Nyerere: Napenda vyama viwili vya kijamaa
“Mimi binafsi nitafurahi sana kuona Tanzania nayo ikiwa na vyama viwili vya kijamaa; na ikakataa kabisa kabisa kuweka vyombo vyake vya ulinzi na usalama mikononi mwa wapiganaji wa siasa hiyo.”
Baba wa Taifa na Rais wa Awamu ya Kwanza Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyasema haya katika Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Agosti 16, 1990, jijini Dar es Salaam.
Mwinyi: Nilisema ruksa kula chochote utakacho
“Wakati wa uongozi wangu kulitokea vurugu zinazofanana na hizo baada ya watu kuvunja mabucha ya nguruwe, ambayo yalikuwa yanakwaza wale wanaofuata Dini ya Kiislamu. Niliwaambia wananchi ‘ruksa’ kula chochote watakacho, pia nilikuwa sitaki imani ya mtu mmoja kumuudhi mwingine, au ivunje sheria.”
Haya ni maneno ya Rais mstaafu wa Awamu ya Pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, aliyepata pia kuwa Rais wa Zanzibar. Vurugu hizo ndizo zilisababisha akapewa jina la utani la ‘Mzee Ruksa’.
Mtatiro: Nauli zimepanda huduma hazijaboreshwa
“Nauli zimepanda bila huduma kuboreshwa, nadhani hiyo ilikuwa hoja ya msingi ya Sumatra kukataa kupandisha nauli. Watanzania ni maskini, na hivi sasa kila kitu bei yake iko juu, leo tena nauli zinapanda, hapa tunajenga taifa la walalahoi.”
Hii ni kauli ya Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, wakati akikosoa upandishaji nauli za vyombo vya nchikavu na majini ulioanza kutekelezwa nchini Aprili 12, mwaka huu.