Ongeza thamani kwa ukifanyacho

Mchezaji bora katika timu si yule mwenye umri mkubwa zaidi ya wachezaji wengine au aliyeitumikia timu kwa muda mrefu, bali ni yule mwenye thamani.  Ndiye hulipwa zaidi ya wote.

Thamani ni gharama au ubora wa kitu kutokana na hali na kuhitajika kwake kwenye jamii.  Kila  unachokifanya kitakulipa kuendana na thamani unayoitoa. Ukiwa kazini usifikiri kwamba unalipwa kwa saa nane unazoyafanyia kazi kila siku, hapana.

Unalipwa kutokana na thamani unayoitoa. Kadri unavyoongeza ubora wako, thamani yako itapanda. Watu wenye hekima hawakukosea waliposema, “Utavuna ulichopanda.”

Ongeza thamani katika bidhaa yako kama wewe ni mfanyabiashara. Kila siku jiulize maswali haya: Nitawezaje kufanya kwa ubora zaidi ya jana? Au ni mbinu gani nizitumie ili nibaki na wateja nilionao na nizidi kuwatafuta wateja wengine zaidi? Kuwa na upendo kwenye kitu unachokifanya. “Kama ukipenda unachokifanya na ukakifanya vizuri, pesa itafuata,” anasema Samantha Wills, mbunifu wa vidani na mjasiriamali.

“Lolote mkono wako utakalolipata kulifanya, ulifanye kwa nguvu zako zote.” (Mhubiri 9:10).

Ili uongeze thamani kwenye unachokifanya, fanya mambo yafuatayo; kwanza, tengeneza falsafa yako. Falsafa ni mtazamo au hekima yako. Falsafa ni mambo unayoyaamini wewe kuwa kweli. Hii itakusaidia ujue ni uwezo gani ulionao na upi huna.

Falsafa yako itakusaidia uwezo kuona mambo hasi yanayoweza kutokea katika upande mmoja, lakini pia kuona fursa zinazoweza kujitokeza kutoka upande mwingine.

Pili, jifunze kila siku. “Ukiacha kujifunza, unaanza kufa,” alisema Albert Einstein, mwanafizikia mwenye asili ya Kiyahudi  na mshindi wa tuzo ya Nobel ya Fizikia mwaka 1921. Watu wengi hufikiri kuwa wakihitimu shule au chuo kujifunza kumeishia hapo, kwa msingi huo Benjamin Franklin aliyewahi kuwa balozi wa Marekani nchini Uswidi na mwandishi wa vitabu alikuwa na haya ya kusema, “Watu wengi wanakufa wakiwa na miaka 25 na hawazikwi mpaka wanapofikia miaka 75.”

Kuacha kujifunza katika karne hii ya taarifa na maarifa ni sawa na kuwa marehemu kaburini.

Jifunze kutokana na mambo unayoyaona. Umepewa macho yatumie ipasavyo. Mwenye macho haambiwi tazama.

Jifunze kutokana na unayoyasikia. Unaweza kusikiliza watu wanasema nini, au ukajifunza kutokana na mafundisho katika semina au warsha. Kumbuka kuwa msikilizaji makini anayeweza kuchuja anayoyasikia maana si kila unaloambiwa ni jambo la kubeba. Kuwa msikilizaji mzuri maana watu wengi si wasikilizaji wazuri, bali hupenda kusikia tu yale wanayopenda kuyasikia.

Jifunze kutokana na maisha yako ya nyuma. Hapa unaweza kujifunza kutokana na makosa uliyoyafanya kwani wanasema makosa ni jiwe la kukanyagia kuelekea hatua ya ziada. “Nyakati mbaya zina thamani ya kisayansi. Haya ni matukio ambayo mwanafunzi mzuri hapaswi kuyakosa,” anasema mwanafalsafa wa karne ya 19, Ralph Waldo Emerson.

Jifunze pia kutokana na mafanikio uliyopata, jiulize ni mbinu zipi zilikufikisha katika hatua hiyo.

Jifunze pia kutokana na maisha ya nyuma ya watu wanaofanya kitu kama unachokifanya. Siku hizi ni rahisi sana kuwasiliana na watu wengi kutokana na kukua kwa sayansi na teknolojia. Wafuatilie watu wanaofanya kitu kama unachokifanya kwenye mitandao ya kijamii kama kwenye kurasa zao za Instagram, Facebook na Twitter.

Unaweza kujifunza mambo mengi kutoka kwao. Usitumie muda wako mrefu kwenye mitandao ya kijamii kufuatilia watu wengi wasiofanya kitu kama chako. Tai huruka na tai wenzake. Jifunze kutafuta tai wenzako ili muweze kuruka pamoja. Ukiwa tai, usipende kukaa na kuku kwani hawawezi kuruka na kupaa juu, watakudumaza.

Mwisho, soma vitabu vyote unavyotamani kuvisoma, vitabu vinavyohusu maendeleo binafsi, vitabu vya biashara, vitabu vilivyoandikwa na watu waliofanya kazi kama unayoifanya, soma vitabu vya historia za watu unaotamani kuwa kama wao. Vitabu vinaongeza uelewa. Vitabu vinakuza fikra. Vitabu vina siri kubwa ambazo wengi hawazifahamu ndiyo maana watu wanafika hatua ya kusema, “Ukitaka kumficha Mwafrika weka kwenye maandishi.”

Kumbuka unaposoma vitabu na kuona kitu kinachoweza kukusaidia chukua hicho kitu na anza kukitumia mara moja. kuwa na hamasa bila vitendo, utapata tabu sana.

“Jitahidi usiwe mtu wa mafanikio, bali kuwa mtu wa thamani,” anatukumbusha mwanafizikia, Albert Einstein.