Sijatamani na sitatamani kuwa rais wa nchi yetu, kwa sababu nafsi yangu haijapata kunisukuma, moyo haujashituka na akili hazijanishawishi kuwania wadhifa huu. Ingawa napenda kufanya kazi, kusoma na kijifunza maarifa mbalimbali na kusikiliza mawazo na falsafa mbalimbali na uadilifu wa rais mzalendo katika nchi yake. 

Unaweza kusema sina sifa ya kuwa rais. Hilo si jibu. Sifa na uwezo upo, bali moyo wa kuridhia haupo. Moyo wangu umepata kufunguka katika kucharaza maneno gazetini, redioni na runingani. Moyo unaweza pia kufanya kazi nyingi za kitaaluma na kazi ya mtulinga. 

 

Nasema ukicheka umenielewa. Ukishangaa haujanifahamu. Sasa nifuate katika aya zifuatazo. Kutaka na kuweza ni mambo mawili tofauti. Unaweza Kutaka jambo na uwezo hauna. Unao uwezo lakini hautaki. 

Uwezo na matakwa yanakwenda pamoja katika kutenda jambo yakiongozwa na uadilifu katika kauli na matendo. Si marais tu, hata viongozi katika madaraka mbalimbali wanashindwa kutekeleza wajibu wao kwa sababu uwezo na matakwa yao yako nje ya uadilifu. 

Soma nukuu hii: “Inatupasa tutumie muda vizuri na siku zote tukumbuke kwamba muda huenda sahihi.” Mwisho wa nukuu. Ni Rais wa Kwanza wa Afrika Kusini, Nelson Rolihlahla Mandela (kuanzia mwaka 1994 – 1999).

Rais Mandela anatumia uwezo na uadilifu wake kuthubutu kuwakumbusha na kuwasihi wananchi wa Afrika Kusini (hata Afrika) kwamba muda ni mali na utumike kupata mafanikio na kuongeza maarifa ya kufanya kazi kwa ufanisi. Muda usipotezwe, ukipita haurudi. Fikiri kwa kina. 

 

Angalia nukuu hii: “Ushindi una baba wengi, ila kushindwa ni yatima.” Mwisho wa nukuu. Ni Rais wa 35 wa Marekani, John Fitzgerald Kennedy (kuanzia mwaka 1961 – 1963). Aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiopenda kuona baba wengi wanashinda katika kukuza uchumi na ushirikiano kati ya Marekani na nchi nyingine duniani. 

Rais Kennedy anatufahamisha daima wananchi wazalendo wanapenda kuona mafanikio ya kazi za viongozi wao pamoja na kazi za wananchi wenzao, katika kuinua na kudumisha masilahi yao. Viongozi wanaposhindwa kufanya hivi, wananchi huwa yatima na wanakosa watu wa kuwalea na kuwafariji. Tafadhali zama zaidi katika nukuu hii. 

 

Kila mtu anapenda ushindi ambao ni furaha na uhai. Kushindwa ni huzuni na ufu. Taifa lisilotaka ushindi wa kiuongozi, kiuchumi na kijamii ni taifa maskini, mithili ya yatima wasiopewa misaada na wanaodhulumiwa haki zao. 

Weka jicho lako katika nukuu hii: “Sijaribiwi na sitajaribiwa.” Mwisho wa nukuu. Ni Rais, Dk. John Pombe Magufuli wa Tanzania (kuanzia mwaka 2015 hadi sasa). Ni maneno yenye kuonyesha msimamo. Ndiyo yale niliyozungumza awali, UWEZO. Hauwezi kuthubutu kusema iwapo hauna msimamo. 

Viongozi wengi huonekana kubabaika au kuhofu kutoa uamuzi kwa kukosa uwezo na msimamo. Penye msimamo hakuna mtetemeko au myumbisho kufikia malengo. Kiongozi anapokuwa na uwezo na msimamo hupukutisha wapambe wasaliti na wanafiki wanaokusudia kupindisha mwelekeo wake asipate mafanikio. 

Malizia kwa kutafakari nukuu ifuatayo: “Mtanzania wa leo hawezi kununua watu bila kwanza yeye kununuliwa.” Mwisho wa nukuu. Ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Kwanza wa Tanganyika na Tanzania. (kuanzia mwaka 1962 – 1985).

Hii ni hadhari kwa kiongozi yeyote na ni nasaha kwa mwananchi asirubuniwe kupoteza utu na haki zake za ubinadamu. Hasa mtu unapokuwa kiongozi busara itawale na uadilifu ushamiri. Ama sivyo watu hawatakuelewa. Kiongozi huru ndiye taifa huru, na taifa huru ndiye mwananchi huru.