Niongee lini, ninyamaze lini?

 

Baada ya kuandika makala yenye kichwa kisemacho: “Ukiwa na ndoto usipige kelele, kaa kimya,” katika Gazeti la JAMHURI, Toleo Na. 411 la Agosti 13-19, 2019 nimepongezwa na wasomaji kwa kunipigia simu wakiniambia kuwa makala hiyo imegusa maisha yao na itawasaidia.

Mmoja wao ambaye amekuwa mfuatiliaji mzuri wa makala za ‘Nina Ndoto’ kutoka Arusha aliniuliza swali zuri: “Je, nikae kimya muda wote? Na kama kuna muda wa

kuzungumza, niongee lini na ninyamaze lini?”

Akaendelea kusema inawezekana tunasema watu wakae kimya, basi ndiyo wakakaa kimya muda wote. Akaomba nielezee kwa undani ukimya niliouzungumzia.

Hakuishia hapo, akaendelea kusema yeye ni mjasiriamali na anamiliki shule. Aliwahi kuwapeleka

wanafunzi wake nchini Kenya kwa shughuli za kimichezo. Baada ya kurejea aliweka picha za matukio hayo mtandaoni. Mtu mmoja baada ya kuona hivyo akamwambia asitangaze, anajionyesha sana.

Akauliza: “Je, ni kweli nilistahili kukaa kimya kwa kufanya kitu hicho?” Nikasema: “Hapana, tena hapana kubwa.”

Akaniomba kwa mara ya pili nizungumzie kwa undani ukimya huo niliouzungumzia. Basi, na mimi nikamwahidi kutomwangusha kwa hilo. Hivyo nikasema nitaandika kuelezea kwa undani.

Ukiwa na ndoto si kwamba muda wote ni wa kukaa kimya na si muda wote ni wa kuongea. Kila jambo na wakati wake. Tatizo kubwa walilonalo watu wengi wanatumia nyakati hizi kwa kuzichanganya. Muda ambao mtu anatakiwa kuongea, yeye ananyamaza na muda ambao anatakiwa kunyamaza yeye anaongea.

Maana yangu ya kusema: “Ukiwa na ndoto usipige kelele, kaa kimya,” niliwalenga wale watu ambao muda wa kunyamaza wao wanaongea.

Ukitaka kuwaalika watu kula chakula mezani unaanza kukiweka mezani kisha unawaalika wajongee kula chakula ulichoandaa. Tatizo la watu wengi lipo hapa: wanawaalika watu kula chakula kabla hata hawajaenda sokoni.

Si rahisi mtu mwenye njaa akusubiri wewe uende sokoni na urudi, uanze kupika, kiive, kisha ndipo aje kula. Hata ningekuwa mimi mate ya hamu ya chakula yangenitoka hadi yaishe, nisahau kama nilipaswa kula chakula.

Ndoto nyingi zinakufa kwa sababu watu wanaalika wengine muda wa kwenda sokoni badala ya kuwaalika muda chakula kinapokuwa tayari. Hapa namaanisha nini? Si jambo jema kutangaza ndoto zako katika hatua za mwanzo. Pambana mwenyewe kimya kimya au kama nilivyosema kwenye makala, ndoto yako waifahamu tu wale unaowaamini na ambao kwa namna moja au nyingine wanaweza kuwa msaada mkubwa wa wewe kuifanikisha (niliandika katika makala niliyoitaja hapo juu).

Kama ilivyo kwa muda wa kukaa kimya, kuna muda pia wa kuongea ndoto zako mbele za watu. Kama nilivyotangulia kusema, watu wengi hutumia nyakati hizi kwa kubadilishana, muda wa kuongea, hunyamaza na muda wa kunyamaza huongea.

Ukikaa kimya muda wa kuongea unafanya kosa kubwa. Inawezekana kuna mtu bado anajiuliza, je, niongee lini? Ongea muda ambao tayari mambo yamekuwa tayari. Ni kama yule anayeandaa chakula, anawaalika watu chakula kinapokuwa tayari na amekiandaa vizuri mezani. Huyo

asipowaalika watu, chakula chake hakitaliwa.

Umelima shamba kubwa la matunda na mboga mboga, msimu wa mavuno unapokaribia waambie watu utavuna karibuni na unatafuta wateja. Kama wasemavyo walimwengu, biashara ni matangazo. Kama watu hawasikii lolote kuhusu wewe, unafikiri watakuwa wateja wako? Hapana.

Muda ambao unataka watu wajue kitu unachokifanya hakikisha watu wanajua. Huo ndiyo muda wa kupiga kelele sasa.

Msomaji wangu baada ya kuwapeleka wanafunzi wa shule yake Kenya alikuwa na haki ya kuuonyesha umma kuwa shule yake inathamini michezo na talanta mbalimbali za watoto. Hiiitawafanya wazazi wengi wapeleke watoto wao katika shule yake.

Tunaweza kusema mtoto akisoma katika shule hiyo anakuwa anaua ndege wawili kwa jiwe moja, yaani anajifunza mambo ya darasani, lakini pia anakuza kipaji chake kupitia michezo (wanamichezo ndio watu wanaolipwa zaidi duniani).

Yamkini una kitu chako kikubwa umekifanya, usikae kimya. Iambie dunia wewe ni nani na umefanya nini.

Usiwashe mshumaa na kuuficha uvunguni. Uweke mezani umulike kote. Kumbuka waambie watu ndoto zako ukiwa katika hatua nzuri na si katika kuanza.