Julius Nyerere: Wanaotumia fedha kuomba uongozi hawatufai
“Sisi hapa Tanzania tulikuwa tumeanza utaratibu ambao ukitumia fedha nje ya fedha za chama na Serikali na ukatumia fedha zako mwenyewe katika uchaguzi, tunakutoa. Hufai! Huo ndiyo ulikuwa utaratibu wetu. Tulikuwa tunakuuliza: “Hii nchi ya maskini, wewe mwenzetu una mali umeipata wapi?”
Hayo ni maneno ya Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ndiye Rais wa kwanza wa Tanganyika na baadaye Tanzania.
Mother Teresa: Tunda la imani, upendo, huduma ni amani
“Tunda la ukimya ni sala, tunda la sala ni imani, tunda la imani ni upendo, tunda la upendo ni huduma, tunda la huduma ni amani.”
Maneno hayo ni ya Mtawa wa Kanisa Katoliki wa nchini India, Mother Teresa wa Calcuta.
Carl Jung: Ukijua giza lako utakabiliana na la wengine
“Kujua giza lako mwenyewe ni mbinu bora ya kukabiliana na giza la watu wengine.”
Kauli hiyo ni ya mtaalam wa magonjwa ya akili na mchambuzi wa saikolojia, Carl Gustav Jung wa nchini Uswissi. Alizaliwa Julai 26, 1875. Alifariki Juni 6, 1961.
Fatou Bensouda: Waathirika katika kesi za ICC ni Waafrika
“Tunasema kwamba ICC inawalenga Waafrika, lakini waathirika wote katika kesi zetu katika Afrika ni wa Kiafrika.”
Haya yalisemwa na Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa kivita (ICC), Fatou Bensouda, ambaye ni mwanasheria maarufu wa nchini Ghambia.