Mambo ni mengi muda mchache
“Muda ni kitu tunachokihitaji sana, lakini ndicho kitu tuna chokitumia vibaya,” anasema William Penn. Siku hizi ukipita mitaani utasikia watu wakisema, “Mambo ni mengi, muda mchache.” Ukweli ni kwamba mambo si mengi wala muda si mchache.
“Tatizo la muda linaanzia kwenye matumizi yetu ya muda. Linaanzia kwenye vipaumbele vyetu na jinsi tunavyoutumia. Kila dakika ya muda wetu, ikiwa tunaweza kusimamia hili vizuri, ikiwa tunaweza kudhibiti matumizi yetu ya muda, tutaona jinsi ambavyo tuna muda mrefu na kuweza kufanya chochote tunachotaka kufanya,” aliandika Makrita Amani kwenye kitabu chake kinachoitwa Biashara Ndani ya Ajira.
Usipokuwa na vipaumbele utampa kila mtu muda wako. Usipokuwa na vipaumbele utafanya mambo ambayo hata ulikuwa hujayapa ratiba. Kuwa navipaumbele ni muhimu kwa mtu yeyote mwenye ndoto na mwenye nia ya kufanikiwa.
Ili uwe mtu wa vipaumbele kila siku kabla ya kulala andika orodha ya vitu unavyotaka kuvifanya siku inayofuata. Ukiamka anza kufanyia kazi ratiba yako, usiache kufanya mambo ambayo hayapo kwenye orodha na kwenda kufanya mambo mengineyo, ‘fokasi’ kwenye orodha ya majukumu yako ya siku husika ndipo mambo mengine yafuate.
“Usiache mpaka kesho kitu ambacho unaweza kikifanya leo,” anashauri Benjamin Franklin.
Unaweza kusema kwamba hakuna muda wa kutosha na kuendelea kusisitiza ‘Muda ni mfupi’ ebu tizama hapa: Wiki moja ina saa 168. Unatumia saa 56, maana ya kwamba unalala saa 8 kila siku kwa kiwango kilichowekwa na wataalamu, ingawa kuna wanaolala saa pungufu. Unatumia saa 35 kula, kuoga, kuendesha gari, na kadhalika.
Unatumia saa 40 kufanya kazi katika wiki nzima. Ukijumlisha saa zote hapo juu utapata saa 131. Kwa hesabu za haraka haraka unabaki na saa 37 ambazo zinatosha kabisa kutimiza ndoto na malengo yako.
Jiulize saa zote 37 katika wiki umezitumia kufanya nini? “Habari mbaya ni kwamba muda unapaa. Habari nzuri ni kwamba wewe ni rubani,” anasema Michael Altshuler.
Jifunze kuongoza muda, si muda ukuongoze, muda unapaa na wewe ndiye rubani.
“Muda unapotea kwa namna ile ile kila siku,” anatukumbusha Paul Meyer, leo tazama ni mambo gani yanayokupotezea muda na anza kutumia muda huo kufanya mambo ya msingi.
Ukitumia muda wako mrefu kufanya mambo yafuatayo huwezi kubaki kwenye kundi la watu wanaosema mambo mengi muda mchache;
Mosi, tumia muda wako kufanya mambo ambayo umekuwa ukipenda kuyafanya. Jiulize huwa unapenda kufanya nini muda mrefu? Ni mambo gani yanakupa furaha maishani?
Siku moja mchezaji maarufu wa mpira wa kikapu wa Marekani, Kobe Bryant aliulizwa siri yake ya mafanikio ilikuwa ipi, yeye alijibu akisema, “Toka nikiwa mdogo nilikuwa nikitumia muda wangu mrefu kutazama wachezaji wengine mashuhuri walivyokuwa wakicheza hatimaye nimekuwa hivi nilivyo leo.”
Pili, tumia muda wako kufanya mambo ambayo watu wanasemahayawezi kufanyika. Kumbuka karibia kila kitu kilichopo leo kuna muda kilikuwa hakiwezi kufanyika, kunabaadhi ya watu walijitoa ufahamu na kwenda hatua ya ziada leo tunaona vitu kama magari, simu, vitabu, magazeti, nguo, na kadhalika.
Tatu, fanya mambo yanayoongeza uwezo wako kwa viwango vya juu.
Nne, fanya mambo yanayoongeza thamani kwako na kwa watu wengine. “Huwezi kufanikiwa kiroho, kifamilia, kiutawala, kielimu, kimaadili na kiafya kwa kuwaangusha wengine chini. Yule anayejitolea kuwasaidia wengine ndiye huinuliwa na watu aliowasaidia kuinuka,” aliandika William Bhoke.
Tano, fanya mambo yanayoibua ubunifu ulionao, “Huwezi kuwa mtaalamu ndani ya siku tano,” inatukumbusha methali ya Kiafrika. Watu wote unaowaona ni wabunifu na kuwasha ngaa au muda mwingine kuwaona wamebarikiwa na wana bahati zaidi yako wanatumia muda wao mrefu kukuza ubunifu wao.
Sita, fanya mambo yanayokuza umoja baina yako na wengine. Vidole vikikosa ushirikiano, mkono hauna maana. Meno yakikosa ushirikiano huwezi kutafuna chakula vizuri. Wewe pia ukikosa kushirikiana na wengine kuna mahali utakwama, usipende kufanya mambo peke yako, kidole kimoja hakivunji chawa.
Mwisho, fanya mambo mapya na yanayobeba fursa. Tumia muda wako kujifunza mambo mapya, tatua matatizo mapya.