Benki ya NMB imepata mikopo miwili ya muda mrefu na dhamana ya kukopesha kutoka taasisi tatu za fedha za Jumuiya ya Ulaya (EU) yenye thamani ya sh. bilioni 572 kwa ajili kuendeleza sekta binafsi na kusaidia ujumuishaji wa kifedha nchini.

Makubaliano ya ufadhili huo yalitiwa saini jijini Dar es Salaam kwenye kilele cha kongamano la biashara kati ya Tanzania na Jumuiya ya Ulaya Ijumaa wiki iliyopita na kushuhudiwa na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt Hussein Mwinyi.

Jumla ya mikopo iliyoipata NMB ni bilioni 546. Dhamana ya kusaidia kuwakopesha wajasiriamali ni TZS bilioni 26 kutoka Benki ya Maendeleo ya Ujasiriamali ya Uholanzi (FMO).

Mashirika yaliyoikopesha benki hiyo ni Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) iliyotoa Euro milioni 100 huku FMO kwa kushirikiana na Taasisi ya Ufaransa ya Kufadhili Maendeleo (Proparco) zikiipa NMB dola za Kimarekani 125.

Akizungumza kabla ya utiaji saini hizo, Mhazini wa NMB, Bw Aziz Chacha, alisema fedha walizozipata zitasaidia kuwakopesha wajasiriamali wadogo na wakati hasa biashara zinazomilikiwa na wanawake na vijana pamoja na uwekezaji kwenye shughuli za uchumi wa bluu.

Aidha, afisa huyo mwandamizi alibainisha kuwa fedha hizo zimepatikana wakati muafaka kusaidia ukopeshaji unaofanywa na benki hiyo ambayo mwaka jana ilitoa mikopo mipya yenye thamani ya TZS trilioni 1.3.

“Ufadhili huu utatuwezesha kuongeza ukopeshaji endelevu na jumuishi kwa ajili ya ukuaji wa biashara zinazomilikiwa na kusimamiwa na akina mama pamoja na maendeleo ya shughuli za uchumi wa bluu,” Bw Chacha alibainisha huku akiipongeza serikali kwa sera stahiki zinazowavutia wafadhili na mitaji ya kimataifa.

Mbali na kufadhili biashara za wanawake na miradi ya uchumi wa bluu, fedha ilizozipata NMB zitatumika pia kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati wa kilimo biashara.

Bw Chacha alisema makubaliano yao ya ufadhili na FMO na Proparco yanaonyesha imani ambayo taasisi hizo mbili zinayo kwa Benki ya NMB na ni ishara ya kukua kwa benki hiyo kama mshirika anayekubalika katika harakati za upatikanaji wa ufadhili endelevu kwa wote.

“Kupitia mkopo huu, tunaamini ufadhili tuliopata utakuwa na matokeo makubwa kwa wajasiriamali nchini, biashara zinazomilikiwa na wanawake pamoja na kilimo biashara, shughuli ambazo kwa pamoja zinaajiri takribani asilimia 70 ya watanzania wote,” Bw Chacha alibainisha.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi za Fedha wa FMO, Bw Marnix Monsfort, alisema walichokifanya wao ni pamoja na kuisaidia NMB katika nyanja za kuboresha mazingira, shughuli za kijamii na utawala bora.

Mhazini wa Benki ya NMB, Aziz Chacha (kulia) pamoja na mkurugenzi wa taasis za fedha wa Benki ya maendeleo ya ujasiriamali ya Uholanzi (FMO), Marnix Monsfort (wapili kushoto) wakionesha mikataba ya makubaliano baada ya utiaji saini ambao Benki ya NMB itapatiwa Dhamana ya kusaidia kuwakopesha wajasiriamali yenye thamani ya shilingi bilioni 26 kutoka taasis hiyo ya kiholanzi. makubaliano haya yamesainiwa katika kongamano la biahara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya lililofanyika jijini Dar es Salaam

Afisa Mtendaji Mkuu wa Proparco, Bw Francoise Lombard, alisema ufadhili wao umezingatia zaidi ujumuishaji kifedha wa wajasiriamali, wanawake na wote wanaojihusisha na shughuli za kilimo biashara.

Dhamana ya FMO imetolewa chini ya mpango wa NASIRA ambao lengo lake kuu ni kuzisaidia taasisi za fedha kuongeza kuwakopesha wajasiriamali wadogo na wa kati katika nyanja za biashara ambazo hazipati mikopo ya kutosha.

“Kupitia mpango huu wa NASIRA ambao umewezeshwa na Tume ya Ulaya pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje ya Uholanzi, tunaenda kuisaidia NMB kuweza kuyafadhili makundi haya ambayo yana changamoto ya kupata mikopo hususani wajasiriamali kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo, pamoja na biashara za akina mama na vijana,” Bw Monsfort alifafanua.

Ufadhili wa NMB kutoka EIB ni sehemu ya mikopo yenye thamani ya Euro milioni 270 ambazo benki hiyo ya Ulaya imezipa benki tatu nchini zikiwa ni sehemu ya Euro milioni 540 ilizotangaza kutoa kwenye kongamano la biashara la Tanzania na EU kwa ajili ya kusaidia uwekezaji katika sekta binafsi nchini.

Euro milioni 170 ya mikopo hiyo zitatumika kufadhili uwekezaji katika makampuni yanayoongozwa na wanawake huku Euro milioni 100 zikiwa ni kwa ajili ya uwekezaji katika makampuni yanayojishughulisha na uchumi wa bluu.

Chacha alisema mkopo wa EIB kwao utawawezesha wafanyabiashara kote nchini kukua na kuisaidia nchi kuondokana na vikwazo vya muda mrefu vya uwekezaji.

Naye Makamu wa Rais wa EIB, Bw Thomas Östrost, alisema wamefarijika kurudi tena Tanzania baada ya miaka saba kuyasaidia makampuni nchini kupanua shughuli zao na kutengezea ajira mpya.