Msamaha si kwa ajili yako bali kwa wengine
Unapokosewa kuwa tayari kutoa msamaha kwa anayekukosea, unapokosa omba msamaha pia. Kusamehe ni jambo lililowashinda watu wengi, ukijenga tabia ya kusamehe wanaokukosea utakuwa umejiondoa katika kundi la wengi.
Usiposamehe siku zote utabaki kuishi maisha ya siku za nyuma na si maisha ya sasa. Watu wanaoishi maisha ya siku za nyuma hawawezi kukamilisha ndoto zao kwa ukamilifu. “Msamaha haubadilishi wakati uliopita, lakini unakuza wakati ujao,” alisema Paul Boese.
Washindi ni wale wanaoishi maisha ya sasa na si yaliyopita, hawakukosea watu wenye hekima na akili waliposema: “Yaliyopita si ndwele, tugange yajayo.”
“Wasamehe wengine, siyo kwamba wanahitaji msamaha, lakini kwa sababu unahitaji amani,” anasema Jonathan Huie. Watu wenye vinyongo, chuki na hasira siku zote huwa wanaishi maishi yenye msongo wa mawazo. Ukisamehe unajipa amani ya moyo. Ukikosa kusamehe ni kujikosesha amani.
Yusufu pamoja na kuuzwa na ndugu zake utumwani Misri aliamua kuwasamehe. Yusufu aliwaambia ndugu zake: “Mimi ni Yusufu, ndugu yenu ambaye mliniuza kwenda Misri. Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinipeleke mbele yenu kuhifadhi maisha yenu.” (Mwanzo 45: 4-5).
Inawezekana waliokuumiza au kukukosea walikufungulia milango ambayo bila wao leo hii usingekuwa hapo ulipo. Yusufu aliuzwa na ndugu zake utumwani ambako baadaye alikuwa waziri mkuu. Kuuzwa kwake kulifungua njia ya yeye kuwa kiongozi wa juu. Alipitia mengi lakini aliamua kusahau na kufanya maisha yaendelee.
Nelson Mandela akiwa wakili alianzisha harakati dhidi ya ubaguzi wa rangi uliokuwa ukifanyika nchini Afrika Kusini. Hiyo ikasababisha yeye kuhukumiwa kifungo cha maisha kutoka serikali ya kikoloni iliyokuwa madarakani kipindi hicho.
Alitumikia kifungo hicho kwa miaka 27, mwaka 1990 aliachiwa huru. Baada ya kutoka gerezani huku akiwa amepoteza miaka 27 ya kukaa jela aliwasamehe waliomfunga na kuahidi kutengeneza serikali ya pamoja na wale waliokuwa wamemfunga.
Kufungwa kwake kulimfanya awe rais wa kwanza mweusi aliyeipatia uhuru Afrika Kusini. Nelson Mandela alikuwa na haya ya kusema kuhusu kusamehe: “Kidonda kikubwa tunachosababishiwa hakiwezi kupona mpaka pale tunaposamehe.” Akijua pia mchango chanya wa wale waliomfunga, alijigamba akisema: “Kwenye nchi yangu kwanza unakwenda jela halafu unakuwa rais.”
Mandela aliteswa, alifanyiwa ukatiri, alikosa haki za binadamu, halikosa uhuru kwa kipindi cha miaka 27 lakini alikubali kusamehe, huyu anaweza kuwa somo kubwa kwetu sote.
Muda mwingine tunawachukia watu kwa sababu walitukosea, tunaendelea kuibeba chuki hiyo siku hadi siku, waliotukosea wanaendelea na maisha yao bila wasiwasi wowote, sisi tunabaki tukiibeba chuki. Kubaki na chuki bila kusamehe ni kujiweka katika kifungo cha gereza ambacho kitabaki kukutesa siku zote. “Kusamehe ni kumwachia mfungwa huru na kugundua kuwa mfungwa huyo alikuwa na wewe,” anakazia Lewis B. Smendes.
Unapokesewa unazo chaguzi mbili; kusamehe au kutosamehe. Anayechagua kusamehe anakuwa amechagua fungu lililo bora zaidi. “Tusiposamehe, hatumuumizi mtu mwingine, hatuiumizi kampuni iliyotukosea, hatumuumizi Mungu. Tunajiumiza sisi wenyewe,” anatukumbusha Mchungaji Joel Osteen.
Immaculee Ilibagiza ni mwandishi na mhamasishaji aliyezaliwa mwaka 1972 nchini Rwanda. Mwaka 1994 wakati wa mauaji ya kimbali nchini Rwanda alipoteza familia yake wakiwemo baba, mama na kaka zake wawili (Damascene na Vianney), alibaki na kaka yake aliyeitwa Aimable ambaye alikuwa masomoni nchini Senegal wakati vita ikiendelea. Familia yake iliuliwa na wanajeshi wa Kihutu.
Wakati vita imeanza Immaculee alikwenda kujificha kwa mchungaji mmoja mwenye asili ya Kihutu, yeye alikuwa Mtutsi. Mchungaji aliwaficha pamoja na wanawake wengine saba katika bafu lililokuwa na vipimo vya mita 0.91 kwa mita 1.2, walikaa huko jumla ya siku 91.
Katika siku 91 alizokuwepo mafichoni siku zote alikuwa akisali, alipokuwa akisali sala ya ‘Baba Yetu’ na kufikia sehemu inayosema: “Utusamehe makosa yetu, kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,” alishindwa kutamka maneno hayo kwani ndani yake alikuwa na chuki isiyo ya kawaida dhidi ya wale wauaji.
Baada ya vita kwisha siku moja alikaa chini na kutafakari: “Kama namuomba Mungu kuniokoa katika chumba hiki nilichopo kwanini nisiwasamehe walionikosea?” Immaculee aliamua kuwasamehe walioipoteza familia yake. Ameandika vitabu viwili ‘Left to tell’ na ‘Led by choice’.