Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoani Pwani, imetoa rai kwa mtumishi ama mtendaji yeyote anaejihusisha na vitendo vya rushwa kuacha mara moja vitendo hivyo kwani vinachangia kuzorotesha utoaji wa huduma kwa wateja.
Akifungua maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja kimkoa, Meneja wa NSSF Mkoani Pwani, Witness Patrick ,ameeleza wanashirikiana na Taasisi ya kupambana na kuzuia rushwa (TAKUKURU) kudhibiti mazingira ya vitendo vya rushwa kwenye maeneo ya kazi.
Amewaasa kila mmoja kujitathmini na kuchukua hatua za haraka kukabiliana na vitendo vya rushwa ili kudumisha imani kwa wanachama na wadau.
“Mfuko hautamvumilia mtendaji yeyote atakaeshindwa kuendana na viwango na kasi ambayo mfuko unatarajia kuifikia hivyo ,kila mmoja wetu kwa nafasi yake ajitathmini na kuchukua hatua za kutekeleza majukumu aliyopangiwa kwa weledi ili kumaliza changamoto za malalamiko “amesema Witness.
Ameeleza ,rushwa Ina madhara makubwa kwa mfuko na kwa kila mmoja lakini pia ni adui wa haki na inaharibu sifa nzuri ya mfuko ambayo imejengeka kwa kipindi kirefu.
“Nichukue fursa hii kusisitiza juu ya masuala hayo yanayochafua taswira ya mfuko licha ya mafanikio makubwa ambayo mfuko umeyafikia kwa kipindi cha mwaka 2022/2023.”
“Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inapinga rushwa kwa vitendo,nasi tunaunga mkono juhudi hizi za serikali kwa kukemea masuala yote ya rushwa” amefafanua Witness.
Amewaomba wanachama na wateja ,kutambua kuwa huduma zinazotolewa na mfuko ni bure na ni wajibu wa kila mtumishi kutoa huduma kulingana na mkataba wa huduma kwa wateja uliopo kwenye tovuti ya Mfuko.
Vilevile Witness amewahimiza ,watumishi na wananchi wema kutoa taarifa za vitendo vya rushwa vinavyotendeka katika maeneo yao ya kazi kwani kutokutoa taarifa ni kushiriki rushwa.
Sambamba na hayo, mfuko utaandaa utaratibu wa kuwazawadia watoa taarifa na zoezi hili litafanyika kwa siri.
Halikadhalika,” anawasihi kutumia mfumo mpya wa NISS katika kuandikisha wanachama wengi zaidi wa mfumo was kujichangia kwa hiari ili kuongeza wigo wa kinga ya Hifadhi ya Jamii kwa wananchi.
Nae mwanachama wa Nssf Kibaha, Vicent Ndumbili aliipongeza Nssf kwa kujali wateja wake.
“Kikweli huduma zao ni nzuri, nimshukuru na Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa kudhibiti masuala ya rushwa ,na kuendelea kuhahakikisha anasimamia Taasisi za kupambana na rushwa katika utoaji wa huduma kwa wananchi,na kupinga vikali “amesema Ndumbili.
Maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja ilianzishwa rasmi kimataifa mwaka 1984 kwa lengo la kutambua umuhimu wa huduma bora kwa wateja na juhudi za wafanyakazi wanaotoa huduma bora kwa wateja ambapo mwaka huu 2023 yanaanza octoba 2-octoba 6 kilele.