Tanzania ni miongoni mwa nchi duniani zenye utaratibu wa kufanya uchaguzi kila baada ya kipindi cha miaka mitano ya buongozi. Kuna na demokrasia iliyozoeleka. Ni ya kupokezana vijiti.

Kutokana na utaratibu huo uliowekwa na waasisi wa taifa hili, wananchi ambao ni wapigakura tumezoea kuwaona wenzetu wanaoomba ridhaa ya kutuongoza wakifika kwetu na kutueleza dhamira zao ikiwa ni pamoja na matarajio katika kulisogeza mbele gurudumu la maendeleo ya taifa.

Miaka kadhaa iliyopita tulishuhudia jinsi wagombea walivyokuwa wakijinadi huku wakirushiana shutuma za hapa na pale bila kuumizana wala kupaniana.

Tanzania ina historia tuliyojiwekea, historia ya kuwa taifa lenye upendo, amani na utulivu katika vipindi vyote.

Watanzania wenzangu sasa tunaanza kufuta historia hiyo taratibu kupitia kampeni zinazoendelea nchini huku tukianza mambo mapya yasiyo na tija kwa taifa letu.

Kampeni zinazoendelea nchini zimeanza kuonyesha dalili ya kutugawa Watanzania na kupandikiza chuki ambayo tusipokuwa makini tutajikuta tumebaki vipande vipande kutokana na itikadi zetu.

Wengi wetu tumeanza kuyashuhudia haya kupitia katika mitandao ya kijamiin kwa jamii zinazotuzunguka.

Tunashuhudia namna ambavyo tumeanza kidogokidogo kupandikiza mbegu ya chuki miongoni mwetu ilihali tukitambua wazi kuwa sisi ni ndugu.

Tunaanza kuvunja misingi yetu ya umoja na amani tuliyojiwekea kutokana na mapenzi yetu ya vyama; hakika tunafarakana na kujitenga na wenzetu kutokana na itikadi zetu za vyama, tunaanza kubezana na kutukanana kutokana na kutofautina kiitikadi!

Hii si Tanzania ninayoifahamu.

Tunalo jukumu kubwa la kujiuliza na kutafakari kuhusiana na nchi yetu baada ya uchaguzi. Tutafakari kuhusu maisha yetu baada ya uchaguzi. Zaidi tutafakari kuhusu taifa letu baada ya mwezi Oktoba.

Watanzania ni lazima kufahamu ya kuwa mafanikio ya maisha yetu kamwe hayategemei wagombea urais wanaoshabikiwa katika kampeni hizi, hatima ya maisha yetu haitegemei vyama vya siasa.

Ni vyema kutambua wazi kuwa mimi na wewe mafanikio  na maendeleo ya maisha yatu binafsi yapo mikononi mwetu, hivyo tunapofikiria kuchagua viongozi kupitia uchaguzi huu tukumbuke ya kuwa sisi wenyewe ndio viongozi wa maisha yetu binafsi sio Ukawa wala CCM.

Ni vyema kila mmoja wetu akatambua wazi kuwa hatima ya amani ya nchi yetu ipo mikononi mwake. Amani yetu haiwezi kuimarika bila kuwa na upendo wa kweli.

Bila upendo wa kweli ni vigumu kuwa na amani. Hivyo basi ni vyema tukajitafakari katika kipindi hiki na kujipima ni mabadiliko ya aina gani tunayataka katika maisha yetu, na yanaletwa na nani hasa?

Mimi ni miongoni mwa wanaohitaji mabadiliko ya mfumo, mabadiliko yenye lengo la kumsaidia Mtanzania na kunufaika na raslimali zake, lakini si muumini wa mabadiliko ya kuhatarisha upendo, umoja na amani tuliyonayo.

Natamani kuiona Tanzania inayoondokana na unyonywaji unaofanywa na kupe wachache walioamua kunyonya kila kizuri tulichobarikiwa. Sitamani katu kuona kupe hao wanakuwa chanzo cha mifarakano ya sisi kwa sisi kutokana na ufukara wetu.

Nachukizwa na chuki tunazopandikizwa kutokana na mapenzi yetu kwao. Wanatupandikiza kuchukiana na kuhasimiana huku tukiapizana viapo visivyo na faida kwa vizazi vyetu na nchi kwa ujumla.

Baada ya uchaguzi huu natamani kuiona Tanzania nchi yangu yenye amani na utulivyo kama ilivyo kabla ya uchaguzi. Tukiishi kwa kusalimiana na kusaidiana sio kuendeleza kile kinachoonekana sasa.

Tanzania ni nchi yetu, hatuna budi kuwapinga wazi wazi wale wote watakaohubiri siasa za chuki na kuja kutufarakanisha kwa maslahi yao wenyewe. Tunalo jukumu la kulinda amani ya nchi yetu.

Amani yetu hii ambayo tumeanza kuichoka wenzetu wanaitafuta na kuililia baada ya kuichezea hivyo kukumbwa na vurugu zinazowagharimu na kuishi maisha ya kuhamahama huku wakiwapoteza wapendwa wao.

Mimi, wewe na yule ni jukumu letu sote kukemea pale panapobidi ili kuweza kufanya uchaguzi wetu kwa amani na utulivu huku tukitumia haki yetu ya kuchagua viongozi tunaoona wana sifa za kuliongoza taifa letu na kutuletea mabadiliko ya kweli. Tanzania nchi yetu, Tanzania taifa letu sote.