Nyerere: Kuna watu wenye kasoro CCM

“Kutokana na umri wake mkubwa, watu wengi wenye kasoro wamejiingiza kwenye chama hiki. Sasa kimekuwa kama kokoro ambalo wakati mwingine hubeba viumbe visivyohitajika. Tunao watu wa ajabu ndani ya CCM ambao hawafanani na CCM.”

 

Maneno haya ni ya Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wakati akikemea watu wasio na sifa ya kuwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Theresa: Uaminifu ni kipimo cha utu

“Kuwa mwaminifu katika mambo madogo kuna maana, kwani ni katika hayo utu wako utapimika.”

 

Hii ni kauli ya Mtawa wa Kanisa Katoliki wa nchini India, Mother Theresa, ambaye pia ni mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel.

 

Lowassa: Ukosefu wa ajira kwa vijana

“Matatizo ya kutozingatia mabadiliko ya uchumi, biashara, siasa, jamii, teknolojia na uwekezaji kwenye programu ya ajira, yanachangia ukosefu wa ajira kwa vijana wengi.”

 

Haya ni maneno ya Waziri Mkuu wa Tanzania aliyejiuzulu na Mbunge wa Monduli mkoani Arusha, Edward Lowassa.


Kafulila: Tuwapime DNA viongozi wetu

“Tunahitaji kuwapima DNA (vinasaba) viongozi wetu kama kweli wana asili ya Tanzania, maana kwa namna wasivyotujali ni kama si Watanzania wenzetu.”

 

Kauli hii ilitolewa na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, wakati akizungumza bungeni kuhusu viongozi wanaotumia madaraka vibaya na kwa kutojali maslahi ya wananchi.