Wivu ni kidonda, ukishiriki utakonda
Wivu ni hali ya kutofurahia kwa kumuona mwenzio akiwa na mtu au kitu. Wivu ni hisia yenye nguvu inayoweza kumfanya mtu ahisi hangaiko, huzuni au awe na hasira.
Waswahili wamelipa neno ‘wivu’ majina mengine kama: kijicho, gere, husuda, uhasidi, na kadhalika.
Wivu siku zote huwezi kuona chema cha mtu, bali huona baya la kila mtu. Watu wakisema mtu fulani ni mkarimu, mwenye wivu atatoa simulizi mbaya kuchafua picha yake ya ukarimu.
Wivu huzaa chuki. Wivu hudumaza. Badala ya kuwaza kuhusu maisha yake, mtu mwenye wivu anatumia nguvu nyingi kumuwaza mtu anayemwonea wivu.
Mwenye wivu siku zote hataki wengine wafanikiwe. Mara zote atataka yeye abaki kileleni, mwingine akipewa sifa yeye huumia. Wivu ni kidonda, ukishiriki utakonda.
Ukitaka kuwa mtu wa viwango vya juu epuka wivu. Wivu ni mateso unayojitengenezea. Wivu ni sawa na kubeba msalaba usio wako, wakati imeandikwa “Kila mtu aubebe msalaba wake.”
“Wivu ni kansa ya akili,” alisema B.C. Forbes. Kama tunavyojua kwamba kansa ni ugonjwa hatari, kwanini bado tunaona wivu juu ya wenzetu? Mwenye wivu hata akiwa na kingi, akiona mwenye kidogo bado roho yake itaumia. Ni sawa unaendesha gari na unapishana na mtu anaendesha baiskeli na bado roho inakuuma. “Unaweza kuwa mwezi na bado ukazionea wivu nyota,” ni maneno ya Gary Allan.
Usiwe mtu wa kuwaonea watu wengine wivu. Usitamani warudi nyuma kwani huwezi jua watu hao ndio wanaweza kuwa wameibeba hatima yako. Nduguze Yusufu walimwonea wivu baada ya kuwaambia ndoto zake. Wakaamua wamuue, baadaye wakabadili uamuzi na kumuuza kama mtumwa.
Baadaye Yusufu huyu huyu anakuja kuikomboa familia yake isife njaa. Unaweza kuishi na mtu na ukaanza kumwonea wivu katika nafasi aliyonayo kumbe unafukuza baraka. Ni sawa na vidole vya mkono kukionea wivu kidole gumba kwa sababu ya unene na kuwa kidole cha kwanza. Vidole hivyo vinasahau kuwa kidole gumba kikikatwa mkono huwezi tena kushika kiktu vizuri.
Jenga tabia ya kufurahia mafanikio ya wengine. Wapongeze wengine wanapofanya kitu kizuri. Usiruhusu wivu utawale maisha yako. “Usipoteze muda wako kwenye wivu, wakati mwingine utakuwa mbele, wakati mwingine utakuwa nyuma,” alishauri Mary Schmich.
“Kutoka kwenye kisima cha wivu, ni wapumbavu tu ambao hunywa maji,” ni msemo wa watu wa Nigeria.
Msemo wa Kilatini usemao, “Furahi na wanaofurahi, lia na wanaolia,” unatukumbusha kuwa na wengine katika mambo yao. Mtu akipandishwa cheo mpongezi, sio useme, “Huyu kijana anakuja juu siku hizi angalia asijechukua nafasi zetu.”
Rafiki yako akivaa viatu vizuri mpongeze, lakini usiseme, “Nilikuwa na viatu kama hivyo viliharibika haraka.” Huo ni wivu. Ukiona rafiki yako amenunua simu mpya mpongeze bila kuongeza maneno kama, “Simu nzuri, lakini siwezi kulipia laki nne kununua simu ambayo siyo iphone.”
Mwenzio akipata mchumba achana na viji-neno vya chinichini kama, “Mpenzi wako anapendeza, lakini nimekuwa nikifurahia wanaume wenye ngozi ya rangi ya hudhurungi.” Huo ni wivu.
Wenye wivu siku zote hawakosi maneno ya kuongea. Mtu akinunua gari, wakiona ameegesha siku mbili au tatu anakwenda kazini kwa kutembea m (lengo lake likiwa kufanya mazoezi) utasikia, “Siku hizi amefulia, gari alinunua sijui alifikiri wanaweka maji!”
Palitokea mkulima aliyekuwa akifuga mbwa na jogoo. Alimlisha nafaka na akamlisha mbwa nyama. Siku moja jogoo akafikiria kama mbwa asingekuwapo, basi angekula chakula chote peke yake.
Akaamua kwenda porini akaparua mizizi yenye sumu. Akaja akamwekea mbwa kwenye chakula. Mbwa akatapika sana. Mkulima yule kwa vile alimpenda mbwa, akaamua amchinje jogoo ili mbwa wake anywe supu apone.
Kwa hiyo jogoo akaishia kuwa chakula cha mbwa. Wivu ni kidonda, ukishiriki utakonda.
Ukiwa mtu wa kuyafurahia mafanikio ya wenzako, hata Mungu anafungua milango ya baraka kwako. Mungu atakuunganisha na watu wapya, fursa zitaanza kukujia.
Hakuna mtu atakayependa kufanya kazi na wewe kama utakuwa mtu wa kuwasema wengine vibaya, kama utakuwa mtu wa kuwaonea wengine wivu. Watu watakukimbia kama ukoma. Iponye nafsi yako kwa kuiepusha na wivu.
“Wivu hauli chochote isipokuwa moyo wake,” ni msemo wa Kijerumani.