Jiji la Dar es Salaam ni moja ya majiji yanayoongoza kwa idadi kubwa ya wakazi hapa nchini. Hali hiyo inasababishwa na ongezeko la watu wanaoingia jijini kila kukicha, wakitokea mikoa mingine katika harakati za kutafuta maisha bora, ambayo wengi wao wanaamini kuwa yanaweza kupatikana Dar es Salaam.
Ongezeko la watu jijini Dar es Salaam limesababisha mambo mengi likiwamo la ujenzi holela katika baadhi ya sehemu za halmashauri za manispaa tatu za jiji hilo. Kitu kingine kinachoambatana na tatizo hilo ni msongamano wa magari katika barabara mbalimbali za Dar es Salaam – Kinondoni, Temeke na Ilala.
Katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke tatizo la msongamano wa magari na maegesho holela limeshika kasi kama ilivyo katika halmashauri za manispaa za Kinondoni na Ilala. Moja ya mambo yanayosababisha msongamano wa magari ni maegesho holela, gereji bubu na magari ya abiria kutofuata taratibu za kupakia abiria katika vituo vyake maalum.
Ili kupambana na tatizo hili, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke imeiteua Kampuni ya Alcon System Security kama wakala wake wa kudhibiti tatizo la maegesho holela katika manispaa hiyo.
“Kuna sheria ndogo ndogo (by-laws) zinazotuongoza kuhusu suala zima la usafiri na kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam na hii ni kwa manispaa zote. Tulifuata taratibu zote, tukatangaza tenda na Kampuni ya Alcon System Security ikashinda tenda, na sasa ndiyo wakala wetu katika kutekeleza kazi hiyo,” alisema Meya wa Manispaa ya Temeke, Maabadi Suleiman Hoja.
Mbali na udhibiti wa maegesho holela, Kampuni ya Alcon System Security pia inafanya kazi ya kukamata taksi bubu katika maeneo mbalimbali ya Temeke. Chini ya utaratibu huu, zinakamatwa taksi ambazo hazijasajiliwa na zinazoegesha katika maegesho ambayo ni tofauti na zilizosajiliwa.
Hali kadhalika, kampuni hiyo inadhibiti magari yote yanayopakia abiria bila ya kuwa na kibali cha kupakia abiria. Alcon System Security inadhibiti magari yanayotumia barabara bila kuzingatia uzito wake. Lakini pia kwa mamlaka iliyopewa na Manispaa ya Temeke, kampuni hiyo pia inakamata bajaji zote ambazo hazina ufito (sticker) wa Sumatra.
“Sumatra iliziagiza manispaa zote kukamata bajaji zote ambazo hazina ufito wa Sumatra, kwa hiyo kazi hii pia tumepewa sisi kwa upande wa Temeke,” anasema Meneja wa Kitengo cha Operesheni cha Kampuni ya Alcon System Security, Adelardo Marcel.
Kampuni hiyo pia inafuatilia taksi ambazo hazijalipa mapato ya manispaa. “Zipo taksi ambazo zimesajiliwa lakini hazijalipa mapato ya manispaa, hizi nazo pia huwa tunazikamata ili zikalipe,” alisema Marcel.
Suala la weledi katika utendaji wa kazi ni jambo la muhimu sana. Kuna wakati baadhi ya wananchi katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Temeke, wamekuwa wakihoji uwezo wa baadhi ya wafanyakazi wa kampuni ya Alcon System Security katika utendaji wao wa kazi.
Tatizo linalolalamikiwa na wananchi katika utendaji ni pale baadhi ya wafanyakazi wanapoamua kutumia vitisho na nguvu za ziada isipotakiwa, na hata wakati mwingine kudaiwa kutaka rushwa ili kutatua tatizo bila kufika mahala panapohusika.
“Mimi waliwahi kunikamata kabla hatujafika katika maegesho yao yaliyoko pale Temeke Hospital, mmoja wao akaniomba Sh 80,000 baada ya hapo wakaniachia,” alisema mzee mmoja aliyedai kuwa gari lake lilikamatwa akiwa eneo la Mbagala Misheni akinywa supu katika baa fulani. Mzee huyo anadai kuwa alikuwa ameegesha gari lake pembeni mwa barabara karibu na baa hiyo.
Meya Hoja anasema kuwa ni vigumu sana kupima uweledi wa wafanyakazi wa Kampuni ya Alcon System Security kwa sababu katika utaratibu wa kushinda tenda ni makaratasi tu ndiyo yanayoeleza utendaji wa kampuni hiyo na si mtu mmoja mmoja.
“Kwetu kama manispaa huwa tunatoa tenda kutokana na maelezo ya mwombaji. Labda niseme kuwa endapo malalamiko kama haya yakitufikia na yakazidi kuwa mengi, tuna uwezo wa kuwanyima tenda wakati ujao kwa sababu hata mwaka jana tulikuwa na kampuni nyingine ambayo utendaji wake ulikuwa mbaya tukawanyang’anya kazi,” alisema Meya Hoja.
Meya Hoja anatoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika mara tu watakapoona kuwa hawajatendewa haki katika jambo hili. Hata hivyo, meya huyo anawaasa wananchi kuepuka tabia ya kutaka kufanya mambo kwa harakaharaka, hali ambayo anasema kuwa kwa namna moja ama nyingine inachangia vitendo vya rushwa.
“Rushwa ipo kila sehemu hapa duniani na kinachosababisha hayo yote ni binadamu kuwa na haraka na kutaka kufanya mambo kwa njia ya mkato,” alisema.
Kwanini magari mengi yamekuwa yakivutwa baada ya kukamatwa? Kwa mujibu wa Meneja wa Kitengo cha Operesheni cha Kampuni ya Alcon System Security, Marcel, magari mengi yanafikia hatua ya kuvutwa kwa sababu ya ubishi wa madereva na ukaidi wa matajiri pale wanapoambiwa kuwa magari yao yamekamatwa.
Hali kadhalika, kwa mujibu wa Marcel, kuna baadhi ya kampuni ambazo huwatia jeuri madereva wake kwa kuwaelekeza kwamba hawana haja ya kufuata taratibu za kulipa faini pale watakapokamatwa.
“Kuna kampuni moja ambayo tulikamata gari lake baada ya kufika katika ofisi za kampuni hiyo tukakuta maelekezo ya ajabu kwa madereva wake, mojawapo likiwa la kukaidi amri pale atakapokamatwa na kosa mahali popote. Sasa hii haitoi ushirikiano hata kidogo na matokeo yake sisi tunaonekana wabaya,” alisema Marcel.
Polisi kuvuta magari
Kumekuwa na matumizi ya gari la polisi katika kufanikisha shughuli nzima la kudhibiti maegesho holela na hasa katika kuvuta magari. Hatua hiyo imekuwa ikiwapa hofu baadhi ya wananchi wa maeneo ya Temeke, wakijaribu kuhoji uhusiano wa Kampuni ya Alcon System Security na Polisi.
Marcel anasisitisa kuwa kampuni yake imekuwa katika uhusiano mzuri na Jeshi la Polisi. Lakini pia taarifa kutoka katika kikosi cha matengenezo ya magari ya Polisi zimethibitisha kuwa kitengo hicho kina mkataba maalum na wakala huyo wa manispaa katika kufanikisha kazi hiyo.
“Kuna wakati Mkuu wa Jeshi la Polisi aliwahi kutoa wito kwa vitengo mbalimbali vya jeshi hili kubuni mbinu za kuongeza mapato, kwa hiyo hata sisi tumeingia mkataba maalum na wakala wa manispaa katika hili, lakini mwisho wa siku tunaingiza mapato kwa upande wetu,” kilisema chanzo cha habari kutoka Kitengo cha Matengenezo ya Magari ya Polisi.
Kuhusu faini za makosa mbalimbali, Marcel anasema gari ndogo (saloon) ambalo linakutwa kinyume cha taratibu za maegesho faini yake ni Sh 80,000. Katika malipo haya Sh 30,000 zinalipwa katika ofisi za wakala (Alcon System Security) na Sh 50,000 zinalipwa katika Ofisi za Manispaa.
Magari ya kati (mfano Fuso, Canter) faini yake ni Sh 160,000. Manispaa Sh 100,000 na Wakala anapata Sh 60,000. Magari makubwa kama vile ya mafuta faini yake ni Sh 200,000. Manispaa inalipwa Sh 120,000 na wakala anapata Sh 80,000.
Bajaji ambayo haina ufito wa Sumatra inalipa faini ya Sh 80,000, Sh 30,000 zinakwenda kwa wakala na Manispaa inalipwa Sh 50,000.
Maelezo ya Marcel yanathibitisha kuwa gharama za kuvuta gari hadi kwenye maegesho ya manispaa hutegemea ukubwa wa gari na hata umbali uliopo kutoka eneo la tukio. Aidha, anasema kuwa jukumu la kumlipa mwenye kuvuta gari linakuwa kwa mwenye gari.
Anafafanua kuwa uvutaji wa gari uko wa aina mbili. Kwanza kuna gari linalovutwa baada ya mwenye gari kukaidi amri, lakini pia kuna gari ambalo limeharibika mahala fulani na likapewa muda fulani liwe limeondolewa.
“Huwa hatukurupuki kuvuta gari la mtu bila kuzingatia taratibu. Kwa mfano, utakuta mtu kapaki gari sehemu anashusha mizigo, hajawasha taa za kutoa ishara yoyote na wala hakuna viashiria ambavyo vinatakiwa kuwapo kwa mujibu wa sheria, hili tunalivuta. Wakati mwingine gari ni bovu liko sehemu na hakuna ishara yoyote na dereva au utingo yuko ndani amechapa usingizi, hili nalo tunavuta kwa sababu kuna sheria zimekiukwa,” alisema.
Rushwa katika utendaji
Marcel anakubali kuwa huenda rushwa zipo na hata lile tatizo la vijana wake kuwatisha wananchi anakubaliana nalo.
Ili kudhibiti vitendo hivyo anasema kuwa kwa sasa wana magari maalum ambayo yanafuatilia utendaji wa vijana wake wanapokuwa katika maeneo mbalimbali.
“Siku hizi kuna watu nimewaweka kufuatilia utendaji wa kazi, ambao kazi yao ni kuandika namba za magari yote yanayokamatwa. Jioni wakati wa majumuisho ndiyo tunaanza kuulizana moja baada ya jingine,”
“Hii imesaidia sana kupunguza vitendo vya rushwa, adhabu ambayo imekuwa ikitolewa kwa wafanyakazi wenye tabia kama hizi ni kulipa gharama za magari waliyoyakamata au kusimamishwa kazi mara moja,” alisema.
Marcel anatoa wito kwa wananchi kuwa endapo wataona kuna dalili za vitendo vya rushwa, ni bora wakaomba kitambulisho cha huyo aliyemkamata na hata kama ikiwezekana kupiga picha namba ya gari.
“Kwa njia hii itakuwa rahisi kufuatilia vitendo vya rushwa kwani kutakuwa na ushahidi kwa kiasi fulani,” alisema.
Changamoto
Kwa mujibu wa Marcel, moja ya changamoto ambazo zimekuwa zikiwakumba wafanyakazi wa Kampuni ya Alcon katika utendaji wa kazi ni vipigo kutoka kwa wananchi.
“Hali kadhalika, kuna kundi la baadhi watu wachache ambao bado wanakaidi amri. Kumekuwa pia na matatizo katika matumizi ya yadi ya Temeke, hali ambayo imetusababishia kukwama kidogo katika udhibiti wa gereji bubu.
“Kwa sasa tumepata yadi mpya na muda si mrefu gereji bubu zitadhibitiwa ipasavyo,” alimalizia.