Hesabu baraka zako
Ukiwa na ndoto si kila kitu unachokifanya kitaleta matokeo unayotarajia. Ni jambo jema kuwa na matarajio makubwa, lakini ni vema pia kuwa na moyo wa kustahimili.
Moyo wa ustahimilivu ndiyo huwafanya wenye ndoto waendelee kubaki katika mstari ingawa muda mwingine maisha yatawatoa nje ya mstari.
Kuwa mstahimilivu ni kuwa na tabasamu wakati ambao unatakiwa kununa, kuwa na furaha wakati ambao ulitakiwa kuwa na hasira, kutokuwa na wasiwasi wakati ambao ulitakiwa kuogopa.
Kuwa mstahimilivu ni kuwa na furaha wakati unatakiwa kusononeka.
Kuna muda utajaribu kila njia ili ufanikishe ndoto yako, lakini matokeo ni yale yale au ni madogo zaidi ya uliyowahi kuyapata. Huu ni muda unaotakiwa kuhesabu baraka zako na si balaa zako.
Muda mrefu tunashindwa kuona baraka tulizonazo na kuanza kuona balaa tulizonazo. Ukianza kuhesabu balaa zako unaanza kupishana na ndoto yako.
Usiwe mtu wa hasira, kulalamika, kusononeka, kwa sababu tu ndoto yako haijaleta matokeo unayotarajia. Hawakukosea waliosema: “Hasira hasara.” Na wale waliosema: “Hasira ya mkizi, furaha ya mvuvi.”
Unapokuwa na hasira au unasononeka muda wote unazalisha vitu ambavyo hata kabla havikupaswa kutokea kwenye maisha yako.
Tuchukue mfano, umekasirika kwa sababu biashara zako hazikwenda sawa – hasira hizo unaamka nazo na kuzipeleka kwenye biashara yako kunapokucha. Wateja wakifika kwenye biashara yako wanakuta umenuna. Wachina wana msemo: “Kama hauwezi kutabasamu hauruhusiwi kufungua duka.”
Mbali na kununua mteja anakuuliza kitu, bado unamjibu kwa hasira. Kwa kufanya hayo ni kama tayari umemfukuza mteja. Mteja huyo anaweza kukutangaza vibaya kwa mteja mwingine. Tayari unazidi kufukuza wateja zaidi. Wewe ni shahidi wa hili - ni mara ngapi umekwenda kununua bidhaa mahali baada ya kuambiwa na rafiki yako? Ipo wazi, ni mara nyingi.
Ikumbukwe kuwa mteja ni mfalme. Sam Walton (1918-1992) mwanzilishi wa stoo za Wal-Mart anasema: “Mtu wa muhimu zaidi kwenye kampuni ni mteja, anaweza kumfukuza yeyote kuanzia bosi hadi mtu wa chini. Anafanya hivyo kwa kutokuja kwenye biashara yako na kutumia pesa yake kwingineko.”
Badala ya kuwa na hasira, kwanini usijivunie mafanikio uliyowahi kuyapata hapo nyuma? Kumbuka siku ulizopata mauzo ya juu. Kumbuka mafanikio yaliyoletwa na kitu ulichokifanya.
Hata ukiwa na hasira namna gani, usiifanye ikutawale. Itawale kwa kuwa mtu mwenye furaha, wajibu watu kwa upole na ukarimu. “Kujibu kwa upole hutuliza hasira, lakini neno kali huchochea hasira.” (Mithali 15:1)
Kuna hadithi moja ya vijana watatu waliokwenda kutalii jangwani. Wakiwa katika tembea tembea yao na kutazama maajabu ya Mungu jangwani, mmoja wao aligongwa na nyoka mwenye sumu kali mguuni.
Vijana wale wawili walipoona mwenzao akianguka na kupiga yowe kutokana na maumivu aliyopata, wakashikwa hasira na wakaanza kumkimbiza yule nyoka. Baada ya muda walimpata na kumuua. Waliporudi ili kumtazama rafiki yao walikuta tayari sumu ya nyoka imekwishaingia katika mfumo wa damu. Rafiki yao huyo alikatwa mguu.
Vijana hao wawili walikuwa na uchaguzi wa aina mbili; mosi, kumhudumia rafiki yao; pili walikuwa na uchaguzi wa kumuua nyoka. Walichagua wa pili. Uchaguzi wao uliobeba hasira mwishowe unaleta matokeo mabaya zaidi.
Kuna kila haja kwenye maisha yetu kuwa watu tunaohesabu baraka zetu na si balaa zetu. Bila kujali unapitia magumu yapi katika kutimiza ndoto yako, hesabu yale mazuri uliyonayo.
Kila siku unapoamka jenga tabia ya kujitamkia maneno ya hamasa, kaa chini na hesabu vi-mafanikio vidogo vidogo ulivyowahi kuvipata. Usiwe mtu wa kulalamika kila mara. “Silalamiki sina viatu, wenzangu hawana miguu,” aliwahi kuimba Mwana FA.
Mshale hutupwa kwa kuvutwa nyuma. Maisha yanapokurudisha nyuma na changamoto nyingi, kumbuka yanakufanya ulenge mahali sahihi kama mshale unavyotua ulikolengwa. Baki ‘ukifokasi’, endelea kulenga.
Nick Vujicic ni raia wa Australia aliyezaliwa bila mikono wala miguu, anaweza kuogelea, kuendesha boti, ni mwandishi wa vitabu na mhamasishaji mkubwa duniani. Una nini cha kulalamika wewe uliyezaliwa na viungo vyote?
Nick anasema: “Ni uongo kusema wewe si mzuri vya kutosha. Ni uongo kama unafikiri hauna thamani yoyote.” Hesabu baraka zako na si balaa zako.