Faida Baada ya Kodi ya TZS Bilioni 398, ikiwa in ukuaji wa asilimia 22% mwaka hadi mwaka
*Jumla ya mali zote zimefikia TZS Trilioni 11.5, ikiwa ni ukuaji wa asilimia 22 mwaka hadi mwaka
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Benki ya NMB imetangaza kupatamatokeo imara ya kifedha katika kipindi kilichoishia Septemba 30 mwaka 2023, ambapo faida kabla ya kodi ya Benki imefikia TZS Bilioni 569 ikiwa ni ongezeko la asilimia 23 ikilinganishwa na TZS Bilioni 464 za kipindi kama hicho mwaka jana. Faida baada ya kodi ya Benki hii kiongozi nchini imeongezeka kwa asilimia 22 na kufikia TZS Bilioni 398 ukilinganisha na TZS bilioni 324 zilizopatikana kipindi kilichoishia Septemba 2022.
Ufanisi huu mkubwa unaashiria mwendelezo wa utekelezaji makini wa Mkakati wa Benki na nidhamu kubwa ya utekelezaji wa Mkakati huo, ambapo matokeo yake ni ukuaji wa biashara, nidhamu yaudhibiti wa gharama za uendeshaji na usimamizi mzuri wa ukopeshaji. Ukuaji huu mkubwa wa biashara pia, ni matokeo ya utulivu na mazingira wezeshi ya kibiashara na kiutendaji nchini.
Benki imeendeleza ufanisi wa mapato ambapo mapato halisi ya riba yameongezeka kwa asilimia 20 hadi kufikia Bilioni 692, hasa kutokana na kuongezeka kwa mikopo kwa wateja binafsi na wale wakubwa.
Mapato yasiyotokana na riba nayo yameongezeka hadi kufikia TZS bilioni 334 ikilinganishwa na TZS bilioni 297 za mwaka 2022 ambalo ni ongezeko la asilimia 12. Ongezeko hili linatokana na wateja kutumia zaidi njia mbadala za huduma ambako kunaakisi matokeo chanya ya kasi ya uwekezaji katika masuluhisho ya kidijitali na bunifu ya kifedha.
Mizania ya Benki iliendeleza kasi ya ukuaji na kuvuka kiasi cha TZS trilioni 11.5 kufikia mwisho wa robo ya tatu ya mwaka 2023. Ukuaji huu ulitokana na kuongezeka kwa mikopo na uwekezaji katika dhamana za Serikali.
Mikopo halisi ilikuwa kwa asilimia 25 na kufikia TZS trilioni 7 mwishoni mwa robo hii ya mwaka, huku amana za wateja zikiongezeka kwa asilimia 15 hadi kufikia TZS trilioni 8.2.
Benki ya NMB inaendelea kuonyesha ufanisi mkubwa katika uwiano wa gharama za uendeshaji na mapato, ambapo uwiano huu ulifikia asilimia 38 mwezi Septemba 2023 ukilinganisha na asilimia 41 kwa kipindi kilichoishia Septemba 2022. Haya ni matokeo ya mipango madhubuti na nidhamu katika gharama za uendeshaji na kuongez kasi ya ukuaji wa mapato. Uwiano wa mikopo chechefu nao umeshuka hadi kufikia asilimia 3.5 ambayo ni ndani ya wigo wa kikanuni wa asilimia 5 uliowekwa na Benki Kuu.
Akizungumzia ufanisi huu na matokeo mazuri na makubwa kiutendaji, Afisa Mtendaji Mkuu, Bi Ruth Zaipuna alisema:“Tumefurahishwa na matokeo mazuri tunayoendelea kuyapata mwaka hadi mwaka. Matokeo haya imara ya kifedha yanaashiria imani kubwa waliyonayo wadau na wateja wetu na yanathibitisha dhamira yetu ya kuwa kichocheo cha maendeleo ya kijamiii na kiuchumi nchini.
“Tunawashukuru wateja wetu, Serikali, wanahisa, wadau wetu na wafanyakazi wote kwa kuendelea kutuunga mkono. Tunapoelekea mwisho wa mwaka, tunaamini ushirikiano wao utatuwezesha kuumaliza mwaka vizuri na tunayo matumaini na safari iliyo mbele yetu huku tukidhamiria kuendelea kuzisaidia jamii tunazozihudumia.
“Benki ya NMB inaendelea kuwa imara, thabiti na yenye mtaji na ukwasi wa kutosha. Katika kusonga mbele, tutaendeleza ukuaji wa mapato, kuhakikisha ufanisi wa kudhibiti gharama na kuboresha mizania yetu ili kuwapa faida wanahisa wetu na kuinufaisha jamii yetu.
“Kwa aina ya uwekezaji tunaoendelea kuufanya kwa wafanyakazi wetu, miundombinu ya kiteknolojia, misingi ya utawala bora, na mahusiano na wadau wetu, tuna matumaini ya kuendeleza ukuaji endelevu wa Benki hii, kwa vizazi vijavyo.”
Aidha, Benki imekamilisha robo ya tatu ya mwaka 2023 ikiwa taasisi kubwa iliyoorodheshwa katika masoko ya hisa ya ukanda wa Afrika Mashariki baada ya kufikisha mtaji wa soko (la hisa) wa TZS trilioni 2.3. Katika robo hii ya mwaka, NMB ilikua kwa kiasi kikubwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam. Thamani ya Benki iliongezka kwa asilimia 32.2 na kufanya hisa ya NMB kuongoza katika kipindi hicho.