Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Serikali imetoa wito kwa washiriki wa Kongamano la Nishati wakiwemo Mawaziri, Watunga Sera, Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma na Binafsi, Wafanyabiashara na Viongozi mbalimbali wa Makampuni kutoka ndani na Nje ya Tanzania walioshiriki Kongamano la Tano la Nishati Tanzania kwa mwaka 2023 kutumia mazingira rafiki yaliyopo Tanzania ili kuwekeza katika Sekta hiyo ya Nishati.
Akizungumza tarehe 21 Septemba, 2023 wakati wa hafla ya kufunga Kongamano hilo la siku mbili lililofanyika kuanzia Septemba 20 – 21, 2023 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, Mgeni Rasmi, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Othman Masoud Othman amesema Tanzania ni nchi yenye kila sifa ikiwepo Amani na Utulivu wa kisiasa.
“Kwa wale wageni ninawaalika kuja kuwekeza Tanzania kama mnavyojua kwa miongo kadhaa sasa Tanzania tumekuwa kinara wa Amani, Tanzania ni moja kati ya nchi zenye utulivu wa kisiasa Duniani, imekuwa nafasi nzuri kwenu nyote mliopo hapa leo kwa kupata nafasi ya kujadili na kutafuta ufumbuzi sambamba na ubunifu wa nishati katika kuiendeleza Sekta hii maarufu,” alisema Mhe. Othman.
Akiongelea upande wa Zanzibar, Mhe. Othman amesema, kama ambavyo Tanzania Bara, Zanzibar pia imejiwekea Mikakati Maalum ya Uwekezaji, hususan Sera za Uchumi wa Buluu ambao aliutaja kama tegemeo visiwani humo na kwamba nayo inahitaji Wawekezaji na Washirika wa Kimataifa watakaowezesha Mabadiliko ya Kweli katika Sekta za Nishati, Gesi Asilia na Mafuta kupitia Mapinduzi muhimu ya Teknolojia.
“Natumai hatma iliyofikiwa kwenye majadiliano yenu itawekwa kwenye majumuisho na kuwasilishwa Serikalini kwa ajili ya rejea na maboresho katika Sekta ya Nishati, Nawahakikishai kwamba tutayapitia mapendekezo yote na tutayatumia kuboresha mifumo na taratibu zetu,” alisema Mhe. Othman.
Kongamano la Nishati Tanzania kwa mwaka 2023 limejumuisha Wajumbe kutoka takriban Nchi 93 Duniani ambao pamoja na mambo mengine wamejadili na kuweka mapendekezo, juu ya Usambazaji wa Gesi Asilia (LNG); Bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP); Ubunifu wa Nishati Endelevu; Mbinu Mbadala katika Uzalishaji wa Nishati; na Namna bora ya Ufadhili wa Miradi Mikubwa ikiwemo ya Nishati, ndani na nje ya Bara la Afrika.