Weka malengo
Ndoto inahitaji malengo. “Ndoto bila malengo ni ndoto tu, vinginevyo utaishia kupata mambo usiyoyategemea, hivyo kuwa na ndoto na kuwa na malengo,” anashauri Denzel Washington.
“Malengo ni maono na ndoto vikiwa katika nguo za kazi,” anasema Dave Ramsey.
Malengo ndiyo humfanya mtu aweke jitihada ya kutimiza ndoto zake, hivyo kuwa na malengo katika maisha ni jambo la msingi sana. Weka malengo ya maisha, malengo ya miaka, malengo ya mwaka mmoja, malengo ya mwezi, malengo ya wiki na malengo ya kila siku.
“Kuweka malengo ni hatua ya kwanza ya kubadili kisichoonekana na kukifanya kionekane.” (Tony Robbins.)
Hakikisha una kitabu maalumu ambamo unaandika malengo yako. Uandishi wa malengo una maana kubwa mbili; kwanza, si rahisi kuyasahau. Pili, utakuwa na muda wa kuyapitia mara kwa mara na kuona ni yapi yametimia na ni mahali gani unatakiwa kuweka nguvu zaidi ili utimize malengo yako.
Unahitaji kusoma malengo yako kabla haujalala na unapoamka kila siku, hii itakupa dira ya mambo gani unatakiwa kuyafanya. Kama una malengo ya kila siku yaandike kabla haujalala kila siku.
Watu wenye ndoto kubwa huwa na malengo makubwa. Kama malengo yako hayawatishi watu wengine jua kwamba una malengo madogo, lakini pia ndoto yako ni ndogo sana. “Ili uwe mtu ambaye haujawahi kuwa lazima ufanye mambo ambayo haujawahi kufanya,” anasema Les Brown.
“Lengo kwenye mwezi, hata kama ukikosa utatua katika nyota mojawapo.” (Normal Vicent Peale)
Kinachowatofautisha watu waliofanikiwa na wasiofanikiwa ni malengo. Nionyeshe mtu mwenye malengo, nitakuonyesha mtu atakayetengeneza historia. Nionyeshe mtu asiye na malengo nitakuonyesha mtu mwenye maisha yasiyo na mbele wala nyuma.
Malengo yanahitaji nidhamu ya hali ya juu lakini pia yanahitaji kufanyiwa kazi bila kukoma. “Nidhamu ni daraja kati ya malengo na utimizwaji wake.” (Jim Rohn)
Unapoweka malengo: “Anza na mwisho kwenye akili yako,” alisema Steve Harvey. Naye Solon alikuwa na haya ya kusema: “Katika mambo yote unayoyafanya, jali mwisho.” Ukitazama mwisho utaona kitu unachokitaka.
Yusufu ndoto yake ilimuonyesha kuwa atakuwa kiongozi mkubwa, familia yake ilimuona katika maisha yake ya kila siku. Ukiwa na malengo yanayoonyesha mwisho usishangae watu wakakuona kichaa, malengo yamebeba ndoto zako si zao.
Unapoweka malengo hakikisha yamejikita katika maeneo haya saba: malengo ya kikazi, malengo ya kiuchumi, malengo ya kiroho, malengo ya kimwili (kuwa na mwili imara na wenye afya), malengo ya kiakili, malengo ya kifamilia, malengo ya kijamii.
Hizo ni kama spoku kwenye gurudumu la maisha. Unahitaji kufanikiwa katika maeneo yote saba. Kama ukifanikiwa kiuchumi na kiroho bado hali ni tete wewe haujafanikiwa, kinyume chake ni sahihi pia.
Malengo yanayofanya kazi huwa katika makundi manne
Moja, malengo lazima yawe maalumu na yanapimika. Unapoweka malengo usiyaweke ili mradi tu, lazima yalenge kitu maalumu na yapimike. Hauwezi kusema nataka kutengeneza pesa nyingi, bado haujaweka malengo, au useme nataka kupunguza uzito.
Badala yake unaweza kusema, nataka nipungeze kilo 20 za uzito au nataka kutengeneza milioni 20 kila mwaka, au nataka shahada ya chuo katika…
Mbili, malengo lazima yawe na ukomo wa muda. Siku zote kumbuka kuweka mwisho wa kutimiza malengo yako. Malengo ambayo hayana ukomo wa muda hayawezi kukuwezesha kuyavunja katika shughuli ndogo ndogo zitakazokuwezesha kufikia malengo makubwa. Mfano, usiseme: “Nataka kuwa mbunge,” sema “Mwaka 2025 nitagombea nafasi ya ubunge katika jimbo langu.”
Tatu, malengo lazima yawe yako. Ukiwa na malengo ya mtu mwingine hauwezi kuwa na motisha ya kufanya kazi kwa bidii na uvumilivu kama unavyokuwa na malengo yako. “Mama yangu alitaka niwe daktari,” swali ni je, wewe unataka kuwa daktari? Malengo yasiyo yako yatakuweka katika wakati mgumu siku zote.
Watu wote wanaoshinda ni wale wanaostahimili magumu na kupitia vikwazo. Hauwezi kustahimili magumu na kupitia vikwanzo katika jambo lisilo moyoni mwako lazima ukate tamaa.
Siku zote kumbuka kuishi maisha ya ndoto zako na si maisha ya watu wengine.
Nne, malengo lazima yawe katika maandishi. Kama nilivyotangulia kusema malengo yaliyoandikwa yana nguvu kubwa sana. “Malengo yaliyoandikwa ni kifungua kinywa kwa washindi,” anasema Dave Ramsey.