*Marekani yapiga marufuku nyara kutoka Tanzania

Uamuzi tata na wa kijazba wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, umeanza kuleta athari kwa tasnia ya uwindaji wa kitalii nchini.

Marekani imepiga marufuku nyara zinazotokana na ndovu kutoka Tanzania kuingizwa nchini humo. Hilo ni pigo kubwa kwa uchumi wa Tanzania.

Kwa mujibu wa Shirika la Samaki na Wanyamapori la Marekani (US Fish and Wildlife Service-USFWS), hatua hiyo imechukuliwa na Marekani kutokana na usimamizi unaotia shaka, kushindwa kusimamia sheria na utawala mbaya katika sekta ya maliasili kiasi cha kusababisha wanyamapori, hasa ndovu, kupungua mno.

Mchango wa uwindaji wa kitalii kwa Idara ya Wanyamapori ni asilimia zaidi ya 80. Asilimia nyingine huchangiwa na biashara ya wanyama hai na utalii wa picha.

Serikali ya Tanzania imeshutumiwa kwa uzembe na kutoonesha dhamira ya dhati katika mapambano dhidi ya ujangili. Hapa imezingatiwa kuwa Rais Jakaya Kikwete alishautangazia ulimwengu kuwa ana majina ya majangili 50, lakini hadi wiki iliyopita hakuna hatua zozote zilizokwishachukuliwa dhidi ya watu hao.

Hatua ya Marekani inakuja kipindi kifupi baada ya Nyalandu kuteuliwa, na kuna habari za uhakika kwamba baadhi ya misimamo yake na ahadi hewa za kupambana na majangili, vimechangia uamuzi huo wa Marekani.

Katika kipindi hiki kifupi amefanya uamuzi tata na wa kibabe. Wengi wamekuwa wakihoji jeuri hii ya Nyalandu na nia yake hasa ya kufanya mambo yanayoashiria hatari kubwa katika uhifadhi, uchumi wa nchi na hadhi ya Taifa.

Uwindaji wa kitalii una mchango mkubwa katika uchumi wa nchi kwa kuingiza fedha za kigeni na kutoa ajira kwa Watanzania. Tembo, simba na chui ni vivutio vikuu katika tasnia ya uwindaji wa kitalii. Ingawa si wote wanaofanikiwa kuwawinda wanyama hawa, lakini safari zao zinachochewa zaidi na kuwapo wanyama hawa wanaojulikana kama ‘key species’ kwenye safari package zao.

Pesa zinazopatikana kutokana na uwindaji wa kitalii, pamoja na kuchangia maendeleo ya sekta nyingine, ni muhimu katika kuendelea kuwahifadhi wanyamapori na makazi yao.

Baadhi ya uamuzi uliochangia kupigwa marufuku nyara kutoka Tanzania

Miongoni mwa mambo yaliyosababisha uamuzi wa Marekani ni kufukuzwa kwa watumishi wanaotajwa kuwa waadilifu na kuteuliwa watuhumiwa wa ujangili.

Nyalandu aliwafukuza kazi Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Profesa Alexander Songorwa, na msaidizi wake aliyekuwa anasimamia Matumizi Endelevu, Profesa Jafari Kideghesho, na kuwapandisha vyeo Paul Sarakikya na Julius Kibebe.

Sarakikya ambaye huenda akastaafu kwa mujibu wa sheria mwaka kesho, kwa miaka yote amekuwa kwenye idara hiyo, na chini ya uongozi wake na Kibebe ndipo ujangili uliposhamiri.

Nyalandu alidai anawaondoa maprofesa hao kutokana na kutoridhishwa na utendaji kazi wao. Hata hivyo, inasemekana kuwa dhamira yake ni kinyume cha madai yake kwani aliowapandisha walikuwa miongoni mwa watuhumiwa wa ujangili, kiasi cha kufanya tatizo hilo kuwa janga la kitaifa.

Kitendo cha Nyalandu kuwaondoa watu walioleta mabadiliko makubwa ndani ya idara kwa kipindi kifupi cha mwaka mmoja na kuwaweka watu ambao tayari wana madoa, kimewaudhi wakubwa hao na kutilia shaka dhamira ya Tanzania katika kupambana na ujangili.

Kurefushwa msimu wa uwindaji na kupuuzwa ushauri wa kitaalamu

Sababu nyingine iliyosababisha nyara za Tanzania kufungiwa ni uamuzi mwingine tata alioufanya Nyalandu wa kurefusha muda wa uwindaji kutoka miezi sita hadi tisa. Pamoja na kushauriwa na wataalamu, alitumia ubabe huku akiwahakikishia matajiri wa tasnia ya uwindaji kuwa atawalinda dhidi ya “sheria mbaya.”

Pamoja na Nyalandu kuelezwa kuhusu athari za kiikolojia kutokana na uamuzi huo uliolenga kuwafurahisha matajiri, alitahadharishwa pia kuwa uamuzi wake ungeweza kuigharimu Tanzania kiuchumi. Tahadhari hiyo ilizingatia ukweli kuwa tayari lilikuwapo shinikizo kutoka kwa makundi mbalimbali nje ya nchi, lililotaka Tanzania iachane na uwindaji.

Ilielezwa kuwa Tanzania imekuwa ikijitetea kuwa uwindaji wake ni endelevu kutokana na kuwapo mfumo wa udhibiti, ikiwa ni pamoja na wanyama kuwa na muda wa kutosha kupumzika na kuzaa.

Ilielezwa kuwa uamuzi wa kurefushwa muda huu bila sababu za msingi, ungeathiri utetezi wa Tanzania katika jumuiya ya kimataifa na hivyo huenda shinikizo lingeongezeka na kuua kabisa biashara ya uwindaji wa kitalii nchini.

Aidha, ilielezwa kuwa Tanzania ilikuwa hatarini kupoteza soko la uwindaji kwa kuwa asilimia zaidi ya 90 ya soko hilo iko Ulaya na Marekani, ambako wanaharakati wa haki za wanyama wamekuwa wakishinikiza uwindaji upigwe marufuku. Ili kuhakikisha kuwa hili linafanyika, wamekuwa wanazitaka nchi zao (destination states) kuzuia nyara za wanyamapori kutoka katika nchi zetu (range states).

Kwa mfano, mwishoni mwa mwaka 2012 mashirika saba yanayotetea haki za wanyama nchini Marekani (The International Fund for Animal Welfare (IFAW), The Humane Society of the United States (HSUS), Humane Society International (HSI), Born Free USA, Born Free Foundation na Defenders of Wildlife) yaliwasilisha pingamizi katika Shirika la Huduma za Samaki na Wanyamapori la Marekani (US Fish and Wildlife Services) kuitaka Serikali ya Marekani kuzuia kuingizwa nyara za simba nchini Marekani, kwa kumuorodhesha simba kama kiumbe aliye hatarini kutoweka kwa mujibu wa Sheria ya Marekani ya “Endangered Species Act” (ESA). Hii ina maana ya kupoteza wateja wa tasnia kutoka Marekani.

Wakati suala hilo bado liko kwenye mjadala na Tanzania na nchi nyingine zenye simba zimewasilisha hoja za utetezi dhidi ya pingamizi hilo, tayari Tanzania imezuiwa isiingize nyara za ndovu.

“Sasa wakati unawasilisha hoja za utetezi halafu unatengeneza mazingira yanayopingana na hoja hizo haina tafsiri nyingine zaidi ya kukosa umakini,” amesema mmoja wa wahifadhi.

Endapo nyara za simba nazo zitapigwa marufuku, ni dhahiri kuwa biashara ya uwindaji wa kitalii itakuwa imekoma hapa Tanzania. Hii inatokana na ukweli kwamba watalii wanaokuja kuwinda huwa wanavutwa na wanyama wachache — simba, chui na ndovu. Kuwaondoa wanyama hao katika orodha ni kuua biashara hiyo.

Ingawa wanyama kama swala, nyumbu na wengine huwindwa pia, lakini hakuna mtalii anayekuja Tanzania mahsusi kwa ajili ya kuwinda wanyamapori hao.

Makala za Martin Fletcher na zawadi aliyopewa kutembelea Tanzania

Kuzuiwa nyara za ndovu kutoka Tanzania kuingia nchini Marekani kumechagizwa mno na makala za Martin Fletcher wa gazeti la Daily Mail on Sunday la Uingereza.

Mwandishi huyo aliandika makala mbaya “iliyoitukana” Serikali ya Tanzania na kuituhumu kuwa haikuwa na nia ya dhati ya kupambana na janga la ujangili wa ndovu.

Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ilizijibu tuhuma hizo. Kwa busara za kawaida hatua hiyo ilikuwa inatosha.

Lakini Nyalandu, kwa kutaka kumfurahisha Rais Kikwete – kumwonesha kuwa anao uwezo mkubwa wa kumtetea – yeye mwenyewe akalipa maelfu ya paundi za Uingereza kwenye Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na kuzijibu zaidi tuhuma hizo kwenye kipindi chao cha HardTalk. Kuna taarifa za uhakika kuwa Nyalandu hakutumwa wala hakuombwa akafanye hivyo.

Ambacho baadhi ya Watanzania hatufahamu, ni kuwa fedha nyingi za umma zilitumiwa na Nyalandu kufanya maandalizi ya kujieleza kwenye mahojiano ya HardTalk. Kuna wanaodai kuwa alijitahidi. Lakini, ukweli unabaki kuwa alichokifanya Nyalandu katika mahojiano yale ni janga kubwa la kitaifa.

Ikiachiliwa mbali udanganyifu alioutoa kwamba Tanzania ina hifadhi ya tani 118,000 za pembe za ndovu – uzito ambao ni zaidi ya uzito wa pembe za ndovu wote walioko dunia hii – ilifikia hatua mwendesha kipindi alimbishia wazi wazi, akipinga majibu aliyokuwa akitoa.

Hatua hiyo ilionesha kuwa mwendesha kipindi alikuwa anauelewa ukweli wa kilichokuwa kikiongelewa kuliko Nyalandu aliyetumia fedha za umma kwenda kutoa ufafanuzi.

Baada ya mahojiano ya HardTalk yaliyokwenda mrama, Nyalandu akalikoroga zaidi kwa kumleta Mwandishi Martin Fletcher nchini Tanzania. Hapo alilenga kumleta ili mwandishi apate uthibitisho wa tuhuma alizokuwa amekwishazitoa. Ziara hiyo iligharimiwa kwa fedha nyingine za umma, ambazo zilipaswa zielekezwe katika mapambano dhidi ya majangili.

Mwaliko na ukarimu wa Nyalandu ukazaa aibu kubwa! Kwanza, mwandishi  huyo aliweka bayana kushangazwa kwake na mwaliko wa Nyalandu! Kwamba matusi yake yamemlipa “scholarship” ya kuja kulala na kutalii bure nchini kwetu. Safari hii Fletcher akamalizia kazi kwa kuivua nguo Serikali ya Tanzania.

Makala zake mbili na “zawadi ya safari” kuja Tanzania, vinaonesha kukosekana umakini katika kupambana na ujangili. Vinaonesha kutokujua tatizo, mikakati na vipaumbele vyenye maslahi kwa maliasili za Tanzania.