Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Ikiwa ni sehemu ya dhamira yake ya kusaidia maendeleo ya sekta elimu nchini, Benki ya NMB imekabidhi madawati na meza yenye thamani ya shilingi milioni 20 kwa shule tatu za wilaya ya Ilala, Mkoani Dar es Salaam zikiwemo Shule ya Msingi Kiwalani, Shule ya Sekondari Tambaza na Shule ya Sekondari Jangwani ikiwa ni utekelezaji wa Mkakati wa Uwekezaji kwa Jamii (CSI) wa benki hiyo mwaka huu.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vifaa hivyo iliyofanyika katika Shule ya Sekondari ya Tambaza jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam, Dismas Prosper alisema kuwa msaada wa benki hiyo unalenga kurejesha kwa jamii ambapo Benki hiyo inafanyia kazi.
“Tunafuraha kukabidhi madawati na meza kwa shule tatu katika Wilaya ya Ilala kama sehemu ya juhudi zetu za kusaidia maendeleo ya sekta ya elimu. Tunaamini juhudi zetu zitasaidia sana kuweka mazingira mazuri ya kujifunzia,” amebainisha.
Alisema sekta ya elimu ni miongoni mwa vipaumbele muhimu katika mkakati wa Uwajibikaji kwa Jamii wa benki yake ndiyo maana Benki imekuwa ikiwekeza kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa sekta hiyo.
“Sisi kama benki ya NMB tunaamini kuwa elimu ndiyo ufunguo wa maisha. Kama sehemu ya kusaidia miradi ya maendeleo endelevu Tanzania nzima, Benki ya NMB kwa miaka saba imekuwa ikitenga asilimia moja ya faida yetu baada ya kodi ili kusaidia sekta muhimu zinazogusa jamii moja kwa moja zikiwemo elimu, afya na mazingira,” alisema.
Prosper wakati wa hafla hiyo aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kuendelea kusaidia maendeleo ya sekta ya elimu.
“Serikali ya Awamu ya Sita imesaidia sana katika kuweka msingi muhimu katika suala la miundombinu kwa kujenga vyumba vya madarasa nchi nzima. Ni wajibu wetu kama washirika wa maendeleo kuhakikisha kuwa shule zina mahitaji yote ya kufanya kazi kwa ufanisi,”
Naye Naibu Spika wa Bunge ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Ilala, Mussa Azan Zungu wakati wa hafla hiyo aliipongeza Benki ya NMB kwa mchango mkubwa katika kuunga mkono mipango mbalimbali ya maendeleo ya Serikali.
“Benki ya NMB imekuwa mstari wa mbele kuunga mkono mipango mbalimbali ya Serikali na nachukua fursa hii kuupongeza uongozi na bodi yake kwa msaada wao,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo wakati wa hafla hiyo alisisitiza dhamira ya Serikali kuendelea kusaidia maendeleo ya sekta ya elimu ndiyo maana Serikali chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni imekuwa ikiwekeza kwa kiasi kikubwa katika kuendeleza sekta hiyo.
“Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya elimu hivyo Dk. Samia Suluhu Hassan anastahili pongezi kubwa kwa hilo. Kwa upande wa Wilaya ya Ilala, Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 2 hadi sasa kusaidia maendeleo ya sekta ya elimu.
Awali Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Tambaza Hussein Mavunda aliipongeza benki hiyo kwa kusaidia maendeleo ya shule kwa miaka mingi sasa na kuongeza kuwa,” Rafiki kwenye uhitaji ndie rafiki wa kweli. Tumekuwa tukituma maombi ya msaada kutoka benki mbalimbali lakini benki ya NMB haijawahi kushindwa kutusaidia”