Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), umesema unatarajia kuandikisha wanachama milioni 21 kutoka sekta isiyo rasmi, huku umri wa kuchangia ukiwa ni kuanzia miaka 15 hadi 70 na kiwango kikianzia Sh. 30,000 na zaidi kwa mwezi.

Aidha, watu walio kwenye ajira wanaruhusiwa kuchangia michango yao kama namna nyingine (uchangiaji wa hiyari) ya kuweka akiba ya uzeeni kupitia mfuko huo.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mashomba, wakati akizungumza na wahariri wa habari kuhusu safari ya kuelekea kutoa huduma kwa sekta isiyo rasmi kwa kuwa na skimu maalum kwa ajili hiyo.

“Tunatarajia kuandikisha wanachama milioi 21 kutoka sekta isiyo rasmi ambapo umri wa kuchagia ni kuanziamiaka 15 hadi 70 nia ni uwawezesha kuweka akiba ya uzeeni,” amesema.

Mashomba amewataka Watanzania kujiunga na mfuko wa sekta isiyo rasmi (National Informal Sector Scheme-NISS) ambao unatoa fursa kwa wanachama kuchangia kuanzia shilingi 30,000 kila mwezi jambo ambalo litasaidia kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Lulu Mengele akizungumza jambo katika mkutano wa Wahariri wa Vyombo vya Habari na uongozi wa mfuko huo uliofanyika leo Oktoba 1, 2024 jijini Dar es Salaam.

Mfuko huo unatoa fursa kwa mwananchi yeyote aliyejiajiri katika sekta isiyo rasmi ikiwemo kilimo, ufugaji, uvuvi, uchimbaji mdogo wa madini, sanaa mbalimbali, biashara ndogo ndogo, mama lishe au baba lishe, bodaboda, machinga pamoja na wanahabari wa kujitegemea na kuchangia kidogo kidogo kwa siku, wiki, mwezi, muhula au msimu.

Amesema kuwa NSSF imefanikiwa kupiga hatua kubwa za utendaji ikiwemo kuboresha mifumo ya teknolojia pamoja na kukuza mtaji kwa asililimia 70 kutoka shilingi trillion 4.8 kwa mwaka 2021 hadi kufikia trillion 8.5.

Mshomba amesema kuwa mfumo wa teknolojia umewasaidia wanachama wa NSSF kupata taarifa kwa wakati wakiwa mahali popote pamoja na kuondoa usumbufu uliokuwepo awali.

“Lengo ni kuwafikia watu wengi katika sekta binafsi pamoja na sekta isiyo rasmi, tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suruhu Hassani kwa kutupa ushirikiano katika kuendeleza mfuko wa NSSF” amesema Mshomba.

Amesema NSSF imeboresha mifumo ya TEHAMA na hadi kufika Juni mwaka huu asilimia 80 ya huduma zote zitakuwa zinatolewa mtandaoni, ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 40 miaka mitatu iliyopita.

“Wanachama wetu wengi walikuwa wanalazimika kuja kwenye ofisi zetu kupata huduma, sasa tumekuja na portal inayomwezesha mwanachama kuhudumiwa popote alipo kwa kupitia simu au kompyuta. Kwa sasa unaweza kuanza na kukamilisha mchakato wa mafao yako mtandaoni,” Alisema Meneja Mifumo wa NSSF, Mathayo Mihayo na kuongeza;

“Tunataka tufikie asilimia 100 ya mambo yote kufanyika kiganjani au mtandaoni, hadithi ya mteja kusumbuliwa haitakuwapo tena, tuliona wakati mwingine unawaita wazee waje ofisi kurekebisha taarifa wakati unaweza kuwatengenezea mfumo wa kuzirekebisha kwa urahisi wakiwa kokote.” alisema.

Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari wakimsikiliza Mkuu Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF)  Bw. Masha Mshomba.

Akizungumzia huduma ya sekta isiyo rasmi, Mkurugenzi Uendeshaji NSSF, Omary Rufia, amesema kuwa huduma hiyo imelenga kuwasaidia wafanyabiashara wadogo nchini.

“Tutaendelea kutoa elimu kwa jamii ili waweze kujiunga na mfuko huu na kunufaika kiuchumi katika maisha yao pamoja na kusaidia juhudi za Serikali za kupunguza umaskini wa kipato kwa wananchi” amesema Rufia.

Amesema kuwa wamejikita kuongeza wigo wa hifadhi ya jamii kwa makundi ambayo hayanufaiki na huduma za NSSF ingawa wanashiriki kikamilifu kuchangia uchumi wa Taifa.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania ( TEF) na Afrika Mashariki Deodatus Balile, ameipongeza NSSF kwa kuboresha utendaji wa majukumu ikiwemo mifumo ya teknolojia ya kutoa taarifa kwa wanachama.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania ( TEF) na Afrika Mashariki Deodatus Balile akizungumza jambo katika mkutano wa Wahariri wa Vyombo vya Habari na uongozi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) jijini Dar es Salaam.

Balile amesema kuwa NSSF imefanya kazi kubwa katika kuboresha utendaji kazi, huku akitoa wito wa kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ili kulisaidia Taifa na kupiga hatua kimaendeleo.

“NSSF mnatakiwa kuanzisha ajenda za msingi za utekelezaji wa miradi ya kisasa kwa ajili ya kuwasaidia wananchi, kama mlivyotekeleza mradi wa ujenzi wa daraja la Kigamboni ambao umekuwa na manufaa makubwa kwa watanzania” amesema Balile.

Wakizungumzia umuhimu wa kujiunga na NSSF Wahariri wastaafu akiwemo Bakari Machumu pamoja na Flora Wingia, wamesisitiza umuhimu wa kujiunga na mfuko huo kwani unamanufaa mazuri baada ya kustaafu kwa kuwasaidia kuishi maisha rafiki lenye kuleta tija katika uchumi.

Katika mkutano huo NSSF ilitoa tuzo kwa waajiri wa sekta ya habari wanaopeleka michango ya wanachama wao kwa mujibu wa sheria bila kuchelewesha na Kampuni ya Jamhuri Media Limited ilikuwa moja ya kampuni za habari zilizokidhi vigezo hivyo.

Vyombo vya habari vingine ni Mwananchi Communication Ltd, ITV, Azam Media Ltd.

Pia wametoa tuzo ya shukrani kwa baadhi ya wahariri ambao wamekuwa wakifanya kazi ya kuhamasisha wahariri wa vyombo vya habari kutochukua fedha za kustaafu mapema ili ziweze kuwasaidia uzeeni.