataa kuitia najisi Serikali yake kwa kuteua mtu aliyejaa kashfa eti tu ili kuwafurahisha Wamarekani, ni wa kupongezwa kwa dhati. Hii inaua ile dhana iliyojengeka miongoni mwa wengi kuwa kampuni za uwindaji wa kitalii (hasa za Wamarekani) ndizo zenye uwezo wa kuamua nani awe Waziri wa Maliasili, nani awe Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, au nani awe Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori.
Rais Magufuli amejipambanua kama mzalendo wa kweli anayetunza Uhuru wa nchi yetu kama sovereign state.
Pamoja na tambo zake mara kadhaa kuwa ni rafiki kipenzi wa familia ya Rais Kikwete, Nyalandu alitumia nguvu ya Wamarekani kuhakikisha kuwa mambo yake yanapita bila kukwama. Ndiyo maana bila aibu aliwahi kutamka hadharani kuwa Wamarekani wanamtaka yeye ndiye awe Rais wa Tanzania wa Awamu ya Tano! Ndiyo maana, hata pale uamuzi wake wa kuteua Wakurugenzi wa Idara ya Wanyamapori kinyume cha Sheria na Kanuni ulipotenguliwa na aliyekuwa Katibu Mkuu Utumishi (Yambesi) Nyalandu alikimbilia Ubalozi wa Marekani kutaka Marekani ishinikize ili watu wake wabakie.
Ni Nyalandu huyu huyu aliyeandaa mkataba na bepari wa Kimarekani, Howard Buffet, ukiweka sharti kuwa ili bepari huyu atoe misaada ya uhifadhi kwa Tanzania, lazima Nyalandu aendelee kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii! Eti Tanzania tumechoka mpaka Wamarekani waamue kututeulia mawaziri wanaowataka wao!
Aidha, inaeleweka kuwa uamuzi wa hovyo aliofanya Nyalandu kuwafukuza kina Profesa Alex Songorwa (Mkurugenzi wa Wanyamapori) na Profesa Jafary Kidengesho (Mkurugenzi Msaidizi) yalitokana na amri aliyopewa na Wamarekani wenye kampuni za uwindaji nchini baada ya kukwama kuwaweka mfukoni wasomi hao waliosaidia kuleta mabadiliko makubwa sana ya kiutendaji ndani ya Idara ya Wanyamapori.
Sasa Wizara ya Maliasili na Utalii imewapata Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu. Kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa letu, naomba nitoe ushauri. Naomba sana, viongozi hawa wamshawishi Mheshimiwa Rais Magufuli, awarejeshe Profesa Songorwa na Profesa Kidegesho, ili waijenge Wizara hii vilivyo. Endapo ushauri wangu utazingatiwa, Wizara ya Maliasili na Utalii itakuwa imekamilika kweli kweli. Naomba sana ushauri huu uzingatiwe.
Wahenga walisema kuwa ni wachache sana wanaoweza kuachana na hulka zao au urahibu (addiction). Pamoja na harakati za Nyalandu kugonga mwamba, kuna taarifa za kuaminika kuwa sasa anahaha kuupata Uenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira; nafasi iliyokuwa inashikiliwa na rafiki yake mkubwa katika maslahi, James Lembeli.
Itakumbukwa kuwa ili kuhakikisha kuwa hapati upinzani wowote, Nyalandu aliunda “utatu wa ulaji” na James Lembeli na Peter Msigwa (aliyekuwa Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii). Inasemekana kuwa nyuma yao walikuwapo Wamarekani wanaojihusisha na biashara ya uwindaji wa kitalii.
Ingawa ni vigumu kujua kiasi Nyalandu alichokuwa anawalipa Lembeli na Msigwa, lakini lililo dhahiri ni kwamba wawili hawa walineemeka sana katika kipindi kifupi cha uwaziri wa Nyalandu kutokana na ziara za mara kwa mara nje ya nchi. Sioni lugha nyingine rahisi inayoweza kutamkwa zaidi ya ukweli kuwa safari hizi zilikuwa rushwa ya dhahiri ili kuwafunga midomo. Ndio maana Msigwa alisahau kabisa kazi yake kama ‘Watch dog’ akaanza kuzunguka kwenye vyombo vya habari akiimba utukufu wa Nyalandu na kulazimisha umma uamini kuwa Nyalandu ni malaika na msafi, japo yeye mwenyewe siku chache kabla alikuwa anamponda na kushangaa juu ya uteuzi wake. Hii ni aibu kwa Waziri Kivuli, tena anayejiita Mchungaji!
Katika mkakati huu wa kuutaka Uenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, wapo Wamarekani wale wale waliomsaidia Nyalandu kuupata ubunge na baadaye uwaziri; na juzi juzi ubunge tena na baadaye kutaka apewe uwaziri! Wanapigana kufa au kupona kuhakikisha kuwa anapata Uenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge letu! Tusali sana isije kuwa bahati mbaya baadhi ya wabunge wetu wakakubali kununuliwa ili Nyalandu na Wamarekani wafikie malengo yao. Wabunge msikubali tena kuiuza Tanzania yetu.
Tujiulize, Wamarekani hawa wana mapenzi gani na Tanzania? Kama wanampenda sana Nyalandu kwa nini wasimpeleke kwao wakampa hata urais?
Nawaombea wabunge wetu roho ya uzalendo na kukemea pepo ovu la rushwa miongoni mwao. Nchi hii imeumizwa sana na madudu ya Nyalandu na rafiki zake. Mzalendo yeyote wa kweli asingetamani kuyashuhudia tena. Sana sana naamini kuwa mamlaka (wakiwamo wabunge) hazijachelewa kumtaka Nyalandu awajibike kutokana na hujuma zake kwa Taifa hili. Atueleze kwa nini tusimhukumu au kumweka katika orodha ya majipu yaliyoiva yanayotakiwa kutumbuliwa haraka. Huyu muda huu anapaswa kushitakiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka. Ameliumiza sana Taifa letu. Kama kina Basil Mramba na Daniel Yona wanatumikia vifungo jela, sioni ni kwanini Nyalandu na wenzake wasishitakiwe sasa.
Bado tuna kumbukumbu za kauli zilizokuwa zimesambaa katika Jiji la Arusha zikisema watuhumiwa wa ujangili walifanya karamu kusherehekea uteuzi wa Nyalandu kwenye nafasi ya Uwaziri wa Maliasili. Wapo wengine wanaomjua waliolinganisha uteuzi wake na kitendo cha fisi kukabidhiwa bucha ya nyama alinde!
Bado tuna kumbukumbu ya Nyalandu kuvunja vizuizi vya barabarani huko Singida usiku na kutishia walinzi kwa bunduki huku akikataa gari yake iliyosadikiwa kuwa na nyara za Serikali kukaguliwa.
Anataka ubosi wa Kamati akafanye nini wakati ana majina 320 ya majangili hataki kuyaweka hadharani kama alivyowahi kuahidi?
Itakumbukwa kuwa Kamati ya Bunge ambayo leo Nyalandu anataka kuwa bosi wake ilijifanya kumpiga mkwara mzito Nyalandu kutokana na kitendo chake (Nyalandu) kushinikiza Mamlaka za Hifadhi za Taifa (TANAPA) na ile ya Ngorongoro (NCAA) kutoza kiingilio mara moja tu (single entry) bila kujali kuwa wameingia hifadhini mara ngapi. Uamuzi huu uliingizia Ngorongoro hasara ya Sh bilioni 15.
Aidha, Nyalandu alikaidi hukumu ya Mahakama juu ya tozo katika hoteli zilizoko ndani ya hifadhi na kuisababishia nchi hasara ya Sh bilioni 80. Bahati mbaya, mamlaka yake ya uteuzi ilikaa kimya! Na kwa kuwa Kamati chini ya rafiki yake, Lembeli, ilikuwa ikifadhiliwa safari ndani na nje ya nchi haikuwa na ujasiri wa kuhoji.
Waziri Kivuli wa Maliasili, Msigwa, anayejiita Mchungaji, ndiye kabisaa akajifanya kiziwi na kipofu – kutimiliza ukweli wa maandiko matakatifu kuwa rushwa hupofusha. Ni dhahiri kwamba fadhila za Nyalandu kwa kina Lembeli na Msigwa zisingeweza kupotea bure.
Mkwara wa Kamati ile ya Lembeli ulikuwa kutaka kuzibwa midomo kwa pesa zaidi za walipa kodi na zile za marafiki zake Nyalandu (Wamarekani). Baada ya mkwara ule wa Kamati bungeni, hakuna marekebisho yoyote yaliyofanyika. Na hata mmoja wa watendaji wizarani alipouliza kuhusu sakata hili, Nyalandu alisikika akisema kuwa ‘hawanitishi hao, mimi ninawamudu!’
Ni dhahiri kuwa tafsiri yake ilikuwa kwamba wabunge wale wananunulika! Baada ya mkwara ule wajumbe wa Kamati walionekana wakila nchi Dubai, Ethiopia na Afrika Kusini – ziara walizodai kuwa ni muhimu kwa kuwa wao ndio Thinking Tank ya Wizara! Mungu atuepushe na aina ile ya wabunge ambao walijaa pepo wa ulafi!
Kuthibitisha kuwa Nyalandu tayari aliwamudu wajumbe hawa wa Kamati, alihamia mikoani na wilayani huku akiwa hana wasiwasi wowote. Akitumia ndege ya Serikali na kujilipa posho nene kwa madai ya kuhamasisha uhifadhi wakati watu walijua kuwa alikuwa kwenye kampeni za kuusaka urais. Mchana akijifanya yuko kazini, huku usiku akifanya mikutano ya siri na wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM kwenye wilaya husika! Wasiwasi utoke wapi wakati aliamini alikuwa na uwezo wa kuwaziba midomo wana Kamati kwa mamilioni? Na hilo ndilo lililotokea.
Ni wazi kuwa Lembeli, Mwenyekiti wa Kamati, hakuwa na ubavu wa kumgeuka Nyalandu. Asingeweza kufanya hivyo kutokana na kushirikiana naye katika vitendo vya hujuma dhidi ya Taifa kikiwamo kile cha kutaka kuuza Mbuga zetu kwa Kampuni binafsi ya African Parks Network (APN) ya Afrika Kusini. Je, Lembeli angethubutu kumkwamisha Nyalandu angewaambia nini Wamarekani waliokuwa wanawafadhili?
Kama ni majipu, basi Nyalandu ni moja ya majipu sugu. Amekuwa tayari kuwasaidia wafanyabiashara kuhujumu uchumi. Kwa mfano utamwelewa vipi waziri anayejifanya ana dhamana anapowashauri wenye mahoteli kuishtaki Serikali mahakamani akitaka hoteli zote bila kujali daraja zilipe tozo ambayo ni flat rate wakati anajua wazi kuwa kufanya hivyo kunaipotezea Serikali Sh bilioni 70 kwa mwaka?
Kashfa za Nyalandu ni nyingi mno. bahati nzuri, karibu zote zina ushahidi. Tulishamsihi Nyalandu mara nyingi kuwa aende mahakamani kama anaamini kuwa tunamsingizia. Baadhi ya kashfa za Nyalandu ni pamoja na kuhamishia ofisi kwenye hoteli za nyota tano katika majiji ya Arusha na Dar es Salaam huku Wizara ikilazimika kulipa gharama kubwa; kulala Arusha na kuamkia Dar es Salaam kila siku awapo nchini kwa gharama na ndege ya Serikali; kwenda kuzurura Marekani na vimada kwa gharama za Serikali; kujilipa posho tatu kwa safari moja; kugawa kinyemela vitalu vya uwindaji kwa rafiki zake (Wamarekani); kutumia vibaya Leseni ya Rais kuua wanyamapori 700 kinyume cha sheria; kurefusha msimu wa uwindaji ili kuwafurahisha rafiki zake; kuhusishwa na ujangili wa tembo; kutishia walinzi kwa silaha Singida na kuvunja vizuizi pale walipotaka kukagua gari lake; kuwashauri wenye hoteli kuishtaki Serikali kugomea tozo; kusaidia baadhi ya kampuni za utalii kukwepa kulipa kodi za serikali; kufukuza kazi watumishi waadilifu na kuwaweka watuhumiwa wa ujangili; kula njama na Wakenya ili kufungua mpaka wa Bologonja; kuhusika katika kashfa ya kuagiza helikopta chakavu iliyoua marubani wazalendo wanne; kutajwa kama pandikizi la CIA; kuingiza wanajeshi wastaafu wa Marekani kwa kile alichodai kuwa wanakuja kupambana na ujangili lakini baadaye kuwakana kuwa ni matapeli baada ya Wamarekani hao kujihusisha na vitendo vya uvunjifu wa sheria; kutumia pesa za umma kutoa rushwa kwa baadhi ya viongozi wa dini ili wamsafishe mbele ya jamii; kushiriki katika mchezo mchafu wa kutaka kuuza mbuga zetu akishirikiana na James Lembeli.
Nyalandu, pengine atakuwa waziri pekee wa Serikali aliyewahi kula njama kadhaa kuhujumu Serikali ambayo yeye mwenyewe ni sehemu yake: Kwa mfano, Mei 2013 aliwanunua baadhi ya wabunge akitaka bajeti yake ikwamishwe ili kushinikiza aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara, Mama Maimuna Tarishi, na wakurugenzi aliokuwa hawataki wang’olewe wizarani!
Waziri aliyewashauri Wakenya kuzuia magari ya utalii kutoka Tanzania kuingia Jomo Kenyatta Airport ili kushinikiza kufunguliwa lango la Bologonja ambalo yeye aliwaahidi kuwa litafunguliwa, lakini akakwamishwa; Waziri aliyewahakikishia wenye kampuni za uwindaji kuwa amerefusha msimu wa uwindaji, lakini baadaye mchakato ukakwama kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), jambo lililomfanya aungane na wenye kampuni za uwindaji kumponda AG ambaye kimsingi ndiye mshauri wa Serikali wa masuala ya kisheria; ni waziri aliyewahi kuichongea Ikulu katika Ubalozi wa Marekani akitaka balozi aishinikize ili maswahiba wake aliowapa Idara ya Wanyamapori warejeshewe vyeo vyao alivyowapa bila kufuata sheria na kanuni.
Nyalandu katika kipindi chake amekuwa akitoa kauli za kutatanisha. Leo atakuambia kuwa ujangili umepungua kwa asilimia 80; kesho atasema kuwa tembo wataisha baada ya miaka 10! Wakati anaimba ngonjera hizo huku akifuja hovyo pesa ambazo zingesaidia kupambana na ujangili, baadhi ya vituo vikawa havifanyi doria kutokana na kukosa pesa kwa miezi zaidi ya sita.
Nyalandu atakuambia kuwa tembo wameongezeka kutokana na juhudi zake kupambana na ujangili. Tembo wa Nyalandu ambao huzaana baada ya miezi 48 wakawa wanazaana kwa miezi 10! Ujangili umepungua, lakini husikii hata mmoja kati ya wale majangili wake 320 amekamatwa!
Badala ya Nyalandu kutaka kurejea katika sekta ya maliasili kupitia Kamati ya Kudumu ya Bunge ili kufikia malengo yake na wale anaowatumikia, ni wakati mwafaka wa kumburuza mahakamani kutokana na kutumia madaraka vibaya. Ni wakati wa kufilisi mali zote alizojikusanyia kutokana na rushwa. Ni wakati wa kuhoji kuwa mamlaka iliyokuwa imemteua ilikuwa na maslahi gani naye?
Hata Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii aliyeondolewa (Dk. Meru) lilikuwa chaguo la Nyalandu na walisaidiana sana kufuja pesa za umma. Na hapa ndipo tunapopaswa kuhoji, Je, TAKUKURU na ile Tume ya Maadili ya Umma walikuwa wamelala? Ni kweli kuwa hawakuwahi kusikia na kuona madudu ya Nyalandu?
Nihitimishe kwa kuwapongeza viongozi wakuu wa sasa wa Wizara ya Maliasili na Utalii. Tupo tayari kuwapa ushirikiano wowote wanaoutaka ili kuhakikisha Tanzania yetu inasonga mbele. Mungu awabariki sana.