Maisha yanabadilika, watu wanabadilika
Siku si nyingi zilizopita nilikutana na rafiki zangu niliosoma nao kuanzia darasa la sita hadi kidato cha nne. Ilikuwa siku ya furaha sana kwani kuna watu sikuwahi kuonana nao tangu tukiwa shule. Kila mtu alionyesha uso wa furaha.
Siku hiyo tulianza kukumbushana maisha yetu ya nyuma huku tukiulizana wengine wako wapi na wanafanya nini leo hii. Walioweza kufika kila mtu alitoa maelezo yake na kimsingi kila mmoja alichukua somo kubwa siku hiyo. Waliokuwa wanakaribia kukata tamaa tuliwatia moyo, wale waliopiga hatua tulikuwa na wasaa wa kuwaongezea nguvu wazidi kupambana zaidi na zaidi, kwani wamekuwa watu wanaotuhamasisha pia tuzidi ‘kukaza buti’.
Siku hiyo kwangu binafsi ilikuwa ni siku ya baraka sana kwani nilipata ‘shule’ moja kubwa sana. Kama ni somo la kusoma kwa muhula mmoja, basi mimi nilisoma somo hilo ndani ya siku moja, tena kwa saa chache.
Kikubwa nilichojifunza siku hiyo ni kwamba maisha yanabadilika na watu pia wanabadilika. Kati ya watu tuliokuwa nao pale na wengine hawakufika ambao tulipewa habari zao kusema ukweli tulibaki mdomo wazi. Kuna watu ambao darasani walionekana wanyonge mno wasioweza kufanya lolote la maana. Leo hii wanafanya mambo makubwa. Wamefungua biashara kubwa na wanaziendesha vizuri.
Wengine enzi za shule tuliwacheka kwa sababu hawakujua vizuri lugha ya Kiingereza, leo hii wanaongea Kiingereza kiasi kwamba baadhi ya maneno yatusapa tutumie kamusi kuyaelewa. Ama kweli maisha yanabadilika na watu pia wanabadilika.
Pia kuna ambao walionekana wanaongoza darasani, lakini kwenye maisha wameshindwa kuongoza. Hapa naomba nisieleweke vibaya kwamba ukiwa unaongoza darasani, basi kwenye maisha hutaongoza. Hiyo ni topiki nyingine na nitaijadili kwa undani siku zijazo.
Tangu siku hiyo kuna mambo mengi nimejifunza na bado naendelea kujifunza. Kwanza kabisa ni kumheshimu kila mtu bila kutazama umri au uwezo wake. Unaweza kuona mtu ana uwezo mdogo leo, kumbe baadaye mtu huyu huyu akafanya mambo makubwa.
Siku moja Thomas Edison akiwa katika madarasa yake ya chini kabisa mwalimu wake alimwandikia ujumbe uliosomeka, “Mwanao hana akili hawezi kujifunza.” Mama yake baada ya kuusoma ujumbe hule alimjibu mwalimu kwa kumwandikia ujumbe uliosomeka, “Mwanangu hana akili, nitamfundisha
mwenyewe.” Kilichotokea baada ya hapo ni historia. Thomas Edson ndiye mgunduzi wa balbu ya umeme na kamera na vitu vingi vya kielekitroniki.
Jambo jingine nililojifunza ni kwamba mafanikio yako yanategemea mtandao wako. Unavyowafahamu watu wengi na wao wakakufahamu ni rahisi kufanya mambo mengi yakafanikiwa. Hata uwe na akili nyingi za darasani kiasi gani kama huna mtandao wa watu, mafanikio jiandae kuyasikia kwa wengine. Tengeneza mtandao, wafahamu watu, jiunganishe na watu, nenda mahali ambako watu unaotamani kufahamiana nao wanakwenda, tafuta mtu mmoja anayekuhamasisha na jifunze namna anavyohusiana na watu.
Kilichomfanya Yusufu awe Waziri Mkuu ni kuwa na uhusiano mzuri na wafungwa wenzake .
Sikuishia hapo tu, bali nilijifunza kuwa nyuma ya ushindi kuna misukosuko. Hakuna maisha mepesi, maisha yakikaza unakaza zaidi. Maisha ya kuishi ndoto yako yanahitaji kulipa gharama. Ukikwepa gharama jua kwa namna moja au nyingine siyo jambo rahisi kufanikisha ndoto yako.
Pamoja na misukosuko ya maisha, kinachofuata ni kufurahia kile ulichokuwa ukikihangaikia. Yusufu alivuliwa koti na ndugu zake, alipofika nyumbani kwa Potifa ambako aliuzwa kama mtumwa, Potifa akampa koti jingine. Mkewe Potifa naye kama ndugu zake akamvua koti lake alilopewa na bosi wake kwa kisingizio cha kwamba Yusufu alitaka kumbaka. Ni shida baada ya shida, lakini kama wasemavyo wahenga, “Baada ya dhiki ni faraja.”
Baada ya Yusufu kutafsiri ndoto ya Farao, alivalishwa pete na vazi zuri. Yawezekana vazi hilo lilikuwa limebuniwa na mbunifu maarufu wa nchi ya Misri.
Watu wanaweza kukutupa shimoni kama Yusufu, kumbe shimo ni njia mojawapo ya kwenda nchi yako ya Misri. Kuna wakati unaweza kufikiri umezikwa kumbe umepandwa.