Andika maono yako
Kuwa na ndoto ni ishara kwamba una tumaini. Kuwa na ndoto ni ishara kwamba unafikiri unaweza kushinda. Kuwa na ndoto kunakufanya uonekane kijana hata kama umri unakwenda. “Kama haujawa na ndoto kuhusu kitu kipya, kitu kikubwa au kitu bora, anza kuitafuta ndoto hiyo,” anasema Dave Ramsey, mjasiriamali na mtaalamu wa mambo ya uongozi.
Kuwa na ndoto tu haitoshi. Baadhi ya watu huwa na ndoto na huishia tu katika kuwa na ndoto, hakuna hatua yoyote wanayoichukua ili kuzifikia ndoto zao. “Sipendi ndoto ndogo, napenda ndoto kubwa, ukiwa na ndoto ndogo huwezi kuifikia ndoto hiyo nakwambia,” ni maneno ya Ruge Mutahaba.
Ili ndoto yoyote ikamilike, inahitaji kuwa na maono. Maono ni ndoto zilizo na maana zaidi. Maono ni uwezo wa kuona. Mtu anapokuwa kipofu tunasema ameacha kuona, hii ni sahihi pia katika maisha yetu. Hellen Keller (Juni 27,1880-Juni 1, 1968), mwandishi maarufu wa karne ya 19, aliyepoteza uwezo wa kuona akiwa na miaka miwili baada ya kuzaliwa anasema, “Mtu wa kumuonea huruma zaidi duniani ni yule mwenye upeo, lakini hana maono.” Wana macho, lakini hawaoni.
Uwezo wa kuona ni ujuzi ambao kila mtu inabidi ajifunze. Mwandishi wa kitabu cha Mithali anasema, “Bila maono watu huangamia.” Neno “angamia” huwa nikilitafakari kwa kina huwa naona linasema, bila maono, utakufa…utateketea, utapotelea mbali.
Bila maono, ndoa yako itakufa, familia yako haitafanya kazi, maisha yako ya kiroho yatakwenda mrama na pesa yako itapotea. Maono hugusa karibia kila sehemu ya maisha yetu.
Hakuna matokeo makubwa bila maono. Kama huna maono yaliyoandikwa chini kwenye “notibuku” na mipango ya namna ya kuyafikia maono hayo ni sawa na kupiga ngoma kwenye maji. Hailii wala kusikika.
Weka utaratibu wa kuandika maono yako. Unajionaje miaka mitano, 10 au 20 ijayo. Habakuki aliambiwa, “Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji.”(Habakuki 2:2).
Maono yaliyowekwa katika maandishi yana maana kubwa sana. “Sanaa ya kuandika ni sanaa ya kugundua kile unachokiamini,” anasema Gustave Flaubert.
Ukiandika ndoto zako ni wazi kuwa utapata hamasa ya kuchukua hatua kuzifikia ndoto hizo. Makampuni unayoyaona yakiendelea kila siku yana dira (maono) inayoyaongoza katika utekelezaji wa kazi zao. Ukiwa na dira nzuri ni rahisi kufika mahali unakotaka kufika.
Kampuni ya Apple pamoja na kuanzia katika gereji iliyokuwapo nyumbani kwa kina Steve Jobs ilikuwa na ndoto ya kuwa kampuni kubwa duniani. Leo hii ukitakiwa kutaja kampuni kubwa zenye kutengeneza bidhaa bora duniani, utapigwa ukisahau kutaja Apple.
Maono ni kama ramani inayokuongoza katika njia unayoipitia. Ili utimize ndoto yako unahitaji ramani inayoitwa maono. “Maono ni sanaa ya kuona kile ambacho hakionekani kwa wengine,” ni maneno ya Jonathan Swift.
China ambayo leo hii ni ya pili duniani kwa uchumi mkubwa kuna wakati ilikuwa chini kabisa ya nchi kama Japan, Uingereza na Ufarasa. Kuna watu walikuwa na maono ya kuipeleka nchi hiyo mahali ilipo leo hii.
Mwaka 1978 China ilikuwa nchi ya 10 kiuchumi duniani. Miaka 20 baadaye, yaani mwaka 1998 ikapanda na kuwa ya tano. Miaka 20 tena baadaye, yaani mwaka 2018 China ni ya pili kiuchumi duniani. Bila maono watu huangamia. Unahitaji maono kuyafikia malengo yako, unahitaji maono kuzifikia ndoto zako.
Dira ya Taifa ya mwaka 2025 inasema kila Mtanzania awe na uwezo wa kumiliki uchumi wa nchi. Je, ni watu wangapi wamedhamiria kumiliki uchumi wa nchi? Inawezekana kuna wengine ndiyo kwanza wanaona na kusikia hiki kitu.
Kama serikali ina dira au maono, je, wewe maono yako ni yapi? Hakuna kitu ambacho huwa kinaniuma kama kumuuliza mtu, “Unajiona wapi miaka 10 ijayo?” Akajibu,
“Najiona mbali”. Huo ni ukosefu wa maono. Unajiona mbali wapi? Mbali ambako hujui ni wapi?
Tafuta maono yako ni yapi na hakikisha umezungukwa na watu wenye maono pia. Ukiwa na kampuni hakikisha timu yako inafahamu dira yako ni ipi ili kampuni ifanye kazi kutokana na dira yako.