Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
Katika juhudi za kutambua mchango wa sekta binafsi katika kukuza uchumi, Serikali imewezesha ukuaji mkubwa wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), ambapo thamani ya mfuko imeongezeka kwa asilimia 92, kutoka TZS bilioni 4,836.73 mwezi Februari 2021 hadi TZS bilioni 9,299.39 mwezi Februari 2025.
Hayo yameelezwa leo, Machi 17, 2025, Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF,Masha Mshomba ambaye amesema ongezeko hilo limechangiwa na kuongezeka kwa wanachama, mapato yatokanayo na michango, na kukua kwa thamani ya vitegauchumi vya Mfuko. Mwenendo huu mzuri unaashiria uhimilivu na uendelevu imara wa Mfuko.

Amesema, katika kipindi cha miaka minne kilichoanzia Machi 2021 hadi Februari 2025, jumla ya wanachama wapya 1,052,176 wameandikishwa. Serikali ya Awamu ya Sita imefanikisha mikakati mbalimbali ya kuimarisha uchumi na kufungua fursa za uwekezaji na biashara, hatua ambayo imekuwa na manufaa makubwa katika ukuaji wa sekta za viwanda, biashara, kilimo, utalii, na miundombinu.
“Katika kipindi hicho, Mfuko umeandikisha wanachama wapya 1,052,176, na matokeo ya jitihada hizo yamekuwa na athari chanya katika ukuaji wa sekta za viwanda, kilimo, utalii, na miundombinu,” alisema.
Alitaja baadhi ya miradi mikubwa iliyochangia ongezeko hili kuwa ni pamoja na ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere, Mgodi wa Nyanzaga, Kiwanda cha Mbolea cha Intracom, Kiwanda cha Vifaa vya Umeme cha Elsewed Electric East Africa Ltd, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, na Mgodi wa Uchimbaji wa Madini ya Nikeli (Tembo) uliopo Ngara.
Miradi mingine ni Daraja la Kigongo-Busisi Mwanza, Kiwanda cha Sukari cha Bagamoyo, Kiwanda cha Mkulazi Morogoro, na mradi wa reli ya kisasa ya SGR. Hizi ni baadhi ya fursa za uwekezaji ambazo zimechangia pakubwa katika ongezeko la wanachama na michango inayochangia ukuaji wa Mfuko, ambapo jumla ya TZS bilioni 6,994.52 zimekusanywa.

Mkurugenzi Mkuu alifafanua kuwa Mfuko umeongeza uwezo wake wa kukusanya michango, ambapo jumla ya TZS bilioni 6,994.52 zimekusanywa kutoka kwa wanachama, na michango ya mwaka imeongezeka kutoka TZS bilioni 1,131.92 katika mwaka ulioishia Februari 2021 hadi TZS bilioni 2,153.13 katika kipindi kilichoishia Februari 2025, sawa na ongezeko la asilimia 90.
“Thamani ya vitegauchumi vya Mfuko imeongezeka kwa asilimia 92, kutoka TZS bilioni 4,283.32 katika mwaka ulioishia Februari 2021 hadi TZS bilioni 8,212.92 katika mwaka ulioishia Februari 2025,” alifafanua.
Kuhusu ustahimilivu wa Mfuko, Mkurugenzi huyo alisema tathmini ya uhai na uendelevu wa Mfuko imefikia asilimia 90.7, ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 87.7 iliyoonekana katika tathmini ya mwaka 2020. Hii inaashiria kwamba Mfuko upo katika hali nzuri, ambapo malipo ya mkupuo wa awali ya mafao ya wastaafu yameongezeka na kiwango cha chini cha pensheni kimeboreshwa.
Aidha, Mfuko ulilipa mafao ya TZS bilioni 3,108.89, na malipo ya mafao kwa mwaka yaliongezeka kwa asilimia 69, kutoka TZS bilioni 537.08 katika mwaka ulioishia Februari 2021 hadi TZS bilioni 909.16 katika mwaka ulioishia Februari 2025.

Mshomba ameongeza kuwa, kutokana na mabadiliko ya kanuni za ulipaji mafao ya kustaafu (kikokotoo) yaliyofanyika na kuanza kutekelezwa mwezi Julai 2022, wastaafu wa NSSF walianza kupokea mkupuo wa awali wa asilimia 33, ukilinganisha na asilimia 25 waliyokuwa wakilipwa kabla ya mabadiliko hayo. Kutokana na utendaji mzuri wa Serikali ya Awamu ya Sita, wastaafu waliokuwa wanalipwa mkupuo wa asilimia 33 waliongezewa kiwango cha mkupuo hadi asilimia 35 kuanzia Julai 2022.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu aliongezea kuwa Mfuko upo kwenye hatua za mwisho za kuboresha kiwango cha kima cha chini cha pensheni kwa wastaafu kutoka TZS 100,000 hadi TZS 150,000. Viwango vingine vya pensheni vinatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 2 hadi 20. Utekelezaji wa maboresho haya utaanza mara moja baada ya taratibu za uidhinishwaji kukamilika, na utahusisha kipindi kuanzia Januari 1, 2025.