Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Njombe
Jumla ya vitambulisho vya Taifa 369,002 vimezalishwa katika mkoa wa Njombe na kufikia zaidi ya asilimia 95 kati ya vitambulisho 397,143 ambavyo wananchi walijiandikisha na tayari vimeshaanza kusambazwa kwenye ofisi za maofisa watendaji wa kata.
Ofisa usajili mamlaka ya vitambulisho vya Taifa Nida mkoa wa Njombe bwana Makene Mgeni Mbele ya vyombo vya habari anasema zoezi la usambazaji vitambulisho hivyo limeanza na ifikapo machi 20 mwaka huu wananchi wafike katika ofisi za maofisa watendaji wa Kata kuvichukua.
Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama na mkuu wa Wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa anaagiza kupelekwa haraka kwa wananchi vitambulisho hivyo kwani wananchi wamekuwa wakiulizia kwa muda mrefu.
Aidha Kasongwa anawaonya wale wote wenye nia ovu dhidi ya vitambulisho vya watu waliofariki ambapo anasema atakaethubutu kuchukua kitambulisho cha mtu atakumbana na rungu la sheria
Baadhi ya wananchi mkoani Njombe akiwemo Denis Fute na Josephine Msongela wanakiri kupata vikwazo katika kupata huduma katika maeneo mbalimbali kwa kukosa kitambulisho cha NIDA Huku walionavyo wanasema vimekuwa muhimu katika masuala mengi.
Changamoto za kucheleweshwa kwa vitambulisho vya Taifa zimekuwa mwiba mkali kwa mamlaka husika kutokana na malalamiko mengi ya wananchi wakidai ucheleweshwaji huo umewakwamisha pakubwa katika utafutaji riziki na maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla