Kupuuza ubunifu ni kuua ndoto
Kila mmoja wetu amezaliwa na ubunifu ndani yake, jambo hili lipo wazi hasa pale tunapowatazama watoto wadogo. Tukiwa watoto tunaweza kufanya mambo mengi na kujaribu vitu vingi. Watoto hutengeneza vitu kwa kutumia vifaa vinavyozunguka mazingira yao.
Atajenga nyumba kwa kutumia miti, au anatumia kijiti kujifunza kuchora. Au anatumia makopo kama vifaa vya jikoni, atatengeneza gari kwa kutumia miti na mbao, au atatengeneza mpira na ataanza kuucheza. Huu ni ubunifu ambao unaanza kujionesha ndani yetu toka tukiwa wadogo.
Ukiwa mtoto unaamini kila kitu kinawezekana na kinaweza kufanyika. Muda ukianza kwenda na ukaanza kukua mambo huanza kubadilika. Jamii zetu zinazotuzunguka zinaanza kuua ubunifu huu tulioubeba.
Utakuta mtoto akiwa amekazana kufanya mambo ya kibunifu anaambiwa aache anapoteza muda akazane na shule ndiyo itamtoa kwenye maisha kumbe maskini shule aliyopaswa kuambiwa akazane nayo ni hiyo iliyobeba ubunifu wake.
Akili zetu sasa huanza kukubali kwamba sisi si watu wanaoweza kufanya mambo makubwa. Kama ni mzazi atamwambia mwanae “soma uwe daktari au injinia”, matokeo yake tunapata watu ambao wanafanya kazi zisizo zao. Hawana furaha na kazi wanazofanya.
Tatizo kubwa linaanzia katika kudharau ubunifu walio nao watoto wetu, siku hizi utasikia watu wakiuliza, “Tunakwama wapi.” Jibu lipo wazi tunaanzia kukwama tunapoanza kupuuza ubunifu ulio ndani ya watu.
Hatuishii hapo tu, hata wale wanaojitahidi kutoka katika maeneo yao ya faraja na kujaribu kuendeleza ubunifu walio nao bado tunawakatisha tamaa. Hizi ndizo jamii zetu za Kiafrika!
Tunao Watanzania wengi ambao wanafanya mambo makubwa ya kiubunifu, lakini bado tunawapuuzia, kupuuzia ubunifu, ni kuua ndoto za watu.
Nimekutana na kuona watu zaidi ya wanne ambao wametengeneza helikopta, lakini je, kuna watu wangapi wamechukua hatua na kuwapa watu wa namna hii fursa ya kukuza ndoto zao? Tunaishia kusema haziwezi kupaa, huko ni kukatishana tamaa na kuua maono na ndoto za watu.
Tunavyoona ndege za wenzetu huwa tunafikiria walianzia wapi? Ni vyema tukawaza pia jambo hili, au tunafikiri ndege zilishuka mawinguni?
Tukiwatazama watu waliotengeneza ndege – Orville na Wilbur Wright (The Wright Brothers) hawa walianza kwa kuwa mafundi baiskeli mwaka 1896 na hatimaye mwaka 1903 wakawa watu wa kwanza kurusha ndege angani.
Wazo la kurusha ndege walianza nalo mwaka 1899 kwa kufikiria namna rubani anavyoweza kurusha ndege na isianguke kama vile mtu anavyoweza kuendesha baiskeli na asianguke. Ukisikia majina ya ndege kama Airbus, Boeing, Bombadier, Textron, Pilatus na nyingine tambua kuwa yalianzia huko.
Najaribu kufikiria kwanini watu wa namna hii wasiweze kupewa vipaumbele na wakafanya kitu kwa manufaa ya taifa. Siku hizi kuna ndege ndogo zinaitwa ‘drones’ . Hizi zinaweza kutumiwa kunyunyiza dawa mashambani na pia kusafirisha damu kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali zilizo mbali. Nchini Rwanda, ‘drones’ zinatumika kufanya kazi hiyo.
Ukitembea katika vyuo vikuu vingi hapa nchini utashangaa. Ukistaajabu ya Musa utaona ya Filauni. Kuna wanafunzi wengi ambao wanabuni vitu vizuri vinavyoweza kutusaidia kutatua matatizo katika jamii zetu. Watu hawa wakihitimu vyuo, kazi zao huwa zinabaki vyuoni muda mwingine zinatumika tu kama mapambo.
Nichukue fursa hii kumpongeza Rais John Magufuli kwa kutokupuuza ubunifu wa John Fute na Jairos Ngairo waliobuni miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia maji, kusukuma maji kwa kutumia pampu zisizotumia umeme na kusaga nafaka kwa kutumia mashine zinazoendeshwa kwa maji ya mto.
Fute amebuni mradi unaozalisha kilowati 28 na Ngairo anazalisha kilowati 15 za umeme. Kongole Rais Magufuli. Ubunifu utatufikisha mbali kama tutaacha kuudharau. William Kamkwamba (31) wa Malawi akiwa na miaka 14 alitengeneza pangaboi (windmill) lililopeleka umeme kijijini kwao (ingawa mwanzo walimuona kama kichaa). Baadaye alitengeneza jingine kubwa zaidi lililosaidia umwagiliaji mashambani. Ameandika kitabu kinachoitwa The Boy Who Harnessed The Wind ambacho mwaka huu kimetumika kuandaa filamu.