Mara baada ya ratiba ya ndani ya CCM kutolewa, kumekuwapo na mfumuko wa wagombea waliojitokeza kuchukua na kurudisha fomu ya kuwania urais.    
Swali la kujiuliza ni je, utitiri huu umechochewa na nini?
Hoja hii ni mtambuka ambayo inagusa maeneo mengi kisiasa, kiuchumi na kijamii. Hata hivyo, nitajaribu kubainisha baadhi ya mambo muhimu ninayohisi yamechangia wagombea wengi kujitokeza hadi kufikia 30 mpaka wakati naandika makala hii.
Kwa kuanzia, ningependa kujielekeza katika maeneo matatu ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.  Nianze na hoja za kisiasa.


Haki ya mtu kushiriki shughuli za umma imewekwa bayana kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Ibara ya 21 (1) inayosisitiza kuhusu kila raia kuwa na haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, ama moja kwa moja au kwa kupitia wawakilishi waliochaguliwa na wananchi kwa hiari yao kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na sheria.
Pia ibara ya 39 (1), imefafanua sifa za mtu kuchaguliwa kuwa rais ambako pamoja na mambo mengine, inasema; awe ni raia wa kuzaliwa wa Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa sheria ya uraia na pia ametimiza umri wa miaka arobaini na mengineyo.


Sababu ya pili kisiasa imechochewa na kupanuka kwa wigo wa demokrasia nchini. Siyo siri kwamba uongozi wa Rais Jakaya Kikwete umejitahidi kuongeza haki na uhuru wa demokrasia nchini.  Kila mtu mwenye sifa ya kuwania nafasi yoyote ya kisiasa (ruksa) kufanya hivyo, ilimradi atimize masharti.
Sababu ya tatu kisiasa imetokana na kuporomoka kwa mfumo wa chama kama taasisi. Itakumbukwa kwamba enzi za TANU na baadaye CCM kabla ya ujio wa vyama vingi nchini 1992, haikuwa ni jambo rahisi kwa kada yeyote kuchukua fomu ya kugombea urais bila kwanza kupitia tanuri la mchujo wa kimaadili.
Kwa mfumo wa chama enzi za (TANU-CCM) ilikuwa ikiwalazimisha makada wanaotaka kugombea nafasi nyeti kama za urais na ubunge kwanza wapitie mafunzo ya kiitikadi (vyuo vya chama) ili wapikwe. Kipindi hicho ilikuwa ni lazima mgombea wa urais atoke miongoni mwa wajumbe wa Kamati Kuu na siyo nje ya hapo.


Tofauti na ilivyo kipindi hiki, ilimradi wewe ni mwanachama bila kujali unatoka wapi, basi uko huru kuchukua fomu kama vile ni fomu za kuwania uongozi barabarani!  Heshima na hadhi ya chama imeporomoka ndiyo maana utitiri huu umejitokeza.
Sababu ya nne kisiasa inajumuisha kundi la wagombea wanaohusudu ubinafsi na uroho wa madaraka. Wapo wagombea waliojitokeza kutangaza nia, lakini kiukweli hata roho zao zinawasuta kuwa hawawezi kumudu nafasi hiyo.


Hata hivyo, kwa sababu tu ya ubinafsi na uroho wa madaraka wameamua kujipambanua kama ni wagombea safi. Kazi yao kubwa ni kumtegea mwenzao atakayepata, nao pia wajifanye wanamuunga mkono ili aje awakumbuke walau kwenye nafasi ya uwaziri, unaibu waziri au hata uwaziri mkuu.
Sababu ya tano kisiasa; kundi jingine la wasaka urais inatokana na msukumo kutoka kwa mataifa ya nje. Wapo wagombea ambao wameamua kugombea kutokana na msukumo kutoka mataifa ya nje. Mataifa ya nje yanajipanga kumjua kiongozi ajaye Tanzania atakuwa na mwelekeo gani kisera na kidiplomasia. Hivyo, wanatumia mwanya huu kurubuni mgombea watakayemtumia kupitisha sera zao za ukoloni mamboleo.


Sababu za kiutamaduni. Kuna baadhi ya wagombea waliosukumwa na maadili potofu ya kikabila, kikanda na udini. Kundi hili limesheheni wagombea ambao wanaona ufahari rais akitokea kwenye kabila, dini, au kanda wanakotoka. Hawa hawana sera bali ni kutaka kupandikiza utawala  wa kiimla, kichifu n.k, ni kundi hatari kabisa.
Sababu nyingine za kiutamaduni. Kuna kundi ambalo limetumwa kuja kuvuruga wagombea wenye nia nzuri kwa sababu tu za chuki binafsi kutokana na tamaa ya kugombania vyeo. Kundi hili linatumia uzoefu wa kueneza unafiki kwa jamii ili wapate sapoti (huruma) ya kumkandamiza mgombea ambaye anakubalika.
Sababu nyingine za kiutamaduni. Kuna kundi ambalo linajiandaa kugombea ubunge mara baada ya kushindwa kwenye mbio za urais. Hivyo, wanatumia jukwaa la kuwania urais ili wapate umaarufu wa kujipanga upya kuja kuhadaa wapiga kura, eti kutokana na kuwapo kwao kwenye kundi la wazito (wagombea Urais), waje wachaguliwe kiulaini.


Kuna kundi la wagombea ambao wametumwa na intelijensia ili kupitia kwao wapate kuwajua kiundani, baadhi ya wagombea uwezo wao kiuchumi na kiusalama. Kundi hili limesheheni wagombea wanaofuatilia undani wa maisha ya wenzao. Pia wanafuatilia matukio na uhusiano ya wagombea nje na ndani ya nchi na kuwajua washirika wao kibiashara.
Sababu nyingine za kiuchumi. Kuna kundi la wagombea ambao kweli wanaguswa kwa dhati na umaskini unaoongezeka miongoni mwa wananchi. Wagombea wa kundi hili ni wachache. Hawa ni wagombea ambao wanajiuliza kila kukicha kwa nini nchi hii ni maskini? Tufanye nini nchi ili isiwe tegemezi!
Wagombea kutoka kundi hili hawapati usingizi kila uchao. Wanatumia muda wao mwingi  kubuni mikakati itakayowasaidia katika kuhudumia jamii. Mbali ya kutekeleza sera na ilani za chama, lakini pia wana mbinu mbadala zitakazoleta mabadiliko ya kweli nchni. Kundi hili ndiyo wasiotakiwa na baadhi ya viongozi wa chama.


Kundi hili linahofiwa kuwa likipata baraka za wananchi na kushika uongozi (urais), basi pazia la mshikemshike kwa viongozi walioitia nchi hasara kwa kuingia kwenye mikataba ya ovyo litaeleweka.
Kwa msingi huo, wagombea kutoka kundi hili wanatazamwa kwa darubini kali na walioko madarakani. Mwangwi wa uwepo kwao Ikulu itakua noma kwa mafisadi na wala rushwa. Hivyo, kundi hili linapigwa vita kali na walioko madarakani. Kundi hili ndiyo linalojumuisha akina Edward Lowassa.


Hata hivyo, kutokana na ukweli kwamba Serikali ya Rais Kikwete imejitahidi kwa kadiri ya uwezo wake kuweka mambo wazi, hususani demokrasia na utawala wa sheria, ninashawishika kuamini kwamba makundi yote yatapewa jukwaa sawa.
Napenda nitoe ushauri kwa wagombea wote kwamba kabla ya kuamua kuendelea na mchakato huu, ni vema wakajichunguza, wakajipima na wakajishauri kama kweli wanafaa kuvaa viatu vya Kikwete.
Vinginevyo, wasijisumbue kwani Watanzania wa leo siyo wale wa jana. “Sasa kumekucha jogoo anawika Dodoma, hakuna kulala mpaka kieleweke…” Ninawatakia wagombea wote kila la kheri.
 
J. M. Kibasso
Simu; 0713-399004/0767-399004
Email:[email protected]