Benki ya NMB imeendelea kuboresha rekodi yake ya kutengeneza faida baada ya mwaka jana kuongeza kwa kiasi kikubwa pato hilo na kuweza kutenga TZS bilioni 6.2 kwa ajili ya uwekezaji katika miradi yenye tija kijamii.
Kiasi hicho kikubwa kuwahi kutumika na taasisi yoyote ya kifedha hapa nchini kusaidia miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR), ni matokeo ya NMB kupata faida ya kihistoria ya TZS bilioni 429 baada ya makato ya kodi kwa mwaka 2022.
Akitangaza matokeo ya fedha ya NMB kwa mwaka 2022 leo jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi Ruth Zaipuna, alisema faida hiyo ilitokana na ufanisi wa mapato jumla yaliyovuka TZS trilioni 1 na kufikia TZS trilioni 1.2.
“Kutokana na mafanikio haya, sanjari na nafasi ya benki katika uchumi na jamii ya Kitanzania, Benki ya NMB inaendelea kuwa benki kiongozi katika maswala muhimu yanayoigusa jamii,” Bi Zaipuna alibainisha.
“Kwa muktadha huu, Benki ya NMB imetenga jumla ya kiasi cha TZS bilioni 6.2 ili kusaidia miradi mbalimbali ya kijamii. Kiasi hiki cha kihistoria ni ongezeko la zaidi ya asilimia 114 ukilinganisha na kiasi cha TZS bilioni 2.9 kilichotengwa na kutumika kwa mwaka 2022,” aliongeza.
Aidha, alisema fedha hizo ni kwa ajili ya kuleta matokeo makubwa na chanya kwenye maeneo ya afya, elimu, mazingira na mabadiliko ya tabia nchi kwa kushirikiana na wadau muhimu pamoja na serikali kupitia wizara husika.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NMB, Dkt Edwin Mhede, alisema mara hii bajeti ya CSR imeongezewa ziada ya TZS bilioni 2 kwa ajili ya mazigira na maswala ya tabia nchi kwani maeneo hayo ni nyeti sana kwa NMB.
Tofauti na mwaka huu, sera ya NMB ni kutenga asilimia moja ya faida baada ya kodi kwa ajili ya kuwekeza kwenye shughuli za kijamii na kurudisha fadhila kwa wananchi wanaochangia mafanikio yake.
“Utendaji huu muhimu kifedha na kujitolea kwa kiasi kikubwa sana kuendeleza ustawi wa jamii, kunadhihirisha jinsi Benki ya NMB inavyozingatia kwa makini ajenda ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Tanzania, pamoja na kuimarisha nafasi yake ya uongozi sokoni,” ilibainisha taarifa kwa vyombo vya habari.
Bi Zaipuna alisema moja ya sababu za mafanikio kiutendaji mwaka 2022 ni mazingira rafiki ya kibiashara yaliyotokana na sera wezeshi za serikali. Alibainisha kuwa mafanikio hayo ni ushahidi wa kasi ya ufanisi mkubwa wa NMB katika kipindi cha miaka minne na umuhimu wa huduma zake bora kimaisha na kiuzalishaji.
Alisema faida ya TZS bilioni 429 baada ya kodi ni ongezeko la asilimia 47 ukilinganisha na ile ya TZS 290 bilioni ya mwaka 2021. Hili lilikuwa ongezeko la zaidi ya TZS bilioni 130 ndani ya mwaka moja na ukuaji mkubwa sana ukilinganisha na faida ya TZS bilioni 98 mwaka 2018.
Mafanikio mengine makubwa yaliyopatikana mwaka jana ni kufanikiwa kuboresha mali za benki kupitia usimamizi mzuri wa ukopeshaji. Tengo kwa ajili ya mikopo chechefu lilipunguzwa kwa asilimia 33 hadi TZS bilioni 76 huku uwiano wa mikopo hiyo wa asilimia 3.3 ukibaki ndani ya kiwango cha kikanuni cha asilimia tano.
Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Bw Juma Kimori, alisema NMB imekuwa ikifanya vizuri kiutendaji tangu mwaka 2018 na hilo linaonekana vizuri kwenye ukuaji wa mizania yake.
Mtaalamu huyo alisema thamani ya mali za benki hiyo ambayo sasa imefikia zaidi ya TZS trilioni 10.2 ilikuwa ni TZS trilion 5.5 mwaka 2018. Nazo amana za wateja, aliongeza, sasa hivi ni TZS trilioni 7.5 kutoka TZS trilioni 4.2 mwaka 2018.
Mikopo iliyotolewa mwaka jana hasa kwa ajili ya makampuni, watu binafsi na uwekezaji katika sekta za kimkakati ikiwemo kilimo pamoja na biashara ndogondogo na za kati ilifikia TZS trilioni 6 ukilinganisha na trilioni 3.2 mwaka 2018.
“Mizania yetu iko imara na mtaji kutoka kwa wana hisa ambao sasa ni TZS trilioni 1.6 una maana kubwa sana kwetu katika kuendeleza ufanisi ambao tumekuwa tunaupata miaka ya hivi karibuni, kuongeza ukopeshaji na kendelea kutengeza faida,” alisisitiza Kimori.