Anza na ulichonacho, anzia hapo ulipo
Anza na ulichonacho. Anzia hapo ulipo. Kusubiri kila kitu kikae sawa ndipo uanze ni kuchelewesha ndoto zako. Kusubiri kila kitu kikamilike ni sawa na kusubiri meli kwenye kiwanja cha ndege.
Muda sahihi wa kuanza kuishi ndoto zako ni leo, wala si kesho, kesho kutwa au wiki ijayo. Mwanamuziki Ben Pol aliwahi kuimba akisema: “Wakati wako ndiyo leo, kutimiza malengo yako, nakusihi anza sasa, jishughulishe utapata.” Anzia padogo ndipo utakapofika pakubwa. “Safari ya maili elfu moja huanza na hatua moja,” inatukumbusha methali ya Kichina.
Mtoto anayekimbia leo hii ni yule aliyekubali kuanza kutambaa. Siku moja nilikutana na gari lenye maneno yaliyosomeka: “Wanaanza kwa kutambaa.” Anafanikiwa yule anayeanza na si yule anayesubiri.
“Mtiririko wa maisha hutoa zawadi kwa vitendo chanya na huadhibu wanaozubaa,” anasema Robin Sharma.
Yusufu alianza kutafsiri ndoto zake, kisha akatafsiri ndoto za wafungwa wenzake akiwa gerezani, ndipo alipopata nafasi ya kutafsiri ndoto za Farao; kitu kilichomfanya awe kiongozi wa juu (waziri mkuu) katika serikali ya Misri ya wakati huo.
Mojawapo ya kitu kinachowakwamisha wengi kutimiza ndoto ni ukamilifu, kutaka kila kitu kikamilike ndipo aanze kitu alichotaka kukifanya.
Utasikia mtu akisema: “Nasubiri pesa fulani ikamilike ndipo nitakapoanza au nasubiri nimiliki kitu fulani ndipo nitakapoanza.” Ngoja ngoja ngoja huumiza matumbo.
Hakuna aliyekamilisha kila kitu ndipo akaanza kutimiza ndoto zake. Kila unayemuona amefanikiwa katika kuishi ndoto yake alikubali kuanzia hapo alipokuwa na kutumia rasilimali alizokuwa nazo kipindi hicho.
Nakumbuka mwaka 2016 nilikuwa na ndoto ya kuandika vitabu, lakini sikuwa na kompyuta, hiyo ilikuwa ni changamoto kubwa kwangu.
Nilianza kuandika makala kwenye blogu yangu kwa kutumia simu niliyokuwa namiliki kipindi hicho.
Siku moja nikasema, simu niliyonayo ndiyo itaniandikia kitabu ninachotaka kukiandika.
Mwaka 2017 nilifanikiwa kuandika kitabu kinachoitwa ‘Barabara ya Mafanikio’, ambacho kimeuza nakala nyingi, lakini pia kimebadilisha maisha ya wengi.
Inawezekana usingenifahamu leo hii kama nisingeamua kuandika kitabu hicho.
Kitu ambacho watu wengi hawakifahamu ni kwamba zaidi ya asilimia 80 ya kitabu hicho iliandikwa kwa kutumia simu. Nilianza kumiliki kompyuta wakati namalizia kuandika kitabu hicho. Ukiamua unaweza, hakuna kinachoshindikana kwa mtu mwenye nia. “Watu wenye nia, wanaweza kuibadili dunia,” anakazia Steve Jobs, mwanzilishi wa Kampuni ya Apple Inc.
Fikiria, kampuni zinazotengeneza simu, kila mwaka hutoa toleo jipya la simu waliyokwisha kutengeneza kabla. Hiyo ina maana kwamba waligundua toleo lililopita lina upungufu fulani, hivyo wakaamua kutoa toleo bora zaidi. Kumbuka hawakuanza kutoa toleo bora zaidi, bali walianza kutoa toleo lililokuwa ndani ya uwezo wao, walianzia walipokuwa. Naunga mkono maneno ya Mark Zuckerberg, mwanzilishi wa mtandao wa facebook aliyewahi kusema: “Mawazo siku zote hayaji yakiwa yamekamilika. Yanaanza kuonekana pale unapoanza kuyafanyia kazi. Lazima uanze.”
Kuna vitabu ambavyo vikiandikwa, baadaye matoleo mapya ya vitabu hivyo hutolewa, hiyo pia ina maana kuwa kuna sehemu mwandishi aligundua makosa ya kiuandishi au alitaka kuongeza baadhi ya vitu ambavyo awali havikuwemo katika toleo lililopita. Huyo naye alianza na alichonacho. Hakusubiri kukamilisha kila kitu.
Mwaka 1992 wakati wa Sikukuu ya Krismasi, meseji ya kwanza duniani ilitumwa kwa njia ya simu, ilisomeka: “Heri ya Sikukuu ya Krismasi.” Leo hii mamilioni ya meseji yanatumwa.
Inawezekana isingegundulika meseji watu wengi wangekuwa bado wanatumia barua, maana iliaminika hapo nyuma kwamba barua ni nusu ya kuonana.
Kutokana na takwimu za Lori Lewis, leo hii mwaka 2019, ndani ya sekunde sitini (dakika moja); ujumbe mfupi milioni 18.1 unatumwa, meseji milioni 41.6 zinatumwa kupitia mitandao ya whatsapp na facebook, barua pepe milioni 188 zinatumwa na watu 87,500 huandika katika kurasa zao za twitter.
Hakuna wazo litakalofanya kazi mpaka uanze kulifanyia kazi. Ukitaka kutimiza ndoto zako, anza na ulichonacho. Anzia hapo ulipo leo hii.