Na Deodatus Balile
Tangu Urusi ianze mashambulizi dhidi ya taifa la Ukraine, nimekuwa na ufuatiliaji wa karibu wa mashirika mbalimbali ya habari ya kimataifa. Kuna jambo gumu nimejifunza. Nimekuwa nikilisikia hili nililojifunza, ila sasa nimejifunza kwa njia ngumu.
Sitanii, miaka yote niliamini misingi ya Uhuru wa Vyombo vya Habari tunayofundishwa na wakubwa hawa wanaiishi. Kumbe hakika sivyo. Februari 24, 2022 Urusi ilipoanzisha mashambulizi, zilitoka taarifa huru zikasambaa dunia nzima juu ya mwenendo wa vita.
Tulishuhudia manuari za Urusi, ndege za kivita na askari wa nchi kavu wakiishambulia Ukraine kutokea majini, ardhini na angani. Miji kadhaa ikatangazwa kuwa imetekwa. Mji wa pili kwa ukubwa, Kharkiv, nao ukatajwa kuwa umetekwa.
Saa 24 baada ya picha hizo kurushwa, mwelekeo ukaanza kubadilika. Mashirika makubwa kama BBC, CNN, Aljazeera na mengine yakageuza mwelekeo. YouTube wakatangaza kufungia mitandao ya Urusi na Televisheni ya Taifa ya Urusi – RT.
Ghafla tukaona “Ukraine inapata nguvu kupitia vyombo vya habari vya Magharibi”. Ghafla tunapata taarifa za askari 190,000 wa Urusi kuzidiwa nguvu na raia 18,000 wa Ukraine. Nasema raia 18,000 kwa sababu Serikali ya Ukraine imeona jeshi halitoshi na ikatangaza kugawa bunduki kwa raia 18,000. Hawana mafunzo ya kijeshi.
Tangu siku ya tatu, tunaambiwa habari za upande mmoja. Kiev tuliyoambiwa awali ingetekwa ndani ya saa 1, na kwamba viwanja vya ndege karibu vyote vilikuwa vimetekwa na Urusi, sasa tunaambiwa iko huru. Tunapewa takwimu za vifo vya askari wa Urusi.
Sitanii, kwa sasa tunaonyeshwa vifaru viwili, vitatu vya Urusi vilivyodunguliwa. Tunatangaziwa kuwa Ukraine wameua askari 4,300 wa Urusi. Hadi sasa kwa taarifa zinazotangazwa na BBC na CNN ambazo kwa bahati mbaya zinafanana neno kwa neno, zinaonyesha hakuna askari hata mmoja wa Ukraine aliyeuawa. Akili za kuambiwa, changanya na zako.
Wamesahau hata wale askari waliouawa wakatuonyesha waliokuwa katika Kisiwa kinachofahamika kama Snake Island. Ambao meli ya vita ya Urusi ilifuta wakazi wote wa kisiwa hiki katika uso wa dunia. Matangazo yanayoendelea sasa yanaonyesha wananchi 210 wa Ukraine ndio wameuawa na majeshi ya Urusi.
Vyombo hivi vya habari vya Magharibi vinasahau kuwa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, ametamka mara kadhaa kuwa muda wowote maisha yake hapa duniani yatakoma kwa kuuawa. Marekani wamempa fursa ya kumwondoa Ukraine na kumpeleka mahala salama, yeye akasema anataka silaha si kusafirishwa nje ya nchi. Ukraine inaendelea kupata ushindi mkubwa kupitia vyombo hivi vya habari!!!!!
Sitanii, Afrika tunapaswa kuamka katika habari tunazolishwa kutoka vyombo vya Magharibi. Kwa sasa vifaru na mashambulizi yanayofanywa na Urusi havitangazwi popote. Habari katika mashirika haya makubwa zimekuwa za upande mmoja.
Wote wanaonyesha kumshambulia Urusi. Wanatangaza habari za anga kufungwa kwa ndege za Urusi, ila hawatangazi habari za kulipuliwa kwa bomba kubwa na hifadhi ya mafuta nchini Ukraine. Hawatangazi hatari inayolikabili Bara la Ulaya kuwa Urusi ndiye muuzaji wa mafuta namba mbili duniani na muuzaji wa gesi namba moja duniani.
Hawaelezi tena hasara wanayokwenda kupata nchi kama Ujerumani na nyingine za Ulaya zinazotegemea gesi kutoka Urusi kuendesha viwanda vyao na kuwapatia wananchi wao nishati majumbani. Kinachoangaliwa sasa ni siasa za Ubwanyenye na Ujamaa. Nchi za Magharibi zinapambana kupata furaha ya kuiangusha Urusi.
Hiyo Ukraine inayopiganiwa ilimegwa kutoka Urusi mwaka 1991. Nchi za Magharibi zinadaiwa kujitanua kwenda Ulaya Mashariki na hili ndilo analolipinga Rais Vladimir Putin. Anawaambia wakae huko waliko, wao wanasema wanataka kuiingiza Ukraine kwenye Umoja wa Kujihami wa Nchi za Magharibi (NATO).
NATO ilianzishwa mahususi mwaka 1949 kuupinga Umoja wa Kisovieti, uliokuwa unaongozwa na Urusi. Hapa kinachopambaniwa ni umiliki wa rasilimali gesi na mafuta kwa gharama ya kuua wananchi wa kawaida.
Sitanii, kama si ubabe, nchi hizi zingeweza kushirikiana zikatumia rasilimali hizi zinazogombewa kwa pamoja, ila umimi una nafasi kubwa kuliko upendo. Umefika wakati wa kumgeukia Mungu. Tuombe wakubwa hawa wafahamu kuwa ipo siku sote tutatoa hesabu za matendo yetu mbele ya Muumba wetu.
Nahitimisha makala yangu kama nilivyoianza kuwa, kwa vyovyote iwavyo, sijaona weledi, mizania na umahiri kwa jinsi vyombo vya Magharibi vinavyoripoti vita ya Urusi na Ukraine kwa kuandika habari za upande mmoja. Tuombe Mungu aiepushe dunia dhidi ya balaa la nyuklia.