Muda ni mali, utumie vizuri
Watu wanaoishi ndoto zao ni wazuri sana katika suala linalohusu matumizi ya muda.
Muda ni mali, utumie vizuri. Wakati mwingine utasikia watu wakisema muda ni pesa, lakini kwangu mimi jambo hilo ni la tofauti kidogo. Muda ni zaidi ya pesa, unaweza kupoteza pesa ikarudi, muda ukipita umepita. Hauwezi kuirudisha jana au mwaka uliopita.
Kinachowafanya watu wafanikiwe na kila siku wazidi kufanikiwa ni kuwa na nidhamu kubwa katika matumizi ya muda. Je, wewe unatumiaje muda ulionao?
Kuna wakati tunawatazama watu wanaoishi maisha ya ndoto zao na kuona wamebarikiwa kuwa na saa za ziada. Ukweli ni kwamba kila siku ina saa 24 na hiyo itabaki kuwa hivyo miaka nenda rudi, tofauti inakuja pale tunapoanza kutumia muda wetu.
Baadhi ya misemo ya Kiafrika imekuwa ikitufanya tusijali muda. Utasikia watu wakisema, “Hakuna haraka Afrika (No hurry in Africa)” Au wakati mwingine unakutana na mtu unamuuliza anakwenda wapi anakujibu, natembea tembea tu ili muda uende.
Sikiliza rafiki yangu, huwezi kufanikisha ndoto yako kama unatumia muda wako bila mpangilio au mkakati wowote. Siku ambazo huwa nasimamia kazi za ujenzi wa barabara huwa naona ni kwa namna gani baadhi ya watu ni wazuri sana kupoteza muda.
Unaweza kuanza kazi saa mbili asubuhi, ukakuta mtu anakuja kutazama tingatinga linavyochota mchanga kuanzia saa mbili hadi saa sita mchana. Huwa najiuliza huyu mtu hana kazi za kufanya? Unaweza ukaniambia kwamba mtu huyo labda kaliona tingatinga likifanya kazi kwa mara ya kwanza, lakini kadri siku zinavyoendelea mtu huyo huyo huja kutazama kitu kile kile.
Waafrika tukiwa na nidhamu ya muda tutafika mbali. Limekuwa jambo la kawaida kwamba ukipanga kukutana na mtu muda fulani lazima uweke nusu saa nyuma ili mtu huyo awahi. Kama mna mpango wa kukutana saa 3 asubuhi lazima umwambie afike saa mbili na nusu. Jambo la kushangaza utakuta mtu huyo anafika saa tatu kasoro dakika kadhaa. Utamaduni huu sio mzuri. Unaonesha kuwa Waafrika hatujali muda.
Usitumie muda wako mrefu kutazama televisheni, wale unaowatazama walitumia muda wao vizuri wakawa watu bora ndiyo maana unawatazama, jiambie mwenyewe, “Kuna siku watanitazama.”
Oprah Winfrey kabla ya kufanikiwa alikuwa akiendesha kipindi cha televisheni kwa miaka 25 mfululizo. Siku moja akiwa katika kipindi familia moja kutoka nchini Australia ilimpigia simu na kusema hawajawahi kukosa kipindi chake hata siku moja kwa miaka 25. Oprah Winfrey alikwenda kuwashukuru watu hao. Hawa ni watu waliotumia saa moja kila siku wakimtazama mtu mmoja anavyokuwa tajiri.
Siku moja bondia Floyd Mayweather alionekana akifanya mazoezi saa 11 alfajiri, mwandishi wa habari alimuuliza “Ni jambo gani linakufanya uzidi kufanikiwa?” Alijibu akisema, “Wakati wenzangu wamelala mimi nafanya mazoezi, wakiamka mimi nafanya mazoezi, wakirudi kulala mimi nafanya mazoezi.” Leo hii Mayweather ni bondia tajiri zaidi duniani. Tunaweza kufikiri kwamba anatumia muda wake mrefu ‘kula bata’ [kustarehe], hapana. Anatumia muda wake kufanya mazoezi; jambo linalomfanya abaki kileleni.
“Kuua muda ni kuzika fursa,” kama isemavyo methali ya Kiafrika. Fursa nyingi zinatupita leo hii kwa sababu hatukutumia vizuri muda wetu uliopita.
Wiki chache zilizopita nilisimuliwa maisha ya kijana ambaye ni mhitimu wa chuo kikuu hapa nchini. Kijana huyo amesomea mambo yanayohusu usindikaji vyakula na vinywaji. Ameanzisha kampuni yake inayosindika mtindi. Baadhi ya vijana waliosoma naye hivi sasa wanampigia simu ili awape kazi na wengine wanafikia hatua ya kumuomba awakumbushie baadhi ya fomula za kusindika maziwa kama yake.
Unaweza kuona wazi kuwa watu wa aina hiyo wanaoomba kazi na fomula ni watu ambao hawakujipanga. Walisoma kufaulu, na si kujua mambo yatakayowasaidia mtaani. Ukizunguka vyuoni utakuta wanafunzi wengi wakitumia muda mrefu kutazama tamthilia, kucheza ‘magemu’ na kufuatilia mipira ya Ulaya. Hili ndilo taifa la kesho tunalolisubiri mtaani. Msije sema sikusema.
Usipotumia muda wako mrefu kupambana kuishi maisha ya ndoto yako, kuna watu watakuajiri ili uwasaidie kutimiza ndoto zao. Tafakari, chukua hatua.