Watanzania wangependa kuona kazi nyingi za ujenzi wa barabara zikifanywa na mandarasi wazalendo. 

Rais John Magufuli, akiwa Waziri wa Ujenzi, alikuwa mstari wa mbele kuhimiza umoja, weledi na kujituma miongoni mwa makandarasi wazalendo ili waweze kufanya kazi ambazo kwa muda mrefu zimeshikwa na makandarasi wageni. 

Hili ni jambo jema, na kwa kweli Serikali inayowajali watu wake, haina budi kufanya hivyo.

Wamekuwapo makandarasi wazalendo kadhaa ambao ni dhaifu; na ni hao hao huwa mstari wa mbele kulalamikia Serikali kwa kuwapa kazi nyingi na nono makandarasi watokao ughaibuni.

Mimi si mkandarasi, lakini macho tu yananifanya niwe na uwezo wa kuwakosoa baadhi ya makandarasi wazalendo. Kwa mfano, sidhani kama kuna Mtanzania anayeitakia mema nchi yetu anayeweza kuzipa kampuni za kizalendo kama zile zilizofanywa Kinondoni, hasa maeneo ya Polisi Mabatini, au Kijitonyama! Kazi ziliyofanywa hapo zinatosha kushusha hadhi ya makandarasi wazalendo.

Kumekuwa na sababu kadha wa kadha za kuhalalisha udhaifu huu. Wapo wanaodai kwamba makandarasi wetu si wajuzi. Wapo wanaosema uchovu wa kazi zao unasababishwa na rushwa. Hapa inaelezwa kuwa ili kampuni ishinde zabuni, sharti wahusika watoe rushwa kwa wahusika katika ngazi mbalimbali. 

Inaelezwa kuwa mkandarasi aliyepitishwa anachofanya ni kujenga barabara iliyo chini ya kiwango ili walau afidie kile alichowapa watoa zabuni! Haya yanasemwa. Lakini kumekuwa na sababu nyingine zinazotolewa kuhalalisha kazi duni au ucheleweshaji miradi hii ya barabara.

Kwa maudhui ya makala hii, napenda nijadili mkandarasi-kampuni ya Gemen Engineering inayojenga kipande cha Butiama katika barabara ya Makutano-Nyamuswa-Ikoma Gate.

Kwanza nitangaze maslahi kuwa naguswa mno na barabara hii kwa sababu Butiama ndiko nyumbani, kwa hiyo haya nayaandika kwa hisia kali.

Kampuni ya Gemen, siijadili kwa sababu ya kuchelewa kuukamilisha mradi huu, la hasha. Kuijadili kwa jambo hilo kunaweza kuwa ni kuionea kwa sababu kasi ya ujenzi mara nyingi imechangiwa na namna Serikali inavyomlipa mkandarasi.

Naijadili kampuni hii na wahandisi wa Wizara ya Ujenzi kwa sababu sidhani kama kweli kuna wataalamu wa maana wanaostahili kujenga barabara kubwa na yenye hadhi kama hii. Sina hakika na uwezo wa vifaa vyake, lakini shaka iliyopo ni weledi wa wataalamu wetu. Butiama sasa ni wilaya. Ina wahandisi na wataalamu wengine wa barabara. Sidhani kama haya hawayaoni, na kama wanayaona, wamechukua hatua gani kuwajulisha wakubwa wao; na kama hao wakubwa wamejulishwa, nini kinaifanya barabara hii ijengwe kijima namna hii.

Badala ya kuifanya Butiama ifikike kwa urahisi, na pia ivutie hata machoni mwa wenyeji na wageni, barabara hii ‘dude’ la ovyo lililotibua mandhali ya Kijiji cha Butiama. Ashakum si matusi, hii inaweza kuwa ndiyo barabara ya ovyo kabisa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

Kijiografia, Kijiji cha Butiama kipo kwenye miinuko ya wastani, hali ambayo haimlazimu anayejenga barabara kuchimba mashimo makubwa kupindukia. Butiama hakuna maji ya kutuwama ambayo kwa akili tu ya kawaida yangeweza kuwa sababu ya kuchimbwa na hatimaye kujengwa kwa tuta refu kwenda juu ili kukabiliana nayo. Butiama haina ardhi oevu ya kumfanya mkandarasi ajenge tuta kubwa ili kuepuka kutitia au kusombwa kwa barabara. Hakuna.

Badala yake, mkandarasi amechimba milima kwa kile kinachoonekana kama anataka kuifanya barabara isiwe na mwinuko. Hataki madereva waendeshe kwa gea kubwa! Anataka wapite wakiwa na namba nne au tano! 

Katikati ya Butiama, mahali ambako wenyeji wanapaita ‘Stendi’, mkandarasi amejenga tuta refu mno kiasi kwamba aliye upande mmoja wa barabara hawezi kumuona aliye upande mwingine! Huu ni ukandarasi wa aina gani?

Ukiitazama barabara hii, halafu ukafikiria mkandarasi huyu huyu apewe kazi nchini Rwanda ambako kuna milima mikali, hupati picha.

Kana kwamba haitoshi, sasa ni miaka zaidi ya minne wakazi wa Butiama hawana fursa ya barabara za michepuko. Barabara hizo nyingi zilizokutwa na mkandarasi, ama zimevurugwa kwa kuchimbwa mashimo marefu, au zimezibwa kwa milima ya udongo. 

Mfano halisi ni wakazi wa Muhunda na Mutuzu tuliotumia barabara ya mchepuko ambayo kwa miaka miwili sasa imefungwa. Ufungaji huu si wa dharura, kwani inavyoonekana ni kama kazi imekwisha! Barabara kuu ya Mtaa wa Mutuzu imefungwa kabisa. Wananchi sasa wanalazimika kupita katika makazi ya watu wengine kwa tabu. Magari hayavuki kuingia au kutoka barabara kuu. 

Kwa wale waliofika Butiama wameona eneo likiwamo la Chifu Wanzagi, hali ikiwa mbaya zaidi. Kuna gema kubwa mno lililofifisha matumaini ya wakazi wa eneo hilo kuweza kuegesha magari katika viwanja vya nyumba zao. Si hivyo tu, bali barabara hiyo sasa ni hatari kwa maisha kwani endapo mtu atateleza, kupona ni majaliwa.

Jambo jingine baya, mkandarasi huyu na hao walioandaa mchoro wa barabara hiyo walipuuza kabisa kuukwepa mkuyu mkubwa mno katika eneo la Ryamahunda (Nyabisezo). Wakauua mti huo uliokuwa kielelezo kwa wageni waliozuru Butiama. Wazee walinung’unika. Hasira zao wakazionesha kwa kuamuru wananchi wasitumie mabaki ya mti huo kwa kuni au mkaa!

Hapa nikawa nimekumbuka tukio moja la wana mazingira katika Hifadhi ya Taifa Serengeti. Kampuni moja iliyokuwa imeandaa mchoro wa hoteli, baadaye ilibainika kuna mti mkubwa ungeng’olewa kupisha ujenzi. 

Kwa kuthamini miti mikubwa, wataalamu (Wazungu?) wakapinga kukatwa kwa mti huo. Ikabidi uandaliwe mchoro mwingine. Kitendo hicho kiliweza kuchelewesha ujenzi wa hoteli kwa miaka miwili hivi! Utaona namna wenzetu wanavyothamini miti. 

Mswahili yeye akishapewa kazi ya kufanya upembuzi, haangalii kuna nini mbele, na hata mkandarasi akifika eneo la kazi akaona mti mkubwa namna hiyo, hawezi kuonesha huruma. Kwake, kuua mti wenye umri wa miaka 200 ni rahisi zaidi kuliko kuifanya barabara iwe na kona ili kuukwepa. Nadhani pale Mbuyuni, Dar es Salaam aliyeandaa mchoro wa barabara hakuwa mswahili, kwani vinginevyo ule mbuyu leo usingekuwapo!

Ukiitazama barabara hii ya Butiama unashindwa kabisa kuamini kama kweli wataalamu wetu wazalendo wanastahili kupewa kazi kubwa kama hiyo.

Barabara imekuwa kero badala ya kuibua faraja kwa wakazi na wageni. Barabara imeitenga Butiama katika pande mbili kwa kutumia gema kubwa lililowekwa katikati ya kijiji (ambako sasa ni mjini-makao makuu ya wilaya). Hakuna barabara za mchepuko. Barabara haikamiliki. 

Nitakuwa wa mwisho kuamini kama kweli makandarasi wazalendo wanastahili kupewa kazi kubwa na za maana kama hii ya ujenzi wa Barabara ya Makutano-Ikoma (sehemu ya Butiama). 

Pengine kabla ya kufikia hatua ya kuwekwa lami, ni vizuri mabingwa kutoka Wizara ya Ujenzi wakafika Butiama kuona aibu hii na kuirekebisha. 

Kwangu mimi, hii ndiyo barabara ya ajabu kabisa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati. Bado hatujachelewa. Wahusika wanaweza kufanya marekebisho.