Nitawezaje kuamka mapema?
“Ni jambo la aibu, ndege wa angani waamke kabla yako,” alisema Abu Bakr, rafiki wa karibu sana wa Mtume Muhammad.
Siku moja wakati natazama video katika mtandao wa Youtube nilikuta video iliyokuwa ikimuonyesha bondia maarufu Floyd Mayweather. Video hiyo ilimwonyesha akifanya mazoezi kando ya bahari saa 10 alfajiri. Baada ya kuulizwa kwanini anafanyahivyo alijibu, “Wenzangu wakiwa wamelala mimi nafanya mazoezi,wakiamka bado nafanya mazoezi, wakilala tena wananiacha nikifanya mazoezi. Hiyo ndiyo siri ya ushindi wangu kila mara.”
Kuamka mapema ni neno lisilokosa katika kinywa cha mtu yeyote aliyefanya mambo makubwa katika dunia hii.
Wakati naandika maneno haya nimekutana na maneno ya mwalimu wangu Dokta Crn Charles katika mtandao wa Facebook akisema,“Njia mojawapo ya kufanikiwa, ni kulala saa chache mno, kutozungumzia watu ila maendeleo, kutochochea wivu ila kuchochea njia za kufanikiwa, kuchagua watu sahihi wa karibu nawe, kuona yasiyowezekana kuwa yanawezekana….Chanzo cha fursa ya mafanikio ni wewe binafsi kabla ya wengine na mengine.”
Inawezekana mpaka naandika haya yote kuhusu kuamka mapema bado kuna swali linakatiza kichwani kwako likiuliza, “Nitawezaje kuamka mapema, wakati nimezoea kuamka saa 3 asubuhi?”
Kitu cha kwanza cha kujua hapa ni kwamba kuamka mapema ni tabia, na tabia hujengwa. Unapotaka kujenga tabia mpya unahitaji kuwa na nidhamu kubwa ili kuifanyia kazi tabia hiyo kila siku kwa wakati sahihi.
Watu ambao hawafanyi mambo kwa wakati sahihi ni watu waliokosa nidhamu ya maisha yao ya kila siku.
Kumbuka, leo wewe ni mzee ambaye hujawahi kuwa, lakini pia leo wewe ni mdogo ambaye hautawahi kuwa. Utumie kila wakati vyema.
Kuamka mapema kunahitaji nidhamu ya hali ya juu na pia kujitoa. Yaani, ukisema ninaamka, amka kweli kwa sababu ukilala na ndoto zako zinalala. Lakini ukiamka na ndoto zako zinatimilizika. Ndoto zako unazifanya kuwa kweli.
Uchunguzi unaonyesha kuwa tabia mpya hujengwa ndani ya siku 30ambayo ni sawa na mwezi mmoja. Kumbe ili ufaulu kuamka saa 10 au 11 alfajiri, lazima upitie maumivu makali ya kufanya mazoezi ya kuamka muda huo.
Ukiweza kuamka saa 10 au 11 alfajiri kwa muda wa mwezi mmoja mfululizo tayari mwili utazoea na utaona kuamka mapema ni kitu cha kawaida. Tatizo linalowapata watu wengi hujaribu wiki moja na kuacha. Huwezi kujenga tabia yoyote.
Waandishi wa kitabu cha The Miracle Morning For Writers, Hal Elrod na Steve Scott wametoa njia nzuri ambazo ukizitumia unaweza kufaulu kuamka mapema kila siku. Njia hizo ni:
Mosi, Weka Malengo Kabla ya Kulala. Kabla hujalala weka malengo ambayo unatakiwa kuyatimiza siku inayofuata. Kama ni mwandishi andika, utaandika sura ngapi na zitahusu nini.
Pili, Weka ‘Alamu’ Mbali na Kitanda Chako.
Watu wengi wamekuwa wakiweka ‘alamu’, lakini zinapolia wanaamka haraka na kuzizima wakati wameziweka wenyewe. Si wewe tu, hata mimi nilikuwa nikifanya hivyo, lakini niliacha. Ili uweze kuepuka jambo hilo hakikisha ‘alamu’ ipo mbali na kitanda chako kiasi kwamba itakulazimu uamke na kutembea ili uizime. Ukifanikiwa kufanya hivyo si rahisi tena kwako kurudi kitandani. Ugumu wa kuamka mara nyingi upo katika kutoka kitandani.
Tatu, Fanya Usafi wa Kinywa. Mara tu baada ya kuzima ‘alamu’ nenda kafanye usafi wa kinywa.
Nne, Kunywa Glasi ya Maji. Baada ya kufanya usafi wa kinywa tayari utakuwa umekuwa msafi kinywani hivyo unashauriwa kunywa glasi moja ya maji au zaidi.
Umesikia, “maji ni uhai.” Ukinywa maji mara tu baada ya kuamka unafanya mwili wako uwe mchangamfu siku nzima. Usisubiri hadi uandikiwe dozi na daktari au uugue mafua ndipo ukumbuke kunywa maji.
Fanya unywaji maji kwako uwe tabia ya kila siku. Lakini pia kama umefuatilia watu wengi wanaokunywa maji mengi hawaugui mara kwa mara.
Wataalamu wanasema kila mwanadamu inabidi anywe lita moja na nusu ya maji kwa siku kwa kiwango cha chini. Ili unywe maji yako vizuri asubuhi yaandae kabla ya kulala.
Tano, Fanya Mazoezi au Ingia Bafuni Uoge.