Mara baada ya Balozi Khamis Kagasheki kujiuzulu kutokana na shinikizo la wabunge kadhaa, baada ya taarifa ya James Lembeli juu ya Operesheni Tokomeza kuwasilishwa bungeni Novemba, mwaka jana; Lazaro Nyalandu, wakati huo akiwa ni Naibu Waziri katika Wizara ya Maliasili na Utalii, alisafiri sana huku na kule nchini.
Ilitafsiriwa kuwa safari hizo zilikuwa ghiliba kwa Rais Jakaya Kikwete kuwa ni yeye tu alikuwa na uwezo wa kuvaa viatu vya Kagasheki. Kati ya safari alizozifanya zilikuwamo za Wilaya ya Meatu tarehe 1 na 3 Januari, mwaka huu ambazo alizifanikisha kwa kutumia ndege.
Kwa taarifa zilizopo ni kuwa Wizara ilimwandalia Nyalandu usafiri wa anga kwenda Meatu mnamo Desemba 31, mwaka jana kwa kutumia ndege aina ya Caravan inayomilikiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) lakini, safari ilivunjika siku hiyo na kufanyika Januari mosi, 2014. Sababu ilikuwa kwamba Caravan ya TANAPA isingeweza kutua salama kwenye uwanja wa Pori la Akiba Maswa ikiwa na abiria 10 – wengi wao wakiwa waandishi wa habari – waliokuwa wamefuatana na Nyalandu.
Hivyo, Nyalandu mwenyewe akatafuta na kuipata ndege ya pili ambayo ilipatikana; Januari mosi, 2014 safari ya kwanza ikafanyika. Ndege hiyo ya pili Nyalandu alipewa na ‘marafiki’ zake wa kampuni za uwindaji wa kitalii za TGTS na Wengert Windrose Safaris (zote za Friedkin Group of Companies ya Marekani) na alipatiwa ‘bila gharama yoyote’. Kwa hiyo, aliposafiri kwenda Meatu tarehe 1 na 3 Januari 2014 alitumia ndege mbili – haya si makosa ya ki-uandishi! Nasisitiza, alitumia ndege mbili!
Ni muhimu kwa Watanzania kuelewa kuwa kampuni hizi za Marekani ndizo zilikuwa na zimeendelea kuwa na migogoro na Idara ya Wanyamapori ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Ni kampuni hizo hizo za ambazo pia zimekuwa na mgogoro na kampuni nyingine za uwindaji zikilenga kuzinyang’anya vitalu walivyogawiwa wenzao kihalali. Kampuni hizo ni pamoja na ile ya Green Mile Safari Ltd (GMS) ambayo imekuwa ikilengwa na Wengert Windrose Safaris kunyang’anywa kitalu cha Ziwa Natron Mashariki. Kampuni nyingine ni Ferreck Safaris ambao baada ya fujo za FG waliamua kubwaga manyanga na kuachia kitalu ambacho sasa Nyalandu anataka kuwapa Wamarekani hao.
Maswali ambayo yamepata kuulizwa na waandishi kadhaa katika magazeti siku za nyuma ni pamoja na je, Nyalandu alifahamiana lini na kampuni hizi kiasi cha kupewa ndege bure? Wanahusianaje? Je, ‘marafiki’ hawa wa Nyalandu walitoa ndege yao kwa siku mbili bure kwa matarajio gani kutoka kwake? Au Nyalandu alipatiwa ndege hiyo baada ya kutoa ahadi gani? Je, baada ya kupewa ndege bure akipewa amri afanye jambo fulani atakuwa na ubavu gani kukataa kuitekeleza? Tayari tumeona alivyoagizwa na Wamarekani Machi, mwaka huu na tayari amefuta leseni za GMS. Huyu ndiye Nyalandu!
Hivi karibuni kumezuka suala jingine ambalo, kwa haraka haraka, unaweza kuliona kama jipya na lisilohusiana na mgogoro ambao umekuwepo ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii tangu Nyalandu ateuliwe kuwa waziri.
Suala hili ni lile lijulikanalo kama “DVD ya Msigwa” – DVD iliyoibukia bungeni kupitia kwa Msigwa inayoonesha uvunjifu wa sheria uliofanywa na wageni wa kampuni ya Green Mile Safari mwaka 2012. Ingawa baadhi ya watu wanaliona na wangependa suala hili liitwe jipya, lina uhusiano mkubwa na wa karibu sana na mgogoro wa kitalu cha Ziwa Natron Mashariki kilichogawiwa kihalali kwa Green Mile Safari kwa muhula wa uwindaji wa 2013 – 2018, ambacho kinang’ang’aniwa na kampuni ya Marekani ya Wengert Windrose Safaris.
Ni wazi kuwa yaliyofanywa na wageni wa kampuni ya Green Mile Safari mwaka 2012 ni uvunjifu wa sheria ya kuhifadhi wanyamapori pamoja na kanuni za uwindaji wa kitalii. Kwa vyovyote vile ni muhimu kulichunguza kikamilifu suala hili na, pale makosa yatakapothibitika, si tu kampuni ya Green Mile Safari, bali pia mwindishaji wake bingwa na watumishi wa Idara ya Wanyamapori waliosimamia uwindaji huo wanapaswa kuwajibishwa.
Tumekwishatangaziwa kuwa, kutokana na “DVD ya Msigwa” na msukumo wake yeye Msigwa, Nyalandu kainyang’anya leseni na kuifungia kabisa kampuni ya Green Mile Safari kujihusisha na uwindaji wa kitalii nchini. Hii ina maana gani kuhusiana na kitalu chenye mgogoro cha Ziwa Natron? Ni kuwa sasa kiko wazi na huenda kiko wazi kwa Wengert Windrose Safaris tu! Ingawa sheria na kanuni zinazosimamia uwindaji wa kitalii zinaelekeza kuwa kitalu chochote kikiwa wazi kitangazwe, na huenda kikatangazwa kutimiza matakwa ya kisheria, ni kampuni gani nyingine itahitaji kuingia kwenye mgogoro na hao wababe wa Kimarekani, tena wakati Nyalandu yu waziri mwenye dhamana ya wanyamapori?
Nimekuta majadiliano juu ya suala hili kwenye mtandao mmoja. Kati ya wachangiaji wengi mmoja alisema, “Kuna rationale gani ya kuwa na wizara, idara … wakati kazi ya kuibua unyama dhidi ya rasilimali imefanywa na mbunge mmoja, tena kutoka nje ya chama tawala?” Mtu huyu (na huenda wapo na wengine) anaonekana kuamini kabisa kwamba ni Msigwa ‘aliyegundua’ uovu wa kampuni ya Green Mile Safaris uliofanyika mwaka 2012. Hii si kweli, kwani Nyalandu alikuwa ana taarifa ya “DVD ya Msigwa” tangu mapema Machi, mwaka huu. Kama alivyoliona suala hili mchangiaji kwenye mtandao mwingine, “Haikwepeki kwamba kutakuwa na maslahi binafsi ya watu wetu”.
Mchangiaji huyu wa pili anaamini kuwa “Kuna maslahi binafsi ya Nyalandu na Msigwa kumpigania Mmarekani kupora vitalu vya uwindaji.” Anaendelea kuwasihi wenzie kuwa, kabla ya kumpongeza Msigwa wajiulize maswali yafuatayo: Kwa nini imechukua muda mrefu hatua stahiki kuchukuliwa? Usalama wa Taifa hili una vipaumbele gani? Ni nini zaidi kinafanyika nyuma ya migongo yetu Watanzania? Anahitimisha kwa wito kuwa “Kabla ya kumpongeza Msigwa hebu tufikiri nje ya kasha”.
Mchangiaji mwingine kwenye mtandao mwingine anasisitiza akisema, “Someni vizuri maandishi yote, kila kitu msome, ndipo muelewe hasa pana mgogoro? Ni kati ya nani na nani? Nani yupo katikati ya mgogoro? Nani ameuanzisha? Sababu ya kuuanzisha ni ipi? Aliyeuanzisha ana historia gani katika uwekezaji Tanzania? Ana mlinzi? Kama yupo ni nani? Wizara inamuonaje? Kwa kuwa mmeshaona alichokisema Msigwa, DVD, msijinyime kujua. Anzeni kusoma mgogoro kwa kuisoma taarifa ya GMS. Then chambueni.”
Ninaomba kuunga mkono wito wa wachangiaji wawili wa mwisho hapo juu kwani kuna uwezekano kabisa kuwa Msigwa anapewa (au anajipa) sifa asiyostahili. Pia, upo uwezekano kuwa, pamoja na kelele zote alizopiga Msigwa juu ya Green Mile Safari, katumiwa tu na akatakiwa ‘apige kelele mpaka mbingu zishuke’. Kwani hatujawahi kuwaona watu wa aina hii? Tumemsahau Beatrice Shelukindo mwezi Mei pale bungeni wakati akichangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu?
Sasa si siri ya Nyalandu pekee; inajulikana. Inajulikana kuwa tarehe 11 Machi mwaka huu – miezi miwili kabla ya yeye kuwasilisha bajeti ya wizara yake Bungeni – aliandikiwa barua na John C. Patterson, Jr, aliyekuwa Rais wa Dallas Safari Club (DSC) ya Texas, Marekani wakati huo (inayotumia anuani ya 13709 Gamma Road Dallas, TX 75244). Pamoja na mambo mengine Patterson Jr alimfahamisha Nyalandu kuwa siku kadhaa kabla ya tarehe ya barua yake yeye pamoja wanachama wenziye wengi wa DSC walikuwa wameangalia DVD iliyopewa jina la Hunting Trip Tanzania Season 2012. Katika barua yake hiyo kwa Nyalandu, Patterson Jr anaendelea kueleza kuwa video waliyoiangalia inaelekea kutengenezwa na kampuni ya uwindaji ijulikanayo kama Green Mile Safari Co. Ltd.
Sasa baada ya kuyajua haya, swali ni je; kuna Mtanzania anayeweza kudai kuwa DVD anayoiongelea Patterson Jr wa DSC si ile ambayo sisi Watanzania tumeibatiza kimakosa jina la “DVD ya Msigwa”?
Katika barua yake hiyo kwa Nyalandu, Patterson Jr anamweleza Nyalandu pia kuwa, kwenye mfuniko wa video hiyo kuna maelezo kuwa kampuni ya Green Mile Safari inafanya shughuli zake (za uwindishaji) katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwa na vitalu vitatu vya uwindaji wa kitalii: kimoja Arusha na viwili Selous. Kama wakati anaandika barua yake Patterson Jr alikuwa akielewa kuwa Green Mile Safari ina kitalu Arusha, ni lazima alikuwa akielewa pia kuwa kitalu hicho ni kile kinachong’ang’aniwa na Wamarekani wenzie wa Wengert Windrose Safaris. Ninaamini kuwa Wengert Windrose Safaris, ambayo mmiliki wake pia ni wa Texas, ni wanachama wa Dallas Safari Club.
Kuna taarifa kuwa Green Mile Safaris ilishiriki kwenye maonesho ya uwindaji wa kitalii yaliyofanyika mapema mwaka jana mjini Reno, Nevada, pia nchini Marekani. Wakiwa huko Wengert Windrose Safaris iliwafanyia fujo na kuwachafua. Iliwalazimu Green Mile Safari watoe taarifa kwa Safari Club International (SCI) – waliokuwa waandaaji wa maonesho hayo – ambao waliingilia kati. Ni lazima Dallas Safari Club ilishiriki maonesho hayo na huenda Patterson Jr pia alikuwapo.
Wote watakuwa wanaujua fika mgogoro wa kitalu cha Ziwa Natron Mashariki na ni Wamarekani wa Texas. Hatujui uhusiano wa Wengert Windrose Safaris na Dallas Safari Club lakini, inawezekana kabisa kuwa Wengert Windrose Safaris ni mwanachama wa Club hiyo.
Kuna uwezekano mkubwa kwamba barua ya Patterson Jr kwa Nyalandu ulikuwa utekelezaji wa mpango uliokuwa umekwishaandaliwa na pande hizi mbili ili kukamilisha mchakato wa kumwondoa Green Mile Safaris kwenye kitalu kilichosababisha afanyiwe fujo na Wengert Windrose Safaris. Swali tunalopaswa kujiuliza ni, je, Patterson Jr alimpelekea Nyalandu barua tu na kuishia kumwambia wao walikuwa nayo video ya Green Mile Safari? Ninalazimika kuamini kuwa alimtumia hiyo barua na video husika kwa pamoja kwani utekelezaji wa maagizo yaliyo kwenye barua ya Patterson Jr yasingewezekana bila ya yeye kuikabidhi kwa Nyalandu video inayohusika na maelekezo yaliyo katika barua yake.
Kwa hiyo, Nyalandu alipatiwa video na Dallas Safari Club ili aone na, baada ya hapo, atekeleze maagizo yaliyo katika barua yao ya kumtaka amwajibishe Green Mile Safari – yaani amnyang’anye kitalu cha Lake Natron na kumpatia mwenzao Wengert Windrose Safaris.
Julai 17, mwaka huu Dallas Safari Club iliweka kwenye tovuti yake Taarifa kwa Umma (Press Release) yenye kichwa cha habari DSC Praises Tanzania’s Crackdown on Green Mile Safari Co. Taarifa hiyo kwa Umma inaeleza kuwa, “The Dallas Safari Club (DSC) had urged the crackdown and is praising the move as a strong step …” ikiwa na maana kuwa Dallas Safari Club ilikuwa imehimiza kuchukuliwa kwa hatua kali za kinidhamu na inatoa pongezi kwa hatua zilizochukuliwa (na Nyalandu). Taarifa hiyo kwa Umma inaendelea kueleza kuwa, mwezi Machi DVD inayoonesha mwenendo usiokubalika iliifikia DSC. DSC iliwasiliana na Waziri mpya wa Utalii na Maliasili wa Tanzania, Mheshimiwa Lazaro S. Nyalandu, kuelezea uchungu/hasira/msononeko wao juu ya mwenendo mbaya na uliothibitika wa kampuni hiyo (yaani Green Mile Safaris).
Taarifa hiyo kwa Umma inaendelea kusema kuwa, “Rais wa DSC wakati huo, John Patterson, alieleza katika barua [aliyomwandikia Nyalandu] kuwa Club yake ‘inaamini sana kuwa moja ya vitendeakazi muhimu inavyoweza kutumia wizara [ya Nyalandu] katika juhudi zake za kuhifadhi wanyamapori wa nchi [ya Tanzania] ni kugawa vitalu kwa kampuni zitakazoheshimu sheria – na kuziondoa zile zisizoheshimu.”
Tangu mwaka jana au hata kabla ya hapo DSC ina taarifa ya mgogoro wa kitalu kati ya Wengert Windrose Safaris na Green Mile Safari. Je, walimaanisha nini hasa kumwandikia Nyalandu hivi? Kwa nini maagizo yao kwa Nyalandu hayakusema tu kuwa Green Mile Safari waadhibiwe kwa mujibu wa sheria za nchi? Kwa nini wamtake Nyalandu ainyang’anye Green Mile Safari vitalu?
Hakuna ubishi kuwa yeyote anayebahatika kuiona “video ya Msigwa” atakachoshuhudia ni ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia uwindaji wa kitalii nchini. Ni wazi kuwa yeyote anayevunja sheria za nchi anapaswa kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria. Lakini, katika barua ya Patterson Jr kwa Nyalandu lengo lililojificha nyuma ya maneno yake ni takwa kwa Nyalandu kuipoka Green Mile Safari kitalu cha Ziwa Natron Mashariki na kuipatia Wengert Windrose Safaris. Nyalandu amelazimika kulipa ‘fadhila’ za Wamarekani kwani alikwishajitumbukiza kwa hiyari yake mwenyewe katika mtego wao.
Sasa, je, ni kweli kuwa DVD ya Green Mile Safari ‘imevumbuliwa’ na Msigwa? Jibu ni hapana, na hii ni kwa sababu Nyalandu alikuwa nayo tangu siku alipopokea barua kutoka kwa Patterson Jr wa Dallas Safari Club. Na, je, Msigwa aliipata wapi? Kwa asilimia kubwa sana atakuwa amepatiwa na Nyalandu. Sababu za Nyalandu kumpatia Msigwa ziko wazi. Yeye tayari alikwishatangaza nia ya kupoka kitalu cha Green Mile Safari na kuwapatia Wengert Windrose Safaris akakemewa kwenye magazeti. Alitaka ionekane kuwa kufanya hivyo si matakwa yake, bali ameshinikizwa.
Swaiba wake nambari wa hedi, James Lembeli, hakuwa mtu mwafaka kutumika katika hili kwani tayari kwa pamoja wawili hao ‘wanauguza majeraha’ mengi kutokana na madudu waliyoyafanya kwa ushirikiano, likiwemo lile la kutaka kugawa hifadhi zetu kwa African Parks Network (APN) ya Afrika Kusini, ambayo Lembeli ni mjumbe wake wa Bodi.
Anayefuata kwenye orodha alikuwa ni Msigwa kwani, kwa miezi michache kabla ya “DVD ya Msigwa” kujulikana kwa umma wawili hao walionekana kuwa karibu sana. Mtakumbuka kuwa Nyalandu na Lembeli walipoonekana kutofautiana kutokana na ripoti ya Lembeli kuhusu utekelezaji wa Operesheni Tokomeza, msuluhishi alikuwa Msigwa? Tunaposema utatu hatari, tunamaanisha utatu huu!