Kazi yaanza rasmi
Baada ya uzinduzi uliofanywa Pugu, wiki moja baadaye NMB ilianza kazi ya kutembelea shule za msingi. Shule ya Msingi Mlimani, Dar es Salaam ilipata bahati hiyo.

Meneja wa Tawi la NMB Mlimani, George Mwita, akiwa na Meneja wa Kanda wa NMB, Salie Mlay, na Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa NMB, Imani Kajula, waliendesha mafunzo na kuwatunukia zawadi kadhaa wanafunzi.

Katika hotuba yake, Mwita alisema NMB ni benki ya kila mtu – walimu, wafanyabiashara na watoto.

Akasema NMB ina akaunti maalumu kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 18 iitwayo NMB Junior Account. Hii ni akaunti iliyowekwa mahususi kuwafundisha watoto jinsi ya kuweka fedha kwa ajili ya matumizi ya baadaye.

Mwita akawaeleza wanafunzi hao; “Kumbuka siku zote kuwa kesho inaanza leo.”

Akasema NMB kupitia sera yake kwa jamii, ipo kwa ajili ya mambo matatu makubwa – elimu, afya na michezo – na kwamba kupitia sera hiyo, imeanzisha NMB Financial Fitness ambayo imelenga kumfanya kila mtoto awe na uelewa wa matumizi sahihi ya fedha.

“Hii inamaanisha kuwa na uelewa wa masuala ya kifedha. Kwa mfano, usikope kama hujui jinsi ya kuweka fedha. Mtu akijua jinsi ya kuweka fedha anajua jinsi ya kuzitumia kwa uangalifu. Ni kama kujenga ghorofa, lazima msingi wake uwe imara. Nasisitiza wote muanze kujijengea misingi imara ili muwe na maisha mazuri.

“Ili kuwasaidia kujua zaidi, tutawapa kila mmoja jarida linaloelezea kwa undani jinsi ya kuwa na uelewa wa matumizi ya fedha. Ni matumaini yangu mtalifurahia, kuelewa na kuwasimulia marafiki, familia na jamii kwa jumla. Kwa kufanya hili, Tanzania itakuwa na watu wenye uelewa wa matumizi ya fedha,” alisema Mwita.

Baada ya hapo wanafunzi kadhaa waliojibu maswali vizuri na wengine waliofanya vizuri kwenye mitihani yao darasani, walipewa zawadi.

Waliojibu maswali vizuri na kupata zawadi za majarida na chenezo ni Swabra Abdulkadir, Francis Luoga, Amina Joseph na Hassan Ali.

Wanafunzi bora waliopewa zawadi ni Salum Ramadhan, Alfred Shauri, Thomas Mwita na Beatrice Missana. Hafla hiyo ilishuhudiwa na Mwalimu Mkuu, Pendo Kujerwa; na Mwalimu Msaidizi Taaluma, Mathias Shayo.

Kabla ya hapo, wanafunzi walipewa nafasi ya kuuliza maswali. Kwa jumla walionyesha shauku kubwa ya kujua shughuli za benki na faida zake. Maswali hayo yalijibiwa na Mlay, Mwita, maofisa wa NMB Tawi la Mlimani na Kajula ambaye alihitimu masomo shuleni hapo mwaka 1987.

Kwa kasi hii iliyoanzwa na NMB, bila shaka itaifanya Tanzania iwe na wananchi wanaojua vema masuala ya kifedha na benki hasa wakati huu ambao ujasiriamali umepewa kipaumbele. Hongera NMB. Mmeonyesha njia kwa hiyo benki na taasisi nyingine hazina budi kuiga mpango huu wa NMB Financial Fitness.