Aprili 22, mwaka huu, katika safu hii nilihoji waliko “Friends of Nyerere”.

Nilifikia hatua ya kuhoji baada ya kasi ya matusi dhidi yake kuongezeka. Matusi hayo kama ilivyotarajiwa, yakaunganishwa hadi kwa Mwasisi wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume.

Waliosikiliza hotuba ya Mjumbe wa Bunge la Katiba, Tundu Lissu, wanajua kinachosemwa. Lakini wapo waliokomaa wakitaka matusi hayo tuyarejee ili wayapime kubaini kama kweli yanastahili kuitwa matusi au ni ukosoaji tu wa kawaida dhidi ya Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume.

Mwasisi wa Chadema, Mzee Edwin Mtei, ni miongoni mwa watu mashuhuri waliosikitishwa na kauli mbaya za Lissu. Kwa unyenyekevu, Mzee Mtei akavunja ukimya na kujitokeza kwenye vyombo vya habari na katika mitandao ya kijamii kumkosoa Lissu.

Kwa heshima, naomba nirejee — neno kwa neno — kutoka kwenye maandishi ya Mzee Mtei. Alisema: “Nilimsikiliza Mheshimiwa Tundu Lissu na nasikitika kwamba sikubaliani naye jinsi alivyoeleza shutuma juu na dhidi ya Mwalimu Julius Nyerere, Baba na Mwasisi wa Taifa letu.

“Inajulikana na umma wa Watanzania, kwamba mimi binafsi, kama Waziri wa Fedha, nilitofautiana na Mwalimu, nikajiuzulu uwaziri Desemba1979, nikimwomba ateuwe Mtanzania mwingine atakayeshauri mambo ya uchumi na fedha. Lakini tuliendelea kuwasiliana kwa maelewano bila chuki, na hata aliniteua niwe Mwakilishi wa Tanzania na Afrika inayoongea Kiingereza katika IMF (Shirika la Fedha Duniani) chini ya miaka mitatu baadaye Novemba 1972.

“Nimekuwa na mawasiliano na maelewano mazuri sana na Mwalimu hata baada ya kuasisi Chadema Julai 1992 na tulipokamilisha Katiba na Sera za Chadema, nilimtembelea nyumbani kwake Butiama nikampa azisome ajionee jinsi tulivyonuia kuwahudumia wananchi wetu. Hata siku moja siwezi kumtusi Mwasisi wa Taifa letu. Iwe ni mwiko pia kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo kumtusi Baba wa Taifa.

“Ningewashauri uongozi wa Chadema na hasa vijana wa M4C (Vuguvugu la Mabadiliko) tuendelee na uhamasishaji: kwa umakini, tukiwa na huruma kwa wanyonge maskini wa kutupwa, tukijiandaa kwa umakini na kiutaalamu sera na mikakati ya kuwakomboa toka katika umaskini wa kutupwa kwa kutumia nguvu ya umma (Peoples Power) tukitumia mikakati sahihi: kwani Hakuna Kulala Mpaka Kieleweke:

“Mikakati na sera sahihi ikiwa ni kutumia misingi ya uchumi na miundombinu tulionayo licha ya uhalisia dhoofu tuliorithi; tukiwaenzi walioijenga na kuturidhisha kwa unyofu wao.

“Roho ya Julius Nyerere ilale Mahala Pema Peponi. Amen!

With all due respect to Hon. Tindu Lissu, this smacks BAD TASTE”

Ndugu zangu, kabla ya mwezi mmoja kumalizika, tayari “Friends of Nyerere” na “Friends of Karume” wameanza kujitokeza. Hii ni faraja kwetu tunaowaheshimu wazee hao.

Kujitokeza kwao kumemfanya mjane wa Mwalimu, Mama Maria Nyerere, kwa namna isiyo ya kawaida kabisa kwake, ajitokeze kufanya mambo makubwa mawili. Mosi, ni kuungana na vijana walioamua kupita huku na kule nchini kote kulaani matusi na kejeli dhidi ya waasisi wetu. Pili, ni kuyatoa yale ya maoni, ikiwamo ndoto yenye maelekezo kutoka kwa Mwalimu, akituhimiza Watanzania tusali sana kwa sababu mwelekeo wa Taifa letu si mzuri.

Namshukuru na kumpongeza Mama Maria, hata kama kutajitokeza wasiomcha Mungu wanaoweza kuuchukulia kwa wepesi ujumbe huu.

Mila na desturi za Kiafirika zinatufundisha kuwaheshimu waliotuzidi, na pia tuliowazidi umri. Kumkosoa mkubwa au mdogo si jambo baya. Kinachogomba ni namna au lugha inayotumika.

Kwenye mitando ya kijamii Mwalimu Nyerere anatukanwa na kubezwa. Wanaofanya hivi, ama hawaijui vema historia yake na ya nchi yetu; au wanafanya hivyo kwa husda tu za kiitikadi au kiimani. Lakini wengine nadhani ni kwa sababu ya ufinyu tu wa fikra.

Nimepata kuandika mara kadhaa kuwa kuna mkakati maalum katika nchi hii wa kujaribu kulifuta jina la Mwalimu Nyerere na utumishi wake uliotukuka. Wakati sisi tukikaza msuli kumfuta Mwalimu, mataifa mengine ndiyo kwanza yanatumia busara, maandiko na staili ya maisha ya Mwalimu.

Wapo watu wa dini fulani wanaosema Mwalimu aliwatesa kwa kuhakikisha anajenga mfumo wa uongozi unaolinda na kubeba watu wa imani yake. Huko si kumtendea haki Mwalimu kwa sababu ni yeye huyo huyo aliyehakikisha Serikali huru ya Tanzania inataifisha shule zote na kuzifanya kuwa za umma.

Hatua hiyo iliwasaidia na inaendelea kuyasaidia baadhi ya makundi ambayo kwayo elimu dunia haikuwa lolote wala chochote. Tunaweza kusema kwa kujiamini kabisa kuwa uamuzi huo wa Mwalimu ulisaidia kulifanya Taifa letu kuwa Taifa la watu wamoja wasiopishana sana. Lakini matokeo ya uungwana huo leo hii ni matusi na dharau kwake na kwa waasisi wenzake.

Katika Taifa letu kulikuwa na makabila yaliyokuwa yamepiga hatua kubwa kielimu na kimaendeleo. Kuna makabila yaliyokuwa nyuma kweli kweli. Alihakikisha anajenga misingi ya usawa katika upatikanaji elimu na kwenye kugawana rasilimali. Ni wakati wa Mwalimu ambao mtoto wa rais au mtoto wa waziri waliweza kusoma darasa moja na watoto wa wakulima, wafugaji na makabwela wengine!

Hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Kilindi aliwachukua watoto wake wakasome katika sekondari ya kata. Hatua hiyo ikawa gumzo ikionekana kuwa ni jambo la ajabu kweli kweli! Wapo waliohoji, iweje mtoto wa DC asome katika sekondari ya kata? Kwao, mtoto au watoto wa DC walipaswa kusoma academy.

Mwalimu ambaye ni mtoto wa chifu, hakutaka kuona kundi la watoto wa machifu, wa viongozi au wa matajiri wakisoma katika shule zao maalum, huku watoto wengine wa makabwela wakikosa haki hiyo, au kama waliipata, basi katika maeneo yao maalum, tena yaliyo duni.  Hili nalo wapinga Nyerere na Karume hawalioni!

Vijiji vya Ujamaa pamoja na upungufu kwenye utekelezaji Operesheni Vijiji, bado malengo na maudhui ya kuwa na aina hiyo ya maisha yamekuwa na faida kubwa kwa Taifa. Umoja huu tunaoushudia sasa — hata kama unaelekea ukingoni — ni matokeo ya sera na uamuzi wa aina hiyo. Huduma za afya na elimu katika nchi yetu, hata kama si nzuri, huwezi kuzilinganisha na majirani zetu. Katika jamhuri ya vipofu, sisi ni wenye chongo.

Umoja wa kitaifa kupitia vyombo kama Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), lugha ya Kiswahili, shule za sekondari za kitaifa na haki ya Mtanzania kwenda kuishi popote anakotaka alimradi asivunje sheria; ni baadhi ya mambo yaliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere na wenzake. Faida zake tunaziona leo. Kama leo kila kabila lingebaki mahali pake pa asili, sijui ndugu zetu wa Kaskazini wangekuwa na hali gani maana ardhi yao ni finyu mno!

Mara kadhaa Mwalimu aliwashangaa wale wanaoacha mazuri yaliyofanywa na awamu yake, na kukumbatia mabaya. Kwa kauli yake mwenyewe, anakiri udhaifu katika mambo kadhaa wakati wa uongozi wake. Kwa mfano, moja ya mambo aliyokiri hadharani kuwa alifanya makosa ni utaifishaji mashamba makubwa kama ya katani! Ameondoka madarakani akijuta kufanya makosa hayo. Yeye mwenyewe akakiri kwa kusema makosa kadhaa yamefanywa kwa sababu yeye na wenzake hawakuwa malaika.

Waasisi hawa hawa ndiyo waliotusaidia kuweka misingi ya maendeleo tuliyonayo leo. Ukifika Zanzibar, ukatazama majengo yale ya Michenzani na kwingineko, au ukafika Pemba na kuona ghorofa, utatambua kabisa kuwa kazi hiyo ilifanywa na watu waliolipenda Taifa lao, na ambao kwa kweli hawastahili kubezwa.

Ukitazama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ukatembelea miradi ya umwagiliaji kama ile ya Mwanzugi (Igunga), au ukazuru migodi ya uzalishaji umeme kama Kidatu, utaona kabisa nchi hii ilikuwa na miamba ya uongozi inayostahili kuenziwa!

Wazee hawa, pamoja na wenzao kama Mzee Rashidi Kawawa, wamefariki dunia wakiwa hawana ukwasi wowote wa fedha au majengo — zaidi ya ukwasi wa heshima barani Afrika na duniani kote. Nilimfahamu kidogo Mwalimu Nyerere, lakini sikuwahi kusikia akiwa na akaunti katika benki yoyote ya ndani au ya nje ya nchi. Wala sikupata kusikia kafukia noti au dhahabu katika pango.

Ni Mwalimu huyu huyu ambaye wakati tukisoma, tukiishiwa viatu, aliweza kutoa jozi yake na kutuwezesha kwenda shule. Ni huyu huyu ambaye tulipolalamika hatuna usafiri, alitusaidia baiskeli ili tuweze kwenda na kutoka shuleni. Je, hakuwa na uwezo wa kuifanyia familia na jamaa yake shopping Ulaya, Marekani au kwingineko kwenye vitu vya thamani?

Je, alishindwa nini kuchukua magari ya umma ili yaihudumie familia yake? Chombo gani kilichokuwa na nguvu za kumzuia kujimilikisha migodi ya tanzanite, dhahabu na almasi? Kwanini hakufanya hayo? Hakufanya hayo kwa sababu alitaka yeye na waliomzunguka waishi kulingana na yale aliyoyahubiri kwa wananchi na walimwengu wengine. Kama asingeishi kwa namna hiyo, aliowaongoza wasingemheshimu.

Mtu huyu huyu ambaye ameiaga dunia bila hata kuiachia familia yake kitalu cha uwindaji wa kitalii, anatukanwa na kuambiwa aliishi “kisanii” au “kiujanja-ujanja!”

Heshima ya Mwalimu ipo kwenye utu wake. Heshima inayojengwa juu ya utu haiwezi kufutika. Ndiyo maana katika miji mingi duniani kuna mitaa, vyuo na vitu mbalimbali vilivyopewa jina la Mwalimu Nyerere kama ishara ya kutambua mchango wake kwa walimwengu.

Hii ni heshima kubwa ambayo kina Sani Abacha au Mobutu Sese Seko hawawezi kuipata aslani! Wao heshima zao walizijenga juu ya fedha na mali, na uhai ulipowatoka; fedha nazo zikatoweka —  heshima nayo ikayeyuka kama theluji iliyotiwa moto!

Kama nilivyodokeza kwenye makala ya Aprili 22, pengine tunapaswa kukuna vichwa vyetu ili tupate jawabu sahihi la sababu au vichocheo vya matusi dhidi ya Mwalimu.

Wanaotukana wanajifunza kutoka kwa hawa waliopaswa kuwa mstari wa mbele kuwaenzi wazee hao. Kama wenye chao hawakienzi, tutarajie nini kutoka kwa wasio chao? Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ni taasisi kubwa na yenye nguvu, haijafanya kubwa la maana linalolingana na heshima ya waasisi hao. Hakuna alama wala maandiko ya dhati yanayoweza kukisaidia hiki kizazi cha facebook kuwajua majemedari hawa. Sikushangaa siku moja kwenye mtandao wa Jamiiforums nilipokutana na swali hili, “Mwalimu Nyerere alikuwa na elimu ya kiwango gani?”

Kwa haraka haraka unaweza kudhani aliyeuliza swali hili anafanya mzaha, lakini pengine huu si mzaha. Inawezekana huyu mtoto alizaliwa mwaka 1998 au mwaka 1999 kwa hiyo kwake Mwalimu ni “mzee” kama “wazee” wengine wanaopigwa viberiti kule Shinyanga kwa sababu ya kuwa na macho mekundu!

Hakuna alama ya kweli wala mahali ambako watoto wanaweza kuingia na kumjua huyu mtu pamoja na wenzake — akiwamo Mzee Karume. Ukifika Afrika Kusini utajikuta kwa kila namna unalazimika kumjua Mzee Nelson Mandela. Vivyo hivyo, ukienda Cuba hutapata shida kutambua kuwa Che Guevara (ingawa hakuwa Mcuba) na Jose Marti, ni majina yaliyo juu pengine kuliko hata Fidel Castro mwenyewe!

Hapa kwetu ukisikia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, basi ujue huo ni uchochoro wa dawa za kulevya na utoroshaji rasilimali za nchi. Ukisikia “Nyerere Road”, ujue hiyo ndiyo barabara inayosifika kwa ajali na uporaji unaofanywa na majambazi mchana kweupe! Ukisikia jina la shule au chuo kinachohusishwa na Nyerere, hapo ujue ndiko kwenye mtambo unaotoa wanafunzi waliofeli mitihani! Kunafanyika mambo mabaya alimradi jina la Nyerere liwe chafu na lisilofaa!

Hawa hawa wanasiasa ndiyo wanaohubiri usawa huku wakiwa hawataki kusikia jema kutoka ndani ya Azimio la Arusha. Wamefuta miiko yote ya uongozi. Sasa wanachofanya ni kujitwalia kila kilicho mbele yao.

Unaposikia kiongozi akirubuniwa na Wakenya ili afungue mpaka wa Bologonja, unajiuliza, hii ni akili ya aina gani? Wazee waliofunga mpaka huo kwa miaka karibu 40 iliyopita walikuwa wajinga? Je, maslahi ya nchi ya kiuchumi nayo yanapitwa na wakati? Viongozi wa aina hii nao utawakuta wakiimba wimbo uliochusha wa “Kumuenzi Baba wa Taifa”

Utawasikia wakisema awamu hii ndiyo iliyofanya mengi na makubwa kuliko awamu zote! Unabaki ukishangaa, hivi kweli kuijenga nchi na kuwafanya Watanzania wa makabila karibu 130 wawe wamoja ni kazi ndogo?

Niishie hapa kwa kuwaomba “Friends of Nyerere” waendelee kusimama kuilinda na kuitetea heshima ya Mwalimu Nyerere na Mzee Karume dhidi ya wachafuzi waliodhamiria kuyafuta majina haya mema.

Mtu anayeheshimiwa na kupendwa na masikini, matajiri, wasomi na watu wa hali zote duniani kote hawezi kufutwa jina lake kirahisi. Tuwaheshimu waasisi wetu. Asante sana Bibi Maria. Tunasubiri kumsikia Bibi Fatma Karume.