Ukiamua kufanya, fanya kweli

 

Fanya mambo kwa ubora. Chochote unachokifanya hakikisha unakifanya vizuri  na kwa ubora wa hali ya juu; kiasi kwamba watu wakikiona wawe tayari kuwaambia wengine kuhusu wewe. Hata mimi nikiona kazi yako unaifanya kwa ubora nitakuwa tayari kuwaambia wengine na kutoa sifa bora juu yako wewe, hii imekuwa tabia yangu.

Watu wanapenda ubora, watu wanapenda vitu vizuri. Ukifanya mambo kwa ubora ni rahisi kufanikiwa mapema.

Ubora utakutangaza, wala hautatumia nguvu na gharama nyingi kujitangaza.

Yusufu alitumia kipaji chake cha kutafsiri ndoto kwa ubora sana, ndiyo maana aliweza kuwa kuwa kiongozi mkubwa, waziri mkuu wa nchi ya Misri. Huyu alikuwa kiongozi bora na si bora kiongozi.

Kampuni kubwa kama Apple na Samsung hutumia ubora  kuzipiku kampuni nyingine zinazotengeneza simu. Wao hutengeneza simu nzuri na bora, wateja wao baada ya kuzipenda ndio huwa watangazaji wa bidhaa zao.

Penda unachokifanya na kifanye kwa ubora siku zote. Fanya kazi kwa bidii na kubali kwenda hatua ya ziada.

Wanasema: “Hakuna msongamano kweye hatua ya ziada.” Anafanikiwa yule anayekwenda hatua ya ziada.

Ukiwa na biashara tafuta kitu ambacho kitakutofautisha na wengine katika huduma unayotoa. Kuwa tofauti, usifanane na wengine. Utofauti wako katika huduma unayotoa ndiyo utawafanya wateja waendelee kuja kwako na si kwenda kwingine.

Kwa mfano, kama unamiliki hoteli unaweza kutoa ofa ya sharbati (juisi) kwa kila sahani ya chakula au ofa ya yai moja kwa kila anayefika kwenye hoteli yako kupata kifungua kinywa. Hiyo ni huduma ya tofauti ambayo itamvutia mteja aendelee kutumia huduma yako.

Tunaweza kujifunza kwenye baadhi ya kampuni za simu hapa nchi ambazo mtu akiwa anasherehekea kumbukizi  ya kuzaliwa huwa wanamzawadia dakika, SMS na MBs – ni huduma fulani  tofauti ambayo humfanya mteja ajisikie fahari ya kuchagua mtandao husika. Mteja huyo anaweza kuwa mteja wa kudumu.

Ili ndoto yako itimie, kufanya mambo kwa ubora ni mojawapo ya mahitaji muhimu kama ilivyo sukari na majani kwenye chai. Kuwa mchezaji bora na si bora mchezaji, kuwa mwandishi bora na si bora mwandishi, kuwa kiongozi bora na si bora kiongozi, kuwa mwanafunzi bora na si bora mwanafunzi.

Kufanya mambo kwa ubora huanzia mahali ulipo. Usisubiri ufikie hatua fulani ndipo useme nitaanza kufanya mambo vizuri na kwa ubora. Ukifanya hivyo unajidanganya mwenyewe. “Mbwa mzee huwezi kumfundisha mbinu mpya,” ni msemo wa Kiingereza.

Kama umeajiriwa na una ndoto ya kumiliki biashara au kampuni yako anza kuonyesha ubora kwenye kampuni au kazi ya mwajiri wako. Fanya kazi kana kwamba wewe tayari ni mkurugezi wa kampuni utakayoianzisha. Usisubiri uanzishe kampuni au biashara unayotamani kuifanya ndipo uanze kutoa huduma bora, utakuwa umechelewa.

Tatizo la  wengi ambao wameajiriwa katika sekta binafsi au serikalini hufikiri wakifanya kazi kwa ubora wanaifaidisha serikali au waajiri wao. Kazi unayoifanya leo hii inaweza kuwa jiwe la kuvukia kufikia ndoto zako. Usiifanye kwa kuangalia unamfanyia nani. Ifanye kwa kuangalia siku za usoni itakupeleka wapi.

Kuna watu waliofanya kazi benki na kuacha kazi wakaenda kufungua biashara zao. Huduma wanazotoa ni nzuri sana, lakini walijifunza kutoa huduma hizo wakiwa wanafanya kazi wa benki.

Niliwahi kusoma stori ya maisha ya mama  ambaye alikuwa akisafisha vyoo katika ofisi za serikali mahali fulani hapa nchini. Siku moja tajiri maarufu alikwenda katika ofisi zile kufuatilia mambo fulani.

Alipofika mahali pale alikwenda msalani kujisitiri. Alikuta kumefanywa usafi wa hali ya juu. Alishangaa sana, lakini akajisemea kimoyo moyo labda kwa sababu ni asubuhi.

Mchana wa siku ile akarudi tena na kupitia msalani. Alikuta ni kusafi kuliko alivyokuta asubuhi. Akawauliza watu wa mahali pale, nani anayefanya usafi.

Wakamwambia ni mama mmoja anayeishi jirani na zile ofisi.

Tajiri yule akaomba kukutana na yule mama ofisini kwake. Alipofika  akamuuliza: “Ni kitu gani kinakufanya ufanye usafi namna ile?” Yule mama akajibu:

“Naipenda sana kazi yangu, ndiyo inayoniweka mjini.”

Yule tajiri akamwambia fungua kampuni ya usafi mara moja. Kilichofuata ni historia.

Yule mama alipewa zabuni ya kufanya usafi kwenye ofisi za yule tajiri na amekuwa akipata zabuni nyingine za usafi kwenye ofisi mbalimbali.