Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Serikali kupitia Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT)ipo mbioni kuanzisha utoaji wa mafunzo ya Urubani ambapo Chuo kimekamilisha matakwa ya kupata ithibati kutoka TCAA na hivyo mafunzo haya yanatarajiwa kuanza mwezi Mei 2025.

Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Dkt. Prosper Mgaya, ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa chuo hicho katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 20, 2025,Jijini Dodoma.

Ameeleza kuwa kuanzishwa kwa mafunzo haya nchini kwenye Chuo cha NIT kutapunguza gharama ya mafunzo kwa takribani asilimia 50 – 60 ambazo watanzania wengi wanatumia kupata mafunzo hayo nje ya nchi.

Amesema Katika kukiwezesha Chuo hicho kuanza mafunzo hayo ya Urubani Serikali mpaka sasa imetoa jumla ya takribani TZS 6 Bilioni.

“Ifahamike kuwa kama nchi tumekuwa tukitegemea kwa kiasi kikubwa kupelekea watanzania kupata mafunzo ya urubani nje ya nchi,Serikali na watanzania kwa ujumla tumekuwa tukitumia fedha nyingi sana za kigeni kusomesha marubani nje ya nchi, ” Amesema.

Ameeleza kuwa kuanza kwa mafunzo haya hapa nchini kutaokoa fedha za kigeni ambazo zimekuwa zikitumika na kwamba mafunzo hayo kutaongeza idadi ya marubani wazawa hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa utegemezi kwa marubani wa kigeni ambao gharama yake ni kubwa.

“Mafunzo ya urubani yanahitaji kuwa na wakufunzi na vifaa vya kufundishia vinavyokidhi vigezo vya kimataifa Katika kuhakikisha Chuo kinaanza mafunzo ya Urubani Serikali imegharamia mafunzo ya wakufunzi watano ambao wamepata mafunzo haya nchini Afrika ya Kusini kwa Gharama ya TZS Bilioni 1.5 ikiwa ni wastani wa TZS Milioni 300 kwa kila mkufunzi,” Amesema.

Kupitia mradi huo, NIT itapokea Dola za Kimarekani Millioni Ishirini na Moja Laki Mbili Hamsini Elfu (USD 21,250,000) sawa na shillingi za Kitanzania Billioni Arobaini na Tisa (TZS 49 Billioni) kwa ajili ya kuanzisha Kituo cha Umahiri cha Mafunzo ya Taaluma za Usafiri wa Anga na Operesheni za Usafirishaji (Center of Excellence in Aviation and Transport Operations – CoEATO).

Amesema kupitia Mradi huu Serikali imekiwezesha Chuo kujenga majengo Matano katika Kampasi ya Mabibo -Dar es salaam ambao ujenzi wake kwa ujumla umefikia asilimia 97.

Ameeleza majengo matatu ya Kituo cha Umahiri katika Taaluma ya Anga na Operesheni za Usafirishaji yatakuwa na madarasa, maabara, karakana na ofisi za watumishi. Majengo mawili ni Mabweni ya wanafunzi yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 1,504.

“Ujenzi huu unatakamilika ifikapo mwezi June 2025. Gharama ya ujenzi wa majengo haya ni TZS 24.9 Bilioni. Aidha, mradi huu umefadhili ujenzi wa jengo la mafunzo ya urubani katika eneo la KIA ambalo Serikali imetoa,” Amesema.

Aidha amesema Serikali imenunua ndege mbili za mafunzo aina ya Cesna 172 zenye injini moja ambazo tayari zipo nchini kwaajili ya kuanza mafunzo hayo.

Ndege hizo zina thamani ya TZS 2.9 Bilioni Serikali ipo katika taratibu za ununuzi wa ndege nyingine tatu (3) ikiwa ndege moja ya injini mbili (2) ambayo itawasili mwezi Oktoba 2025 ambayo ina thamani ya TZS 5.9 Bilioni.