Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Chuo cha Taifa Usafirishaji (NIT), kimetoa wito kwa vijana waliohitimu kidato cha nne kuchangamkia fursa ya kuomba kujiunga kozi za kimkakati za Chuo ambazo katika mwaka wa masomo wa 2024/2025 zimepata upendeleo wa mkopo kuanzia ngazi ya diploma lengo likiwa ni kupata wataalam wengi watakaojenga na kusimamia miradi ya kimkakati inayotekelezwa kwa sasa na serikali ya awamu ya sita.

Kozi hizo ni za mafundi na wahandisi wa kutengeneza ndege,wataalam wa kujenga na kukarabati meli,wataalam wa mafuta na gesi na wataalam wa kusimamia bandari.

Akizungumza jijini hapa katika banda la Chuo hicho kwenye maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF), Afisa Uhusiano wa NIT, Juma Manday ameeleza kuwa kozi hizo zimepewa kipaumbele na serikali ya awamu ya sita kwa kuwa ni muhimu kwa ajili ya miradi ya kimkakati.

Ameongeza kuwa vijana wenye sifa stahiki watakaoomba kusoma kozi hizo watapata mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuanzia ngazi ya diploma.

“Tunaishukuru serikali yetu ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fursa hii ili kuwezesha kupata wataalam wazawa watakaofanya kazi katika miradi ya kimkakati inayotekelezwa hapa nchini katika sekta ya Uchukuzi.”amesema Manday.

Manday amefafanua kuwa ipo miradi mikubwa kama mradi wa kufufua Shirika la Ndege la Air Tanzania,kuna mradi wa kujenga viwanja vya ndege na kuvipanua,haya yote yanahitaji wataalam ambao sasa watatoka katika Chuo chetu,” amesema.

Afisa huyo ameeleza kuwa upatikanaji wa wataalam hawa hapa nchini utasaidia kuokoa fedha nyingi ambazo hutumika kuchukua wataalam kutoka nje ya nchi.

Please follow and like us:
Pin Share